Maamuzi mabaya katika mchezo wetu dhidi ya Azam Fc
Klabu inachukua nafasi hii kuujulisha umma namna inavyosikitishwa na baadhi ya matukio yanayoendelea kujitokeza katika baadhi ya michezo ya ligi kuu Tanzania inayokamilika tarehe 19/04/2014.
Katika mchezo huo wa tarehe 13/4/2014 uliochezwa uwanja wa sokoine jijini Mbeya tulishuhudia timu yetu ikichezeshwa vibaya sana na waamuzi wa mchezo husika,Waamuzi hao ni muamuzi wa kati Nathani Lazaro(Kilimanjaro),Abdallah Uhako AR1(Arusha) na Godfrey Kihwil AR2 (Arusha). Waamuzi hawa kwa makusudi waliamua kuuharibu mchezo huo kwa kufanya maamuzi mengi mabaya na yenye utata kwa maslahi ya timu pinzani yetu siku hiyo.
Baada ya mchezo husika klabu ilitengeneza jopo la watalaam wa sheria na taratibu zinazosimamia mchezo wa soka ili waishauri kwa kile kilichoonekana siku ya mchezo huo kuhusiana na tafsiri ya sheria za mchezo toka kwa waamuzi hao. Kwa ufupi tunasema hivi:
1. Nidhamu ndani na nje ya uwanja ni msingi wetu mkuu na tumekuwa tukisimamia muda wote,kwa upande wetu nidhamu si swala la kufundishwa wala kukumbushwa na mtu,kwa namna muamuzi alivyoanza kuwatoa mchezoni kisaikolijia wachezaji wetu kwa maneno hasa katika kipindi cha kwanza hakuwa na nia njema na mchezo wetu siku hiyo,wakati wa kuelekea mapumziko wachezaji wetu walimshihi aamue kwa haki ili asiwe sababu ya kuharibu mchezo huo.Haijawah kutokea kama timu kumzonga muamuzi yeyote yule lakini kwa makusudi waamuzi wa mchezo husika walitengeneza mazingira ya kutufikisha hapo.
2. Utata wa penati,mchezaji wa Azam Fc alimuongopea muamuzi kuwa kafanyiwa madhambi ndani ya eneo la mita kumi na nane la gori la Mbeya City,muamuzi wa katikati aliiona fika sehemu sahihi ambako kosa lilifanyika lakini kwa dhamila yake mbaya akikimbia toka katikati ya uwanja alikwenda huku akiashiria kuwa ile ni penati wakati muamuzi msaidizi akiwa haoneshi hivyo,baada ya wachezaji wetu kugomea adhabu ya penati kwa mshangao muamuzi wa kati alibadirisha hata eneo stahili la adhabu ilipopaswa kupigwa.
3.
Utata wa goli la pili la Azam Fc,Hapa ndipo fumbo kubwa lilipodhihirika,mchezaji wa Azam Fc alifnya madhambi kwa kucheza vibaya na hivyo muamuzi msaidizi aliona na kuonesha kibendera juu,bado mchezaji wa Azam fc aliukuta mpira baada ya yeye kucheza vibaya dhidi ya mchezaji wetu,huku bado muamuzi msaidizi akiwa amenyoosha kibendera juu mchezaji huyo alifunga goli huku muamuzi wa kati akiona yote hayo, yeye muamuzi wa kati aliamulu hilo ni goli wakati muamuzi wa pembeni hakuashiria hivyo.Hapa napo ndipo sintofahamu kubwa ilipotokea.Goli hili lilikuwa la dhuluma.
4. Kwa ujumla waamuzi hawakuumudu mchezo kwa makusudi.
Klabu haiamini kuwa waamuzi hawa hawakuwa na uwezo ama sifa za kuchezesha mchezo ule,kama ingekuwa hivyo wasingeweza kufuzu katika majaribio mbalimbali ya kuwa na sifa za kuchezesha ligi kuu ila tunapata hisia kuwa waamuzi hawa walighiribiwa ili wachezeshe kwa faida ya wapinzani wetu.
Matukio ya aina hii yanaweza kuhatarisha amani katika viwanja vyetu,na kuupa tafsiri mbaya mchezo wa mpira wa miguu wenye wapenzi wengi waungwana.Hakuna jambo ambalo ni jema litokanalo na uhalifu,kama mamlaka husika nazo zitabaki kusema “huo ndio mpira wetu” basi mpira kwetu hautakuwa na maana.
Wapanga matokeo ni hatari kwa mpira wetu.
Wizi wa mapato ya milangoni
Kwa mara nyingine klabu imeshuhudia wizi mkubwa wa mapato ya milangoni,baada ya kupata matatizo kama haya katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar na Simba zilizochezwa Mbeya wakati wa mchezo dhidi ya Azam Fc tatizo hilo limejirudia tena.
Maandalizi ya tiketi yalifanyika vizuri lakini hadithi ya kuwa vitabu vilisahaulika kugongwa mihuri imejirudia tena,Si kweli kuwa vitabu vilisahaulka lakini klabu inapata hisia kuwa mchezo huu umeota mizizi na kuna watu wanaouratibu sambasamba na mfumo halali kwani risiti hizi ambazo hazikuwa na mhuri wa klabu ziliuzwa ndani ya mfumo wa uuzaji tiketi halali.
Klabu ilibaini vitabu vifuatavyo havikugongwa mihuri na viliuzwa ndani ya mfumo ulio halali zikiuzwa na wauzaji maarufu wa tiketi wa kila mechi ichezwayo Mbeya,Vitabu hivyo ni namba 06700,08700,11100,12800,13500 na 16600.Hivi ni vile ambavyo tuliweza kuviona hatuna hakika ni vingapi havikuonekana ambavyo tayari viliuzwa kama vilivyouzwa hivi.Pamoja na kuripoti suala hili kwa mafias wasimamizi wa kituo hakukuwa na dalili zozote za kushtushwa na hili.
Tumechoshwa na hali hii isiyokuwa na huruma kwa mapato madogo ya wachezaji wenye kipato kidogo.Tusipokuwa na dhamila ya dhati ya kuwadhibiti watu wenye njaa isiyokoma waliopo kwenye mpira wetu tutakuwa tunatengeneza baadhi ya timu ziitumikie timu zingine hivyo kuondosha dhana ya ushindani iliyojengeka msimu huu.Fedha itokanayo na mapato halali kama ya milangoni ni muhimu katika ujenzi wa timu imara na zenye ushindani ambazo zitaimarisha ligi yetu na hatimaye timu ya taifa imara,kuendelea kuufumbia macho wizi kama huu wa mapato ya milangoni ni kukaribisha maafa makubwa katika mpira wetu.
Wizi kama huu hauwezi kufanywa na watu baki zaidi ya wale wanaojua utaratibu mzima wa uandaaji na uratibu wa tiketi hizi.
Freddy Jackson
AFISA HABARI
MCC FC
18.04.2014
إرسال تعليق