Dodoma. Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid
Mohamed amesema anapanga kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais katika
Uchaguzi Mkuu mwakani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu hivi karibuni
mjini Dodoma, Hamad Rashid alisema: “Kama Mwenyezi Mungu akinijalia
uhai na uzima mwakani, ninatarajia kuingia kwenye kinyang’anyiro cha
urais ama wa Muungano au wa Zanzibar.
“Ila sijaamua kama ni Bara au Zanzibar; kama ni chama cha CUF au kingine, hayo yote yatakuja baadaye,” alisema Hamad Rashid.
Mohamed ambaye ana mgogoro mahakamani na chama
chake cha CUF, ametoa kauli hiyo wakati tayari viongozi wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), CUF kikiwamo wanajipanga kusimamisha mgombea
mmoja wa urais katika uchaguzi ujao.
Mbali na CUF, vyama vingine vinavyounda Ukawa ni
NCCR-Mageuzi na Chadema ambavyo pia vinakusudia kusimamisha mgombea
mmoja kwa nafasi za ubunge na udiwani, lengo likiwa kukabiliana na nguvu
ya chama tawala, CCM.
Hamad Rashid aliyekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu CUF,
alifutwa uanachama Januari 4, 2012 na Baraza la Uongozi la chama hicho
kwa madai ya kukihujumu kwa mujibu wa kifungu 63 (1) (j) na 64 (1-5) cha
Katiba ya CUF. Wengine waliotimuliwa pamoja na Hamad ni Doyo Hassan
Doyo, Shoka Hamis Juma na Juma Said Sanani.
Hata hivyo, Januari 10, 2012 Hamad Rashid na
wenzake waliiomba Mahakama iwatie hatiani wadhamini wa CUF, kwa kukiuka
amri ya Mahakama kutokana na uamuzi wa Baraza la Taifa la Uongozi la
chama hicho kuwafukuza uanachama wakiwa tayari wameweka zuio.
Baadaye Septemba mwaka jana, Hamad alikaririwa na
gazeti moja akisema suluhu yake na CUF haiwezi kupatikana kwa kuwa kuna
baadhi ya mambo ambayo hakubaliani nayo ndani ya chama hicho.
إرسال تعليق