Taarifa kwa vyombo vya habari, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa Paschal Mabiti,kuomboleza vifo vya watu 11

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone : 255-22-2114512, 2116898
E-mail : ikulumawasiliano@yahoo.com
E-mail : press@ikulu.go.tz
Fax : 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa Paschal Mabiti,kuomboleza vifo vya watu 11 ambao wamepoteza maisha yao katika ajali ya basi iliyotokea mkoani humo leo, Jumatatu, Aprili 21, 2014.

Katika salamu hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha  kuwa ajali zabarabarani zinaendelea kuchukua maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

“Nimepokea kwa huzuni nyingi taarifa ya ajali hiyo ambayo nimejulishwa kuwa imetokea katika Kijiji cha Itwimila katika Wilaya ya Busega katika Mkoa wako wa Simiyu wakati basi lililokuwa linasafiri kutoka Tarime, Mkoa wa Mara kwenda Mwanza kupitia Simiyu lilipoacha njia na kugonga nyumba kabla ya kupinduka.”

Amesema Rais Kikwete: “Nakutumia salamu zangu za rambirambi na najiunga nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa katika nchi yetu. Aidha, kupitia kwako, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa familia zote ambazo zimepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Naungana nao katika kuomboleza wapendwa wao. Napenda wajue kuwa msiba wao ni msiba wangu. Pia, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aziweke peponi roho za marehemu.”

Rais Kikwete vile vile ametoa pole kwa wote ambao wameumia katika ajali hiyo, akiwaombea wapone haraka na kurejea kwenye shughuli zao za kujiletea maendeleo.

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
21 Aprili,2014

Post a Comment

Previous Post Next Post