JK, Mishahara kupanda paye kwenda singo digiti




 Rais Jakaya Kikwete, amewaahidi wafanyakazi nchini kuwa mambo mazuri yakiwemo ya kupanda kwa mishahara na kupunguzwa kwa kodi ya mishahara maarufu kama Paye.
Alisema hayo akihutubia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Dar es Salaam leo.
“Najua hiki ndio kilio chenu na wote mnasubiria kwa hamu Serikali inasema nini? Nawaahidi kuwa katika hotuba ya Bajeti Waziri wa Kazi na Ajira, itabainisha wazi, kiwango cha mshahara ambacho Serikali imekiongeza katika mishahara ya wafanyakazi,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, alisema Serikali haitoweza kupandisha mishahara hiyo na kufikia ombi la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA),  la Sh 750,000.
Pamoja na hayo, Rais Kikwete alionyesha kutoridhishwa na namna sehemu kubwa ya sekta binafsi, isivyozingatia viwango vya mishahara vinavyopangwa na Serikali, hali inayochangia kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara baina ya waajiri na waajiriwa.
Akizungumzia suala la Kodi ya Mapato (P.A.Y.E), Rais Kikwete, alisema ombi hilo nalo kama ilivyo nyongeza ya mishahara ni la muda mrefu, na kuwaahidi wafanyakazi hao kuwa nalo linafanyiwa kazi ili kupunguza kutoka asilimia 13 inayotozwa kwa sasa na kufikia tarakimu moja.
Naye Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, alimpongeza Rais Kikwete kwa kupatiwa tuzo ya utawala bora Afrika, na kuwataka waajiri nchini kutumia fursa hiyo kumuenzi kiongozi hiyo kwa kuhakikisha wanafuata nyayo na kusimamia utawala bora, ili kupunguza migogoro ya kazi.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya, akiwasilisha risala ya wafanyakazi katika maadhimisho hayo, aliiomba Serikali ishughulikie matatizo yanayowakabili wafanyakazi ya uboreshaji wa mishahara, kupunguzwa kwa kodi ya P.A.Y.E na kuboreshewe pensheni.






Post a Comment

أحدث أقدم