Tovuti ya Tume ya Jaji Warioba yafungwa....Viongozi wasema ilifungwa sanjari na tume,Katibu mkuu sheria asema anayetaka ufafanuzi aende wizarani


Siku chache tangu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ivunjwe baada ya kumaliza kazi yake ya kukusanya maoni na kuandaa Rasimu ya Katiba, tovuti yake nayo imefungwa rasmi.

Ukifungua tovuti hiyo iliyokuwa na taarifa mbalimbali muhimu zinazohusu tume hiyo na kazi zake, unakaribishwa na maneno kuwa inafanyiwa matengenezo, lakini habari zilizopatikana na kuthibitishwa na maofisa wa sekretarieti ya tume hiyo ni kuwa imefungwa.


Hivi karibuni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba wakati akitoa ufafanuzi wa hotuba yake bungeni, aliwataka wananchi kufuatilia tovuti hiyo kusoma randama ya Rasimu ya Katiba ili kupata maudhui, madhumuni, sababu za mapendekezo ya kila ibara ya rasimu hiyo.


“Tume inapenda kuwashukuru wananchi wote kwa shauku kubwa ya kutaka ufafanuzi wa mambo mbalimbali kuhusu Rasimu ya Katiba. Tunawaomba wananchi wasome Randama ya Rasimu ya Katiba ambayo kwa sasa inapatikana katika tovuti ifuatayo: www.katiba.go.tz,” ilisema taarifa ya tume hiyo kwa umma.


Juzi, Jaji Warioba hakupatikana kuzungumzia suala hilo baada ya na simu yake ya kiganjani kuita bila majibu.



Hata hivyo, aliyekuwa Naibu Katibu wa Tume hiyo, Casmir Kyuki alithibitisha kuwa tovuti hiyo imefungwa baada ya Tume kuvunjwa, kwa kuwa kusingekuwa na mtu wa kuiendesha.


Hata hivyo, katika tovuti hizo Randama ya Rasimu ya Katiba haikupatikana juzi.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Fanuel Mbonde alisema baada ya “Tume ya Katiba kufa na tovuti yake ilikufa papo hapo.”


Alipoulizwa kuhusu taarifa zilizokuwa kwenye tovuti hiyo, Mbonde alisema mtu anayetaka taarifa zozote aende wizarani.


Source: Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم