Jana Rais Jakaya
Kikwete, alitoa mwezi mmoja kwa viongozi wa TAA, kuweka mifumo imara ya
usalama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na wasipotekeleza
atawachukulia hatua.
Hali hiyo imesababishwa na
aibu iliyokwishatokea kwa Taifa, iliyotokana na kukamatwa kwa dawa za
kulevya katika viwanja vya ndege vya kimataifa, zikionekana kwamba
zimepita katika viwanja vya ndege vya hapa nchini.
Alisema hayo wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la
msingi katika mradi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria, kituo cha tatu,
cha JNIA ambalo pamoja na fursa zingine za kibiashara, litachochea ajira
mpya zaidi ya 7,000.
Rais Kikwete alionesha wazi kutoridhishwa na
hali ya usalama katika viwanja hivyo, na kuonya kuwa atawawajibisha
viongozi wa TAA wasipotekeleza agizo hilo, ikiwemo kuwafukuza kazi
wafanyakazi wote wanaotiliwa shaka kuhusika kupitisha dawa za kulevya.
Rais
Kikwete aliweka wazi kuwa ataanza kumwajibisha Mkurugenzi wa TAA,
Suleiman Said Suleiman na Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi hiyo, Lambert
Ndiwaita, wasipotekeleza agizo hilo.
Alisema kuwa maagizo anayotoa
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kuhusu usalama wa viwanja
hivyo ni maagizo yake hivyo yasipotekelezwa atawachukulia hatua.
"Suleiman
(Mkurugenzi wa TAA), nataka ufahamu kuwa maagizo yanayotoka kwa
Mwakyembe ni yangu, usipotekeleza nitaanza na wewe na Mwenyekiti wako wa
Bodi kwani nasononeka sana na hali hiyo ya kuacha wanamuziki wakipita
na dawa za kulevya huku wakiwaimbia," alisema Rais Kikwete.
Pia
aliomba apelekewe majina ya wafanyakazi wanaotiliwa shaka kupitisha dawa
hizo, ili awafukuze kazi yeye mwenyewe kwa kuwa mamlaka hayo ya
kuwaondoa bila kuwaonea haya anayo, na hakuna mtu atakayemuuliza wala
kumshitaki.
Alisema haiwezekani kuendelea na hali hiyo ambayo inamuumiza na ikiwa watendaji hao hawaumii, watachukuliwa hatua.
Amesema
kitendo cha dawa za hizo kupita JNIA na KIA na kukamatwa katika nchi
nyingine, kinasababisha Watanzania wote kuonekana wanafanya biashara
hiyo.
"Tusifanye masihara na usalama wa kiwanja chetu kwani kikiwa
njia ya kupitisha dawa za kulevya, tunaaibisha nchi yetu pamoja na
Watanzania wote.
"Hii siyo nzuri, mnaenda mbele na kurudi nyuma
(katika usalama), ni afadhali kuanza sasa na siyo kuamua kila siku bila
utekelezaji na sisi wote kuonekana tunafanya biashara hiyo," alisema
Rais Kikwete.
Alihadharisha kuwa Sheria ya Manunuzi isiwe kisingizio
cha kuchukua miaka miwili bila utekelezaji, kwani ikiwa sasa abiria
wanaopita katika kiwanja hicho ni milioni 2.5 wanashindwa kuwadhibiti,
itakuwaje kikikamilika kipya na kufikia milioni sita kama sio kuwa
biashara huru ya dawa za kulevya?
Alisisitiza ni vema mfumo huo wa
usalama ukaanza na JNIA na KIA ambako kumeonekana kuwa uchochoro wa
kuingiza dawa za kulevya nchini na kuhadharisha kuwa udhibiti ukifanyika
JNIA pekee, wafanyabiashara hao haramu watakimbilia KIA.
Rais
Kikwete alisema kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho cha tatu, kutatoa
fursa ya ukuaji wa uchumi kufikia wa kati ifikapo 2025 kwani kutakuwa na
ongezeko la idadi ya ndege, abiria na ongezeko la safari za ndani na
nje ya nchi.
Alisema usafiri wa anga kwa sasa siyo anasa, bali msingi
wa usafiri huo ni kuwa wa haraka na uhakika na pia ni mhimili mkubwa
katika sekta ya utalii na biashara.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete,
watalii wengi wamekuwa wakishindwa kufika katika nchi za Kusini mwa
Jangwa la Sahara kutokana na gharama kubwa ya usalama.
Alisema hata
gharama za usafiri huo kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni mara
mbili ya nchi za Ulaya kwa safari ya saa sita hivyo uwanja huo mpya
utasaidia kuboresha huduma, kuongeza biashara na kutokana na ongezeko la
watu watakaotumia uwanja huo, nauli itapungua.
Alisema atahakikisha Hazina wanasaini fedha zinazotakiwa haraka, ili jengo hilo likamilike kwa muda uliopangwa.
Awali
akizungumzia ujenzi wa kituo hicho, Suleiman alisema ujenzi wa jengo
hilo lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka na
miundombinu yake, linatarajiwa kugharimu Sh bilioni 518 mpaka
kukamilika.
Alisema mradi huo, unatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka
benki ya HSBC ya Uingereza kwa dhamana ya Serikali ya Uholanzi kupitia
taasisi ya Atradius na benki ya CRDB.
Suleiman alisema jengo hilo
litakuwa na ukubwa wa meta za mraba 70,000, sawa na mara nne ya jengo
lililopo sasa lenye ukubwa wa meta za mraba 15,000 na limeanza kujengwa
Januari mwaka huu na linatarajia kukamilika Oktoba mwakani.
Mbali na
kuchochea fursa za ajira kwa Watanzania wapatao 7,000, pia jengo hilo na
miundombinu yake, itatoa fursa ya kuegesha ndege aina zote ikiwemo
ndege kubwa kwa sasa duniani ya A380.
إرسال تعليق