
MKE wa marehemu Abeid Amaan Karume, Mama Fatma Karume aliwataka vijana kuyaenzi Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa kuacha chuki za ukabila, kidini ambazo zinaweza kuleta mgawanyiko wa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliyasema hayo katika Hitma ya Hayati Karume aliyeuawa kikatili Aprili 7 mwaka 1972 katika jengo la Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui pamoja na viongozi wengine wa chama cha ASP.
Katika mashambulio hayo aliyekuwa Katibu Mkuu wa ASP Shekhe Thabit Kombo alijeruhiwa kwa kupigwa risasi ya mguu.
“Vijana tuachane na chuki za ukabila na za kidini ambazo zinaweza kuleta mgawanyiko wa wananchi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania....tuishi kama walivyotuagiza wazee wetu,” alisema.
Hitma hiyo iliongozwa na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Shekhe Khamis Haji na kuhudhuriwa na viongozi wa kidini na serikali, akiwemo Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Katika maelezo yake, Mama Fatma alisihi vijana kuishi kama alivyofikiria muasisi huyo wa mapinduzi ya Zanzibar ya kutokuwepo kwa ubaguzi wa aina yoyote ile.
Alisema
ukombozi wa nchi ya Zanzibar umeletwa na Mapinduzi ambapo kabla ya hapo
hakuna mwananchi aliyekuwa na uwezo wa kumiliki ardhi kwa ajili ya
kujenga nyumba au shughuli za Kilimo.
“Tunapomkumbuka
hayati Karume basi tunatakiwa kuyaenzi yale mambo yote mema ambayo yeye
aliyasimamia kwa kipindi chote cha uhai wake,” alisema Mama Fatma.
Alisema
Karume alichukia chuki na ukabila zilizowabagua Waafrika katika nchi
yao, mambo ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yaliyosababisha kufanyika kwa
Mapinduzi ya mwaka 1964.
Naye
mmoja wa viongozi wa waasisi walioshiriki katika Mapinduzi ya mwaka
1964, Mzee Juma Ame (88) alisema utu wa Mwafrika ulikuwa huru kutokana
na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yaliyoongozwa na Karume.
Ame,
ambaye alipata kushika nyadhifa mbalimbali katika Chama cha ASP hadi
Chama Cha Mapinduzi, alisema Karume mara baada ya kushika hatamu ya
kuongoza dola, alitekeleza manifesto ya chama cha ASP ambayo iliweka
kipaumbele suala la wazalendo kumiliki ardhi ambayo ndiyo uti wa mgongo
wa uchumi.
“Karume
alitekeleza manifesto ya ASP kwa kugawa ardhi eka tatu tatu kwa wananchi
wa Unguja na Pemba kwa ajili ya kazi za kilimo na ujenzi wa nyumba
katika mwaka 1965,” alisema.
Naye
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, Makame Mzee aliwataka
Wazanzibari kuyaenzi yale mambo yote muhimu yaliyoasisiwa na Karume
ambayo yameleta manufaa makubwa wa Wazanzibari, ikiwemo Muungano.
“Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo mambo makuu ambayo Karume aliyapa
kipaumbele..... tulipofanya Mapinduzi mwaka 1964 tulikaa muda wa miezi
minne tu tukaungana na wenzetu wa Tanzania Bara na kuzaliwa taifa jipya
la Jamhuri ya Muungano,” alisema Mzee.
Katika
kisomo cha hitma kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu
wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali
Iddi, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano, Alhaji Ali Hassan Mwinyi
pamoja na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Aidha
katika kisomo cha hitma kilichohudhuriwa pia na wanawake akiwemo mjane
wa marehemu mama Fatma Karume, wake wa viongozi wakuu pamoja na wajukuu
wa marehemu.
Wakati
huo huo, vijana wa Chama Cha Mapinduzi wametakiwa kumuenzi rais wa
kwanza wa Zanzibar Abeid Amaan Karume kwa kufanya kazi na kuweka maslahi
ya taifa mbele.
Hayo
yalisemwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa vijana wa Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Khamis Juma wakati akifunga kongamano la
vijana wa Chama Cha Mapinduzi kuhusu wajibu wao na kumuenzi hayati
Karume.
Alisema
miongoni mwa taasisi ambazo zilipewa kipaumbele cha kwanza na Karume ni
Umoja wa Vijana wa ASP, ambapo aliamini kwamba vijana ndiyo nguvu za
chama imara watakaojenga taifa.
Aidha,
Sadifa aliwataka vijana kamwe kuacha kuyumbishwa na watu mbali mbali
wasioitakia mema Zanzibar pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ambao ni kielelezo cha taifa.
Alisema
miongoni mwa mambo ambayo yalipewa kipaumbele na Karume ni kuziunganisha
nchi mbili zilizokuwa huru na kuzaliwa kwa taifa jipya la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Aprili 26, mwaka 1964.
Alisema
faida za Muungano zinaonekana hii leo ambapo wananchi wa Zanzibar wapo
huru kuishi sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupiga
hatua kubwa za maendeleo na uchumi.
“Tunapomkumbuka
hayati Karume basi tunatakiwa pia kuuenzi Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ambao ni matokeo ya juhudi binafsi za mwasisi wa taifa
hili,”alisema.
Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar unatimiza umri wa miaka 50 ifikapo Aprili 26
mwaka huu, ukiwa Muungano wa kupigiwa mfano ulioweza kudumu duniani hadi
sasa.
Kongamano
la kumuenzi hayati Karume lilitayarishwa na Umoja wa Vijana wa Chama
Cha Mapinduzi kwa kushirikiana na ofisi ya mkoa wa Mjini Magharibi ya
chama hicho.
Katika
hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete
ameongoza wananchi mbali mbali katika hitma ya kumbukumbu ya kifo cha
Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume iliyofanyika katika Ofisi
Kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa.
Aidha
viongozi wakuu wa nchi waliweka shada la maua pamoja na wanafamilia wa
marehemu na waliokuwa waasisi wa mapinduzi walioshirikiana na marehemu.
Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliweka shada la maua katika kaburi la
marehemu lililopo pembeni mwa jengo la Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Aidha
Rais Kikwete aliweka shada la maua katika kaburi la marehemu ambaye hadi
anauawa alikuwa makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kiongozi
aliyeshiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar, Juma Ame naye aliweka shada
la maua katika kaburi la marehemu kwa niaba ya wazee walioshiriki katika
Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964.
إرسال تعليق