Hiki Ndicho Alichomaanisha Profesa J katika Kipi Sijasikia


Imeandikwa na Evance Ng'ingo
AAH, niliacha kazi nifanye muziki wakatabiri nitalosti, Jina langu limeshatumika sana kutajirisha watu, Yalisemwa mengi demu wangu alipotoroka, Nimepita mengi, mitihani ya kila namna ndio maana nisishangai wakiniita mbebe lawama, Kote mlikobana kidume ndio natusua, Walishazusha nimekufa eti nimepata ajali washindwe na walegee, Wakasema nina Ukimwi kwa kuwa nilikonda ghafla,  Wanataka kunizika mzima kabla sijafa,  Waliosema nina ngoma wengine tumeshafukia, Na bado wanachonga sana but men the King is here.

HIYO ni baadhi ya mistari ya wimbo unaotamba kwa sasa kwenye vituo mbalimbali vya redio. Ni wimbo wa msanii mkongwe nchini, Joseph Haule ‘Profesa J’ uitwao Kipi Sijasikia.

Wimbo huo unazungumzia masuala mbalimbali yaliyowahi kusemwa kuhusu msanii huyo mkongwe. Wimbo huo alioshirikishwa Nassib Abdul ‘Diamond Platnum’ ambapo Profesa J anasikika akisononeshwa na watu ambao wamekuwa wakimshutumu mengi kuanzia maisha yake binafsi hadi kazi zake za muziki.

Wimbo huo umekuwa ukitumiwa kwa sasa kama wimbo wa ushauri kwa watu wenye kusemwa vibaya au kupakaziwa masuala mengi katika jamii. Akizungumza na gazeti hili, Profesa J aliyeanza kujishughulisha na fani ya muziki tangu miaka ya 1995, alisema aliutunga wimbo huo tangu mwaka 2011.

Profesa J akiwa mmoja kati ya waasisi wakubwa wa muziki huo, aliyeanza muziki akiwa na kundi la Hard Blasters, ni mmoja kati ya wasanii waliochangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha fikra za muziki wa Bongo Fleva nchini. Kupitia wimbo wake wa Chemsha Bongo wa mwaka 1998, alitoa elimu kuhusu vijana ambao wanategemea wazazi wao na kushindwa kujishughulisha kutafuta vipato vyao wenyewe.

Akaendelea kutamba zaidi hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, alipotoa nyimbo zake kama vile Bongo Dar es Salaam, Ndio Mzee na nyinginezo na kuwa mmoja kati ya wasanii wachache wa zamani ambao wanatamba hadi sasa. Kupitia wimbo huu wa Kipi Sijasikia ambao umetoka sasa katika vyombo vya habari, amegusa tena nyoyo za watu wengi hasa kwa kuzungumzia maisha yake.

Profesa J aliliambia gazeti hili kuwa moja kati ya vitu vikubwa vilivyokuwa vikimsumbua kwa muda mrefu ni kuambiwa kuwa ameathirika na ugonjwa wa Ukimwi. Anasema hali hiyo ilimfanya akose amani kwa muda mrefu tangu alipoanza kusikia mambo hayo. Anasema kuwa ikiwa ni kwenye mwisho mwa miaka ya 2000, ilipoanza kutolewa kwa tuhuma hizo, alijikuta akinyooshewa vidole na watu.

Anasema kuwa mwaka 2011, aliamua kutunga wimbo kuhusu mengine mengi aliyosikia akiambiwa kujihusisha nayo. “Najua kuna kipindi nilianza kuambiwa kuwa nimeambukizwa Virusi Vya Ukimwi huku hali hiyo ikielezwa kabisa waziwazi kutoka kwa watu wengine walikuwa marafiki zangu kabisa wa karibu,” alisema Profesa J.

Anaongeza kuwa katika wimbo huo, amegusia hilo hasa kwa kusema kuwa “Mlisema nimeathirika kutokana na kukonda ghafla, lakini wale mlionipakazia wengi wenu tumeshawazika.” Anasema kuwa kauli hiyo katika wimbo wake ni kweli kabisa inawagusia baadhi ya watu anaowafahamu kuwa walimtangaza kuathirika na wengi wao wamefariki kwa ugonjwa huo au matatizo mengine.

