Wajumbe hao waliondoka bungeni kwa mbwembwe
wakisusia vikao vya Bunge hilo na kudai hawarudi ng’o, lakini jana
baadhi yao walirejea kinyemela bungeni na kwenda moja kwa moja Ofisi ya
Katibu wa Bunge Maalumu, kudai posho za vikao ambavyo hawajashiriki.
Mwenyekiti
wa Bunge hilo, Samuel Sitta juzi mchana alitangaza bungeni kuwa,
amepata taarifa kuwa wajumbe wa Ukawa wamerudi lakini si katika vikao
bali wameonekana kwa Mhasibu kuchukua posho.
“Kuhusu hilo la Ukawa
kurudi, taarifa zilizonifikia hivi punde zinaeleza kuwa wamerudi, lakini
wameenda kwa Mhasibu kuchukua posho,” alisema Sitta na kusababisha
wajumbe waliokuwepo ndani ya Bunge hilo kucheka.
Baada ya Sitta
kueleza hivyo, alimkaribisha Mjumbe Adam Malima, ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Fedha, kutoa taarifa kuhusu hatua hiyo ya Ukawa kurudi
kuchukua posho.
Malima alisema utaratibu wa fedha zinazolipwa na
Serikali ni kwa wajumbe wanaokuja katika kazi za Bunge hilo na kuongeza
kuwa, Serikali haipo tayari kuwalipa watu ujira ambao hawajaufanyia
kazi.
“Tumezungumza na Katibu wa Bunge na kukubaliana kwamba, wote
wasio na mahudhurio malipo yao yasitishwe kwanza, hawawezi kuchukua
fedha wakati hawajafanya kazi, hili tunaiachia Kamati ya Uongozi ya
Bunge Maalumu,” alisema Malima.
Baada ya Malima kumaliza kutoa
taarifa hiyo, Sitta alisisitiza kuwa, wajumbe hao hawawezi kuchukua
fedha kwa kugoma kufanya kazi iliyowapeleka Dodoma.
Akizungumza na
mwandishi jana, Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hamad, alikiri kuwa
baadhi ya wajumbe wa Ukawa walirudi kuchukua posho lakini hakuwataja
majina.
Alisema juzi walitangaza wajumbe wajaze fomu kwa ajili ya
malipo yao na inavyoonekana, baadhi ya wajumbe wa Ukawa, kwa kujua
wahasibu hawawafahamu vizuri kama wapo bungeni ama ni miongoni mwa
walioondoka, walichukua fomu na kujaza kuchukua posho.
“Kabla ya
malipo yoyote, utaratibu wetu ni lazima wajumbe wajaze fomu za malipo,
jana (juzi) tulitangaza wajumbe wajaze fomu kwa ajili ya malipo, Ukawa
nao waliingia na kuna fomu walijaza, nimechukua orodha ya mahudhurio ili
kujua waliohudhuria.
“Nimeagiza asubuhi hii fomu zote niletewe,
ambaye hakuwa ndani hata kama si Ukawa ataeleza alikuwa wapi, kama
hakuwa ndani hatutamlipa mpaka Mwenyekiti (Sitta) aidhinishe kwamba
mhusika alikuwa na dharura ya muhimu akiwa Dodoma ndio atalipwa posho ya
kujikimu lakini si ya kikao,” alisema Katibu huyo.
Alisema mjumbe
yeyote atakayelipwa posho ya kikao ya Sh 70,000 ni aliyehudhuria kikao
na kujaza fomu lakini posho ya kujikimu ya Sh 230,000, italipwa kwa
mjumbe aliyefika Dodoma kwa ajili ya Bunge hata kama alipata dharura ya
kutohudhuria vikao kadhaa.
Kwa mujibu wa Yahaya, posho zinazolipwa ni
za kuanzia Aprili 19 mwaka huu hadi Aprili 26 na kwamba za kuanzia
Aprili 18 kurudi nyuma, zote zilishalipwa.
Hata hivyo, alifafanua
kuwa posho ya kujikimu pamoja na kwamba hulipwa mjumbe akiwasili Dodoma,
wapo wajumbe ambao hawajalipwa kutokana na kukosekana ufafanuzi wa
dharura zao lakini maelezo ya Sitta ya uthibitisho yakitolewa,
watalipwa.
Akizungumzia kuhusu uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Bunge
Maalumu iliyokuwa ikae Alhamisi iliyopita kujadili hatma ya posho za
wajumbe wa Ukawa, Yahaya alisema kikao hicho hakikufanyika.
Alifafanua
kwamba sababu ya kutofanyika kikao hicho ni kutokuwa na taarifa kamili
kwa kuwa Sitta aliomba kwenda Zanzibar, kukutana na baadhi ya viongozi
wakiwemo wa Ukawa kutafuta suluhu.
Katibu alisema Kamati ya Uongozi inaweza kukutana muda wowote kuanzia sasa kwa kuwa Sitta amesharejea bungeni.
Sitta
alikwenda Zanzibar Jumatatu wiki hii, ambapo pamoja na kukutana na
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ),
Seif Sharif Hamad, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi-CUF,
pia alikutana na Rais wa SMZ, Dk Ali Mohamed Shein na Rais mstaafu wa
Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Post a Comment