Mwanasheria na wakala wa wachezaji wa FIFA, Dkt. Damas Ndumbaro
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KUFUATIA uongozi wa Azam fc kumsainisha mkataba wa miaka miwili
kiungo mkabaji wa Yanga sc, Frank Domayo `Chumvi` akiwa katika kambi ya
Taifa ya Tanzania, mwanasheria na wakala wa kimataifa wa wachezaji
anayetambuliwa na shirikisho la soka duniani FIFA, Dkt. Damans Ndumbaro
amesema hakuna sheria inayozuia mchezaji kusainishwa mkataba akiwa kambi
ya timu ya Taifa.
Akizungumza na mtandao huu, Ndumbaro amesema sheria inaeleza
kuwa mchezaji anayetakiwa kusajiliwa na timu ni yule aliye huru baada ya
kubakiza miezi sita katika mkataba wake au ana mkataba, lakini klabu
inayomhitaji imezungumza na timu inayommliki mchezaji.
“Domayo ni mchezaji huru na alikuwa huru kwenda klabu yoyote”. Alisema Ndumbaro.
Pia alisema hakuna sheria inayosema kambi ya timu ya Taifa ni eneo linalozuiliwa watu kwenda.
“Kambi ya timu ya Taifa watu huwa wanaenda. Kumbuka Yondani
alisajiliwa Yanga akiwa timu ya taifa, na hatukusikia mzozo wowote
kwasababu hakuna kununi inayozuia hilo”.
“Kama
mchezaji ametoroka kambini ataadhibiwa kwa utoro, lakini kambi ya timu
ya taifa ni sehemu ya wazi na watu wanaruhusiwa kwenda pale na huwezi
kukataza watu kwenda pale”
“Kumbuka timu inakaa hotelini na hoteli huwa hawakai wachezaji tu, kila mtu anaweza kukaa pale”. Alisema Ndumbaro.
Kutokana na tukio lililotokea Aprili 30 mwaka huu kwenye kambi
ya timu ya Taifa (Taifa Stars) iliyopo Tukuyu mkoani Mbeya likihusisha
usajili wa Frank Domayo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Jamal Malinzi amemteua Wakili Wilson Ogunde kuchunguza mlolongo
mzima wa tukio hilo.
Baada ya kukamilisha uchunguzi wake, Wakili Ogunde ataishauri TFF kuhusu hatua za kisheria na kikanuni za kuchukua.
TFF ilitoa wito kwa wachezaji, klabu na wadau wa mpira wa miguu kufuata kanuni na taratibu katika utendaji wao.
Post a Comment