Waathirika wa mabomu yaliyolipuka Mbagala na kusababisha vifo na
uharibifu mkubwa wa mali za wananchi, wameibwaga Serikali mahakamani
baada ya kushinda pingamizi la Serikali dhidi ya kesi yao.
Waathirika hao ambao nyumba zao ziliharibiwa kwa
mabomu, wamefungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, dhidi ya
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.
Katika kesi hiyo ya madai namba 181 ya mwaka 2011,
wadai, Aulerian Temba, Athuman Mtauka, Elovan Agustino na Catherine
Isaya kwa niaba ya wenzao 76, wanapinga malipo ya fidia yaliyotolewa na
Serikali baada ya nyumba zao kubomolewa kwa mabomu hayo.
Wanadai kuwa malipo hayo ni madogo mno
kulinganisha na uharibifu uliotokea, hivyo wanaiomba Mahakama pamoja na
mambo mengine iwaamuru wadaiwa (Jamhuri) iwalipe fidia kwa mujibu wa
uthamini walioufanya kwa kumtumia mthamini binafsi.
Serikali iliweka pingamizi katika shauri hilo
ikiiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo kwa kuwa imefunguliwa
nje ya muda wa ukomo wa kufungua kesi ya madai.
Hata hivyo, jana Mahakama Kuu katika uamuzi wake
ilikubaliana na hoja za wadai kupitia kwa Wakili wao Edson Mkisi kuwa
kesi hiyo imefunguliwa ndani ya wakati na kwamba Jamhuri haikuainisha
sheria yoyote inayounga mkono pingamizi lake na hivyo kulitupa.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Dk. Fauz Twaib
anayeisikiliza kesi hiyo alisema pingamizi hilo la Jamhuri halina msingi
wowote kisheria. Hivyo aliamuru shauri hilo liendelee katika hatua ya
kupanga namna ya kuliendesha katika hatua ya usuluhishi, Mei 28, mwaka
huu.
Awali, Jamhuri iliwasilisha pingamizi hilo
mahakamani hapo, ikidai kuwa tayari wadai hao walishalipwa fidia yao,
lakini mahakama ilipoiamuru iwasilishe mahakamani hapo vielelezo vya
malipo hayo, ilishindwa kufanya hivyo kabla ya baadaye kurudi tena na
pingamizi hilo ambalo lilitupiliwa mbali jana.
Wadai hao wanadai kuwa malipo ya fidia waliyopewa
yalikuwa hayatoshi hata kununua mfuko mmoja wa saruji na wengine
walilipwa fedha ya kununulia mkate tu.
Wanadai kuwa kwa nyumba zenye thamani ya zaidi ya Sh50 milioni, kuna waliolipwa fidia ya Sh12,000 na wengine Sh1,200 tu.
Mabomu hayo yalilipuka Aprili 29, 2009 katika
Kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) KJ 671 na kusababisha vifo vya watu
zaidi ya 25, huku mamia ya watu wakijeruhiwa na familia nyingi kukosa
makazi baada ya nyumba zao kubomoka kabisa.
إرسال تعليق