Ndugu
wanaHabari, Tunapenda mtusaidie kufikisha ujumbe wetu huu kwa umma
unaotokana na malalamiko na manung’uniko ya wanachama wenzetu wa CHADEMA
kuhusu udhaifu mkubwa wa kiuongozi unaoendelea kwa sasa chini ya
mwavuli wa UKAWA.
Kwa wiki kadhaa sasa, kumeibuka msamiati mpya wa kisiasa wa UKAWA
uliopelekea mpaka kuundwa kwa BARAZA KIVULI LA UKAWA pale Bungeni bila
kufuata Utaratibu.
Sisi viongozi ambao miongoni mwetu ni Wajumbe wa vikao halali vya
chama, ambavyo ni Baraza Kuu na Mkutano mkuu wa chama kutoka mikoa ya
Tanga, Pwani na DSM kwa masikitiko makubwa tunasema kuwa hatupendezeshwi
na mwenendo huu wa chama unaofanywa na viongozi wetu wakuu.
KUSUSIA BUNGE LA KATIBA.
Kwa namna ambavyo tumepambana kwa miaka mingi kudai na kuishinikiza
serikali kuridhia uandikaji wa katiba mpya, ni mpumbavu pekee anayeweza
kususia fursa ya uandishi huo tena kupitia chombo huru (BUNGE LA KATIBA)
kwa sababu tu ya mgongano wa kimaslahi.
Tunasikitika sana kuwaona viongozi wetu na wabunge wa chama chetu cha
CHADEMA wamesahau kazi tuliyowatuma ya kwenda kuandika katiba mpya
yenye kuzingatia maslahi ya wananchi badala yake wamekwenda kupigania
vyeo.
Tumefedheheshwa sana na namna ambavyo wawakilishi hawa wamekubali
kutanguliza mbele maslahi yao na kuyaacha maslahi ya wananchi ambao ndio
waliuowatuma, kwenye Rasimu yenye sura zaidi ya 18 ni uzezeta kususia
sura 2 tu za mwanzo kisa tu maslahi yao ya kugawana vyeo wanaona
hayawezi kutekelezeka.
Tunaomba ifahamike kwamba, hakujawahi kukaliwa kikao chochote halali
cha chama chetu kilichoazimia na kuwaagiza wajumbe wanaotokana na chama
chetu wasimamie katiba yenye SERIKALI TATU, na ikionekana haiwezekaniki
WASUSE NA KUTOKA NJE YA BUNGE.
Huu ni udhaifu unaotawaliwa na uroho wa madaraka, sisi kama viongozi
halali wa kikatiba wa chama hatujawahi kuwaza wala kuamua kuhusu ujinga
huu, siku zote tumekuwa tukiwasisitiza wajumbe wetu kwenye fursa yoyote
watakayoipata kwenda kusimamia mawazo na misimamo ya wananchi ambao ni
wanyonge,
Tunawatuma wajumbe wetu kuhakikisha tunapata katiba itakayosimamia na
kuzitunza Rasilimali zetu, na wala si kweli kuwa Idadi ya Serikali kama
ni 3 au 2 au 5 au zozote inaweza kuwa muarobaini wa changamoto zetu.
Daima dumu tumekuwa tukiamini kwenye mapambano ya Hoja ambayo ndio
msingi mkuu wa demokrasia ya kweli Tunayoisimamia kama CHADEMA.
Hivyo Basi tunasema, si sahihi hata kidogo kwa wajumbe wetu wa Bunge
la katiba kususia vikao vile na ndio maana hata baadi ya wabunge wengi
wa chama chetu wamekuwa wakilalamika chini chini kwetu sisi wajumbe wa
baraza kuu kwamba wamechoka sasa kuburuzwa na viongozi wakuu wa chama na
kwamba wao nao wana mawazo na misimamo yao, sasa kwa niaba yao pia
tumeona kama viongozi wa chama tulikemehe hili.
Nipo tayari kuyataja majina ya wabunge hawa wanaolalamika kuburuzwa
ambao ni zaidi ya wabunge 31 wa kuchaguliwa na wa viti maalum.
Muungano wetu huu wa UKAWA ni muungano wa kinafiki usiokuwa hata na
hadidu za rejea, hakunaga muungano duniani kote ambao waunganaji wake
wanaungana kiujanja ujanja tu kama walivyofanya viongozi wetu hawa.
