WAANDISHI WETU
IMEVUJA! Siku chache baada ya kifo cha mwongozaji na mwigizaji wa filamu
Bongo, Adam Philip Kuambiana, daktari mkubwa wa mastaa ameibuka na
kudai marehemu alijiua mwenyewe.
Waombolezaji wakiaga mwili wa marehemu Adam Kuambiana.
Kwa mujibu wa daktari huyo ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini
kutokana na maadili ya taaluma yao kuficha siri ya mgonjwa, siku moja
kabla ya kifo (Ijumaa ya Mei 16, mwaka huu), marehemu alimpigia simu na
kumwambia amekunywa dawa za malaria aina ya Fansidar lakini pia
amekunywa pombe.
Daktari huyo alieleza kuwa, marehemu alimpigia simu kumuomba ushauri juu
ya nini cha kufanya na kama kuna madhara yoyote juu ya pombe hizo na
dawa alizokunywa.
“Aliniuliza kama kuna madhara yoyote ambayo anaweza kuyapata kwa kuwa
alikuwa amekunywa fansidar kwa ajili ya malaria kisha akapata kiu ya bia
na kuamua kunywa,” alisema daktari huyo.

AMSHAURI KWENDA HOSPITALI
Akizidi kuzungumzia tukio hilo, daktari alikwenda mbele kwa kusema licha
ya msanii huyo kuwa na ‘masikhala’ mara kwa mara, lakini kwa kuwa
alimwambia jambo ambalo linahusu uhai wake, alimshauri kwenda hospitali
iliyo karibu ili akaonane na daktari kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa
kutoa sumu kwani kitaalam mtu anapokunywa pombe akiwa amemeza dawa za
aina hiyo vyote hugeuka kuwa sumu.

Alisema kutokana na jinsi alivyozidi kumsimulia hali aliyonayo, aliamini
kwamba marehemu alikuwa anamaanisha alichokuwa akikisema hivyo ikabidi
amsisitize kuwahi hospitali haraka.
“Nilimwambia awahi hospitalini haraka kwani nilijua fansidar ni kali na
si dawa ya kufanyia mchezo. Lakini kesho yake nilipopata taarifa za kifo
chake niliumia sana japokuwa nilijua amejiua kwa kuchangaya fansidar na
bia maana mchanganyiko wa sumu yake mwilini ni mkali sana,” alisema
daktari huyo huku akisisitiza kusitiriwa kwa jina lake.

MAZINGIRA YA KIFO
Kwa mujibu wa mtu ambaye alikuwa karibu na Kuambiana siku ya tukio
ambaye naye hakutaka kutajwa jina gazetini, marehemu asingekufa ghafla
kama tatizo alilokuwa nalo lingekuwa la vidonda vya tumbo ambavyo
vilikuwa vikimsumbua kwa muda mrefu.
“Siku ile marehemu alikuwa na pesa, alikunywa sana pombe kutoka asubuhi
mpaka usiku mwingi, alikuwa anakula kila anapojisikia sasa hatuelewi ni
kitu gani kilitokea maana haiwezekani mtu akutwe anaendesha na kutapika
damu pasipo kuwa na sumu mwilini,” alisema mtu huyo.
DAKTARI AWAASA MASTAA
Katika hatua nyingine, daktari huyo aliwashauri mastaa wengine kuwa
makini kwani mara kadhaa amepata kesi za namna hiyo ambapo wanakunywa
pombe vilabuni usiku huku wakiwa katika dozi ya ugonjwa fulani.

“Mimi nawaambia ndugu zangu, hasa mastaa waache tabia ya kunywa pombe
wakiwa katika dozi, starehe zipo tu. Ni vyema wakawa wanauliza kwa
wataalam wa afya pindi wanapokuwa wamemeza dawa za aina yoyote, nguvu ya
dawa inatofautiana kulingana na ugonjwa husika na muda wa kukaa
mwilini,” alisema daktari huyo.
DAKTARI MUHIMBILI ANENA
Ili kuzidi kupata undani wa mazingira ya kifo cha Kuambiana, Amani
lilimtafuta daktari mwingine mtaalam wa magonjwa ya binadamu wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Naye kwa sharti la kutotaja jina
alieleza madhara ya mtu kunywa pombe akiwa kwenye dozi.

“Unapokunywa dawa hususan hiyo fansidar, inakaa katika mwili kwa
takriban siku saba hivyo mgonjwa anapokunywa pombe ndani ya siku hizo,
pombe inapochanganyika na dawa katika mzunguko wa damu hugeuka kuwa sumu
na mgonjwa ana uwezekano wa kupoteza maisha endapo asipowahishwa
hospitalini,” alisema daktari huyo na kuongeza:
“Wengi huwa wanajisahau na kunywa pombe kabla ya siku saba lakini
wengine huwa wanakunywa pombe makusudi pale tu wanapoanza kupata ahueni
ya ugonjwa pasipo kutambua nguvu ya dawa bado ipo mwilini mwake na
madhara yake ndiyo hayo.”

JB AANGUKA GHAFLA, AZUA HOFU
Wakati shughuli za kuaga mwili zikiendelea juzi, Jumanne katika Viwanja
vya Leaders, Kinondoni jijini Dar, nguli wa filamu nchini ambaye
alikatisha ziara yake ya kikazi nchini Uturuki kwa ajili ya kuja kumzika
Kuambiana, Jacob Steven ‘JB’, alipewa kipaza sauti ili amzungumzie
marehemu ambapo akiwa katikati ya kuongea alianguka ghafla.

Umati wa watu uliokusanyika viwanjani hapo uliingia hofu na kushindwa
kuelewa amepatwa na nini lakini haikuchukua muda mrefu akasaidiwa na
watu na kuendelea na shughuli nyingine.
MASTAA WAONGOZA KWA VILIO
Mastaa mbalimbali wa Bongo Movies wakiongozwa na Wema Sepetu ‘Beautiful
Onyinye’, Aunt Ezekiel, Blandina Chagula ‘Johari’, Miriam Jolwa ‘Jini
Kabula’ waliongoza kwa kulia viwanjani hapo hadi walipofika makaburini,
Kinondoni.

Mbali na mastaa hao kuangusha vilio, Mkurugenzi wa Aset, Asha Baraka
alijikuta akishindwa kuaga kwa kuhofia kuuona mwili wa marehemu na kudai
huwa akitazama maiti anamuota kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Marehemu Kuambiana ambaye alikuwa nguzo muhimu katika ‘ku-dairekti’
filamu, alipatwa na mauti katika Gesti ya Silvarado, Sinza- Kwaremmy
jijini Dar. Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.

Imeandikwa na: Erick Evarist, Musa Mateja, Richard Bukos, Shani
Ramadhani, Deogratius Mongella, Chande Abdallah, Hamida Hassan, Issa
Mnally, Nyemo Chilongani na Mayasa Mariwata.
Credit:GPL
Post a Comment