
Dar/Dodoma.
Meneja Biashara wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji
(Ewura) amekutwa amekufa hotelini katika mazingira ya kutatanisha muda
mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam akitoka Dodoma ambako
alihojiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Meneja
huyo, Julius Gashaza, ambaye alikuwa na jukumu la kupanga bei za mafuta
za kila mwezi, alihudhuria kikao hicho mjini Dodoma kwa siku mbili;
Ijumaa na Jumamosi iliyopita kuhusu mambo mbalimbali, yakiwamo kiwango
cha mafuta kinachoingizwa nchini, mgawo wa fedha unaotolewa na Ewura
kwenda kuhudumia umeme vijijini (Rea) na fedha za mfuko wa barabara.
Nyumbani
kwa meneja huyo wa Ewura, kulikuwa na waombolezaji waliokuwa kwenye
vikundi na kikao cha maandalizi ya mazishi kilifanyika ndani ya nyumba
ya marehemu iliyopo Yombo Vituka na baadaye kuhamia nyumba ya jirani.
Kamati ya
Bunge ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew
Chenge, ilikutana na maofisa wa Ewura, akiwamo Gashaza na wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) na kugundua kuwapo kwa tofauti katika takwimu za
kiwango cha mafuta kilichostahili kutozwa kodi.
Gashaza
alikwenda Dodoma kutoa ripoti ya Ewura kwenye kamati hiyo ya Bunge
akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kamati hiyo, takwimu za Ewura
ziliashiria kuwa fedha zilizopatikana ni nyingi zaidi ya zile
zilizoelezwa na TRA, lakini Wizara ya Fedha ilisisitiza zifuatwe takwimu
za mamlaka ya mapato.
Habari
hizo, zinasema baada ya kurejea Dar es Salaam juzi majira ya saa tatu
usiku, Gashaza hakwenda nyumbani kwake na badala yake alikwenda kwenye
hoteli iliyo karibu na nyumbani ambako mkewe na ndugu yake mmoja
walimfuata na akawaeleza kuwa anahisi kutishiwa maisha yake.
Baadaye walifanya maombi maalumu kabla ya kuachana naye.
Inadaiwa
kuwa marehemu aliomba akalale hotelini kwa sababu hakuona kama ana amani
kulala nyumbani kwake na ilipofika asubuhi alikutwa ‘amejinyonga’ ndani
ya chumba alicholala hotelini humo.
Nyumbani
kwa marehemu waombolezaji walikusanyika katika makundi, lakini baada ya
kukaa katika kikao cha familia walitoka na kauli moja kuwa hawatasema
chochote na kwamba jukumu hilo libaki mikononi kwa polisi.
Polisi wathibitisha.Chanzo Mwananchi
Post a Comment