Mkutano mkuu wa 30 wa kitaifa wa Jumuiya ya Tawala
za Mitaa Tanzania (ALAT), uliokuwa uanze leo jijini Tanga, umeahirishwa
kutokana na kuingiliwa na ratiba za Bunge la Bajeti lililoanza shughuli zake
mjini Dodoma jana.
Akitoa taarifa ya mabadiliko ya ratiba ya mkutano
huo, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari jijini Tanga, Mwenyekiti wa
ALAT Taifa, Dk Didas Massaburi alisema
mkutano huo, sasa utafanyika kuanzia Mei
13, mwaka huu.
Lengo la mabadiliko hayo ni kutoa fursa kwa baadhi ya wajumbe, wakiwemo kutoka Ofisi
ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambao
wanawasilisha bajeti zao sasa, kushiriki ipasavyo.
Mkutano huo wa siku nne, unaotarajiwa kufunguliwa na
Rais Jakaya Kikwete, awali ulipangwa kufanyika Mei 6 hadi 10 mwaka huu jijini
Tanga kwa kushirikisha wajumbe takribani 500.
“Tumewaita hapa ili kuwaeleza wananchi kuhusu
mabadiliko ya ratiba ya Mkutano wetu Mkuu ambao tumelazimika kuuahirisha kwa
sasa na badala yake utafanyika kuanzia Mei 13 hadi 16, mwaka huu hapa hapa Tanga.”
Dk Massaburi alisema na kuongeza, “Sababu ya kuu ya
kufanywa mabadiliko haya ni kama mnavyofahamu kwamba Jumuiya za serikali za
mitaa zote ziko chini ya Ofisi ya waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), sasa kulingana na
ratiba ya Bunge la Bajeti wao wataanza kuwasilisha bajeti zao wakati huu
(jana).”
“Hivyo isingekuwa jambo rahisi kwa Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda pamoja na Waziri wa Tamisemi (Hawa Ghasia) kuacha kuwasilisha
bajeti zao ili kuja kuungana nasi mkutanoni wiki hii,” alisema.
Akizungumzia Mkutano Mkuu huo Massaburi ambaye
ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam,
alisema pamoja na mambo mengine lengo la mkutano huo ni kuadhimisha kwa
kutathmini miaka 30 ya mafanikio ya jumuiya ya hiyo tangu kuundwa kwake Desemba
13, 1984.
إرسال تعليق