Anasema inasikitisha katika jamii kuona kuwa wapo watu ambao kazi yao ni kuwasema wengine kwa mabaya. Anasema mbali na kuwatangazia wenzao kuathirika, pia wanawatangazia ubaya zaidi kwa mambo mengine. Anasema kuwa hali hiyo imesababisha watu wengine kushindwa kuendelea na kazi zao za kawaida za kila siku kutokana na kunyanyapaliwa na watu katika jamii.

“Mimi nakwambia kuwa yupo mwanamama mmoja aliamua kujiua hivi hivi kutokana na kuambiwa kaathirika. Sasa ndugu yangu hata kama iwe ni kweli, sasa inakuwaje mtu anasakamwa kwa kiasi cha mwenyewe kuamua kujiua?” Alihoji Profesa J. Anasisitiza kuwa kutokana na hali kama hizo aliwahi kutunga wimbo uitwao Usinitenge ambapo ndani yake aligusia masuala nyeti kuhusu kunyanyapaliwa kwa waathirika katika jamii.

Profesa J ameendelea kugusia mengi katika maisha ya kawaida ya kila siku. Kuna ubeti anasema, “Kuna washkaji wengine feki wakipata dili hawakujui wamekariri kuwa kila jogoo akiwika ni asubuhi.” Akifafanua kuhusu ujumbe alioulenga katika wimbo huo, anasema wapo hata wasanii wengine ambao wakialikwa kwenye shoo nje ya nchi au hata hapa hapa nchini, wakiombwa namba za simu za wasanii wengine ili nao waitwe inakuwa ngumu kutoa.

Anasema hali hiyo ndio iliyomfanya kuwasema kuwa ni marafiki feki wakipata dili hawakujui na wanaona kuwa kila jogoo akiwika kwao ni asubuhi. Anawasihi wasanii hao kuona kuwa sio wakisikia kuwa wamepata dili la kazi za kulipwa na wao wakiona kuwa nyota imefunguka kwao basi ndio inakuwa hivyo hivyo na kwa wengine wao pia ni asubuhi.

Anasema kuwa hiyo ni moja kati ya vitu vinavyosababisha kushuka kwa muziki nchini kwa kuwa wasanii wengi ni wanafiki ambao wanalenga kuangushana. Anafafanua zaidi kuwa hiyo ni tofauti na wasanii wa Nigeria ambao kwa upande wao wanaungana mkono kwa kuoneshana mahala palipo na dili za muziki.
“Ukiona wasanii kama akina Davido wakija Tanzania wakaziona fursa, basi wakirejea tu makwao wanakuwa mstari wa mbele katika kuwaelezea wasanii wenzao pa kwenda kuchuma,” anaeleza Profesa J. Anawataka wasanii kujua kuwa Mungu ndio anatoa riziki na hakuna kwa namna yoyote ile mwanadamu kuzuia riziki hiyo.

Pia gwiji huyo aliyedumu katika muziki kwa zaidi ya miaka 20, anasema kuwa pia amewagusia watu ambao wanatumia jina lake kujiingizia fedha. Anasema kuwa wapo mapromota wanatangaza kwa wananchi kuwa Profesa J atakuwapo katika shoo zao, lakini inatokea kuwa kumbe hata kumwalika hawajamwalika.

Anaongeza kuwa hali hiyo imekuwa mbaya na inamtesa kwa kuwa wananchi wanatokea kumchukia kwa kudhani kuwa amewadharau na kwa upande mwingine promota anakuwa ameshajiingizia fedha. Wimbo huo umerekodiwa katika Studio ya Bongo Record na amemshirikisha Diamond kutokana na umahiri wake katika kuimba nyimbo za aina hiyo.

“Nimezushiwa mara nne kuwa nimekufa yani ilikuwa ni taarifa rasmi kabisa ambazo watu walinisema na iliniathiri pamoja na familia yangu yote na sasa utaona kuwa ni kwa kiasi gani hali ilivyokuwa mbaya,” alisema Profesa J. Akizungumzia ushirikishwaji wake katika wimbo huo, Diamond anasema kuwa ni wimbo wenye ujumbe mzito na unahusiana na maisha ya kila siku ya wanadamu.

“Sisi tunaimba muziki wa mapenzi zaidi, lakini wapo wanaoimba muziki wa kijamii kabisa na yale muhimu katika jamii na hapa Profesa amewakilisha rasmi Hip Hop na amekuwa akifanya hivyo kwa miaka mingi sasa,” anasema Diamond, mmoja wa wasanii nyota wa Tanzania kwa sasa.Crdt Habarileo
USIKILIZE HAPA CHINI

Post a Comment

أحدث أقدم