Kwa kawaida vijana wengi Afrika, hususan Tanzania wanapohitimu elimu ya juu, jambo ambalo hulifikiria ni kutafuta ajira.
Wengi huanza kuchakaza viatu vyao wakipita ofisi
moja baada ya nyingine kuomba nafasi za kazi zilizotangazwa na mwishowe
hujikuta wakiwa wamefanya usaili zaidi ya ofisi 10 pasipo kuitwa kazini.
Hata hivyo hii ni tofauti na msanii wa Hip Hop
kutoka Kundi la Weusi, Nickson Simon maarufu kama Nikki wa II ambaye ana
shahada ya Uzamili katika maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDMS).
Nikki wa II ambaye pia ni mshindi wa tuzo za
muziki za Kilimanjaro 2014 KTMA kupitia wimbo Bora wa Hip Hop “Nje ya
Box”, aliowashirikisha G Nako na Joh Makini wote kutoka Kundi la Weusi,
anasema licha ya kwamba amehitimu elimu ya juu na kupata alama kubwa,
hayupo tayari kuajiriwa.
Rapa huyu ambaye ni mdogo wa damu wa mwanamuziki
John Simon maarufu kama Joh Makini wiki hii ameachia wimbo wake mpya
“Sitaki Kazi” wimbo ambao umebeba maudhui makubwa yenye kutoa elimu kwa
vijana wa rika na elimu za aina zote.
Msanii huyu aliyeibukia katika fani mwaka 2008 na
wimbo wake “Good Boy” aliokuwa amemshirikisha Rama Dee, anasema hisia
alizonazo ndizo zilizomfanya atunge mistari ya wimbo huo, kutokana na
maisha halisi ya vijana wa sasa.
“Niliimba wimbo huu kutokana na kuwaona vijana
wengi wenye elimu ya juu wakihangaika kupita huku na kule na vyeti vyao
wakitafuta ajira, kwangu mimi naona ni utumwa kwa msomi kutegemea
kufanya kazi za watu wengine, badala ya kuibua cha kwako ili utoe ajira
kwa wengine,” anasema.
Hata hivyo anabainisha kuwa namba ya vijana
wanaohitimu stashahada, shahada ya kwanza na kuendelea inazidi kuwa
kubwa na ajira ni za kubahatisha.
“Ndani ya mistari ya wimbo “Sitaki Kazi” kuna
mistari inayoelezea namna kijana anavyoweza kutatua tatizo la ajira kwa
kubuni vitu mbalimbali ambavyo vitazalisha pato na kuweza kuajiri maelfu
ya vijana wanaohitimu mwaka hadi mwaka,” anasema rapa huyo.
Anasema ingawa nchi haina utaratibu maalumu wa
kuwaandaa vijana pindi watakapomaliza elimu zao, kuna haja ya kutafuta
ufumbuzi wa tatizo hili kwa vijana husika.
“Tatizo kubwa katika nchi yetu hakuna mtu au
utaratibu ambao unawaandaa vijana, lakini sisi wenyewe lazima tutambue
kwamba hii ni karne ya kutengeneza ajira yetu wenyewe, ndiyo maana
nimeimba wimbo huu ili kubadilisha mtizamo na fikra za vijana ambao
wanategemea ajira, ni lazima jamii ibadilike,” alisema Nikki wa II.
Nikki anasema katika usanii alionao anajivunia
kufanya kazi hiyo kwani ni kujiajiri inayomwingizia kipato kikubwa
ukilinganisha na ajira ya ofisini ambayo ingembana na asingeweza kupata
fedha ya ziada nje ya mshahara.
ZAIDI SOMA HAPA
ZAIDI SOMA HAPA
إرسال تعليق