Hatuungi mkono na tunawataka wasiendelee na upuuzi wao huu, warudi
bungeni kama hawataki wajitoe tuchague wabunge wengine
watakaowawakilisha wananchi wanaotuamini.
Ni sawa na ndoa ya mkeka, hakuna maridhiano, hakuna vikao, asubuhi
wapenzi jioni wana ndoa, ndoa ya namna hii kamwe haiwezi ikadumu hata
kidogo.
BARAZA KIVULI LA UKAWA.
Tunasikitika sana na kitendo cha mwenyekiti wa CHADEMA ndugu Freeman
Mbowe, kutufanya sisi wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu hatuna maana
kwenye kufanya maamuzi ya chama.
Walituaminisha kwamba CUF wamefunga ndoa na CCM na kwamba wao ni
sehemu ya serikali hivyo hawawezi kushirikiana na chama ambacho ni
sehemu ya serikali, kwa msingi huu tukaazimia kwenye vikao vya chama
ambavyo ni halali kwamba chama chetu hakitashirikiana na chama kingine
chochote cha siasa kwa kuwa ni washirika wa CCM na kwamba wao ni CCM-B
Tumemkashigu na kumtuhumu James Mbatia na NCCR nzima kuwa ni Tawi la
CCM na ndio maana hata Mbatia ameteuliwa kuwa Mbunge, inakuwaje leo
tunashirikiana na watu hawa ambao wanatumiwa na CCM?.
Ni lini Muungano wa CCM na CUF umevunjika rasmi?.
Ni lini ushirikiano wa NCCR ya MBATIA na CCM umekufa rasmi?.
Je mazingira yaliyofanya tuwahesabu wenzetu hawa kuwa ni CCM B leo
yamebadilika?, na kama yamebadirika yamebadilika lini na
yamebadilikaje?.
Je sio kweli kwamba tuliwatenga wenzetu na kuwakashifu kwa sababu tu ya uchu wa madaraka?.
Yaani sio kweli kwamba tuliwafedhehesha wenzetu hawa kwa sababu ya
UWAZIRI KIVULI?. Na leo tunawasafisha wenzetu hawa kwa UWAZIRI KIVULI
HUO HUO.
Kwanini viongozi wetu wanakuwa na UCHU na UROHO wa MADARAKA kiasi hiki?.
Kama tunaweza tukawaita wenzetu MASHETANI asubuhi na jioni tukawaita
MALAIKA kwa sababu ya UWAZIRI KIVULI, je tukipewa nchi na kushika dola,
si Tutawaita wenzetu majina mabaya zaidi?.
Si tutakuwa na serikali mbovu nay a ajabu zaidi ya hivi sasa tulivyo kwenye siasa za upinzani tu tulio nao?.
Kwa misingi huu, Tunaamini kuwa UKAWA ni UNAFIKI WA KISIASA, na
umebuniwa kwa sababu moja tu nayo ni kugawana vyeo, hakuna sababu yoyote
yenye mantiki iliyopo kwenye uundwaji wa UMOJA huu na ndio maana hauna
hadidu za rejea wala hauna hati za makubaliano miongoni mwetu.
Napenda kuwaambia watanzania kuwa sisi baadhi yab wajumbe wa Baraza
kuu na mkutano mkuu wa mikoa ya Pwani, Dsm na Tanga hatuungi mkono
upuuzi wowote wenye lengo la kusimamia ugawanaji wa vyeo na madaraka,
watu wa namna hii tunawaita WALAFI wa MADARAKA.
Tunaunga mkono watanzania wote wanaoitakia heri Tanzania yetu.
Mungu ibariki Tanzania
Imeandaliwa na Baadhi ya Wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Mikao ya Pwani, DSM na TANGA
na kusomwa na Joseph Yona Patrick ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA WILAYA YA TEMEKE,Mwenyekiti wa BAVICHA mkoa wa TEMEKE
MJUMBE WA BARAZA KUU CHADEMA TAIFA,MJUMBE WA MKUTANO MKUU CHADEMA TAIFA na MJUMBE WA KAMATI YA UTENZAJI BAVICHA TAIFA.
Post a Comment