Kiongozi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP), Helen Clark, ameshauri wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,
waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kurejea kujadili
katika bunge hilo.
Akijibu
swali la waandishi wa habari jana, Clark ambaye ndiye kiongozi wa Shirika hilo
duniani, aliwataka Ukawa kutumia fursa ya Bunge Maalumu la Katiba kuipa nchi
Katiba bora, badala ya kuyumbisha mchakato kwa kususia vikao vyake.
Alisema
Katiba bora inawezekana kwa kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu, kinyume cha
hapo ni kudhoofisha nia njema ya Serikali ya kupatikana kwa Katiba mpya, akijibu
maswali ya waandishi wa habari aliokutana nao jana Dar es Salaam ili kutoa
tathimini ya ziara yake ya siku nne nchini.
Clark
ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand, katika mkutano huo na waandishi
wa habari wa kutoa tathimini ya ziara yake ya siku nne nchini, aliisifu
Tanzania kuwa ni nchi ya kidemokrasia inayopaswa kupigiwa mfano, huku akiitakia
kila la kheri katika mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.
Alipotakiwa
kutoa maoni yake kuhusu baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kususia
vikao vyake, Clark alionekana kushangazwa, lakini akatumia fursa hiyo kushauri
kundi hilo lililojitenga, kuunganisha nguvu ili kuipa nchi Katiba bora.
Alisema
Bunge Maalumu la Katiba ni mahali pekee ambako wazalendo wa kweli wanaweza
kujenga hoja nzito kwa lengo la kuhakikisha inapatikana Katiba bora.
“Kwa
maoni yangu kama ninayoyasikia ya kuwepo kwa kundi lililotoka nje ya Bunge la
Katiba ni kweli, nawashauri wabadilishe msimamo; kazi ya kutunga Katiba
inapaswa kuwa na wigo mpana, si wa makundi.
Kauli
ya Clark, kiongozi anayeshika nafasi ya tatu kicheo katika Umoja wa Matifa
baada ya Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, imekuja wakati kundi la Ukawa likiwa
limetangaza kuendelea kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba hata
litakaporejea tena Agosti 5, mwaka huu kwa awamu ya pili ya mchakato wa Katiba
mpya baada ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia kuongeza siku 60 zaidi.
Awali,
wajumbe hao walikutana kwa siku 70, lakini mchakato wake ulisuasua kutokana na
mivutano ya mara kwa mara, hasa kutoka kundi la Ukawa linaloundwa na baadhi ya
viongozi wa Kambi ya Upinzani na wafuasi wachache, kutoka katika kundi maalumu
la watu 201 walioteuliwa na Rais kwa ajili ya Bunge hilo.
Aidha,
Clark alitumia nafasi hiyo kuelezea kufurahishwa kwake na jinsi Tanzania
inavyoendesha uchaguzi katika nafasi mbalimbali za uwakilishi kwa ufanisi, hata
baada ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi.
“Tanzania
ni mfano wa kuigwa katika hili. Katika uchaguzi uliofanyika mara nne ndani ya
mfumo wa vyama vingi, hakujatokea tatizo la viongozi kushindwa kuheshimu ukomo
wa madaraka unaotajwa katika Katiba. Nawapongeza sana viongozi wa Tanzania kwa
kusimamia hili,” alisema.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema kama kweli Clark, ana nia ya
kutoa ushauri kwao, asingetoaushauri kwa waandishi wa habari ambao ni mtu wa
tatu, kwa kuwa kwanza hana hakika kama ni ushauri sahihi au umechakachuliwa.
Pili
alisema angetarajia Clark kama kweli anataka kutafuta suluhu, asikilize
malalamiko ya anaotaka kuwasuluhisha, ndio atoe ushauri badala ya kutoa ushauri
kama alivyofanya.
Katika
ziara yake, Clark pia alikutana pia na Rais Kikwete na kumpongeza kwa juhudi
anazofanya katika kupiga vita ujangili.
"Tunashirikiana
kwa karibu na Rais Kikwete katika suala hili la ujangili, lengo ni kuona
hatimaye tunafanikiwa katikla vita hii,” alisema Clark ambaye akiwa nchini
alitembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Mkuu
huyo wa UNDP ameendelea kuzitaka serikali duniani kote, kuongeza mapambano
dhidi ya ujangili wa tembo na biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori, kama
meno ya tembo.
Alisema
uhalifu unaotokana na biashara ya meno ya tembo, una madhara makubwa kwa watu
wanaoishi katika mazingira magumu katika nchi zinazoendelea kwa kuliibia Taifa
utajiri wake, kuharibu maliasili kwa ajili ya kizazi kijacho, kuchochea
uhalifu, rushwa na kudhoofisha usalama wa jamii na Taifa.
"Vitendo
hivi vya uhalifu vinawaweka wanawake, watoto na wengine katika hali ya
umasikini na maisha magumu na yaliyo na hatari," alisema.
Clark
alisema sheria zenye nguvu na zinazotekelezeka zinahitajika, ili kupunguza
mahitaji ya bidhaa haramu za wanyamapori na jamii kufanya shughuli za
kujiimarisha na kujipatia kipato Tanzania na nchi zingine zenye tembo na
wanyamapori.
Alisema
shirika lake limejizatiti kusaidia juhudi za kupambana na biashara ya
wanyamapori kwa kusaidia utawala bora, utekelezaji wa Sheria, kupunguza
umasikini na kulinda mazingira kwa kushirikiana na serikali na washirika wengine.
Kiongozi
huyo wa UNDP ameelezea kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na kuwaandaa
wanawake, vijana na walemavu kwa fursa zaidi za uongozi, hasa katika kipindi
hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka kesho.
“Tanzania
ipo mstari wa mbele katika ahadi ya kuboresha ushiriki katika siasa kwa makundi
yaliyotengwa kutokana na dhamira ya vyama vya siasa kufanya hivyo katika uteuzi
wa wagombea kuelekea uchaguzi wa mwaka ujao (2015),” alisema na kuelezea
alivyofurahishwa kukutana na wabunge wanawake mjini Dodoma, wakiongozwa na
Spika Anne Makinda.
Alisema
kutokana na dhamira ya kutaka kuona uchaguzi wa mwaka kesho nchini unafanikiwa,
UNDP imetenga dola za Marekani milioni 22 (sh bilioni 35.8) kwa ajili ya kuunga
mkono utoaji elimu kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Alisema
fedha hizo zitatolewa chini ya Mradi wa Uchaguzi unaoendeshwa na shirika lake.
Alisema shirika lake limepokea maombi kutoka vyama vya siasa kuomba kuungwa
mkono hususani kwenye suala la elimu, kujenga uwezo na uhamasishaji katika
shughuli za uchaguzi mkuu ujao.
Alisema
fedha hizo zitajikita katika kuelimisha na kuhamasisha wanawake na vijana
kujihusisha kwenye mchakato wa uchaguzi huo hususani kugombea nafasi za
uongozi.
Kiongozi
huyo wa UNDP, alipongeza Tanzania kwa hatua iliyofikia katika kutekeleza
malengo ya maendeleo ya millennia; hasa malengo namba moja, sita na saba.
Alisema
pia Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika juhudi za kutokomeza umasikini,
kuimarisha afya kwa watoto na kuwezesha watoto kuendelea na masomo hadi
sekondari.
إرسال تعليق