NAHODHA wa zamani wa Taifa stars na kiungo wa Simba sc msimu uliopita, Henry Joseph Shindika amesema kwasasa ni mchezaji huru na anakaribisha klabu yoyote kufanya mazungumzo.
Katika mahojiano maalum na mtandao huu, Joseph amesema bado anahitaji kucheza soka nchini
Tanzania, japokuwa kuna mchakato anaufanya na kama atafanikiwa anaweza kwenda nje ya nchi.
“Nimemaliza mkataba Simba, naweza kucheza klabu yoyote ya hapa nyumbani, cha msingi ni kuzungumza juu ya maslahi”.
Joseph alisema Simba sc hawajazungumza na yeye kuhusu kuongezewa mkataba, hivyo timu yoyote itakayokaa mezani na kuelewana, atafanya kazi bila tatioz lolote.
Kiungo huyo aliipongeza TFF kuongeza timu mbili msimu wa 2015/2016, lakini aliongeza kuwa zinatakiwa kufika ishirini kwasababu kwa sasa ligi ni fupi sana.
“Sijui kwanini timu zipo chache, labda ni wadhamini, lakini nashauri ziongezwe zaidi. Tunamaliza ligi mapema mno, halafu hakuna mashindano mengine kama kwa wenzetu”.
Aidha, Joseph alisema bado anajiona yupo katika kiwango kizuri japokuwa hakuwa na namba ya kudumu katika klabu ya Simba sc.
“Nadhani ni mipango ya mwalimu. Mimi nilijiona kabisa ninaweza kuisaidia timu, lakini sikuwa na nafasi. Sijui kwa nini, nafikiri mwalimu anajua”. Alisema
Pia aliongeza kuwa wachezaji wengi wa Tanzania hawana uelewe wa mikataba yao, hivyo ni muhimu kutafuta mawakala au mameneja ili wachezaji wapate haki zao za msingi.
“Wachezaji wengi wanasaini tu mikataba bila kupitia vipendekele vyote. Watafutwe mawakala wazuri ili kuepusha kuvunjiwa mikataba bila kupewa haki zao”.
Akizungumzia ushindani wa ligi, Joseph alisema bado haoni kama wachezaji wanashindana katika mechi, hasa timu za chini.
“Nimecheza ulaya, utakuta timu ipo nafasi za mwisho, lakini wachezaji wanapigana mno kwa lengo la kupata ushindi. Hata kama watashuka daraja wanajua kuna timu zitawahitaji”.
“Ukija hapa nyumbani unakuta wachezaji wanaonekana kukata tamaa mapema”.
‘Pia masuala ya maslahi yamekuwa yakiwaathiri sana wachezaji wa ligi yetu”.
“Sisi ni watanzania na tunayajua maisha yetu. Utakuta mchezaji ana familia au ndugu, sasa kama halipwi hawezi kufanya kazi nzuri”.
“Wenzetu wanajituma sana hata kama kuna matatizo katika timu. Malengo yao yanakuwa mbali sana”.
إرسال تعليق