Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP ) ametaja ushirikiano wa
vyama vitatu vinavyounda kambi rasmi ya upinzani bungeni kwamba ni
ndoa ambayo kama wahusika wangekuwa na nia njema, ungeanza siku
nyingi tangu Chadema kilipounda baraza lake mwaka 2010.
Mwanasiasa huyo ambaye ameunga mkono kauli ya Spika Anne Makinda,
kwamba kambi hiyo rasmi ya upinzani imekumbuka shuka kunakucha, amekiri kwamba
haelekei na wala hapatani na wana Ukawa; lakini yeye ni mpinzani na
mzalendo wa kweli nchini.
Mrema alisema hayo juzi mjini hapa akizungumza na mwandishi wa
habari hizi. Alimjibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe ambaye
katika kutangaza Baraza Kivuli la Mawaziri juzi, alisema mbunge huyo hana
dhamira ya kuwa mshirika wa Ukawa na alishaweka wazi kuwa mshirika wa CCM.
Alitaja ushirikiano huo wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, kuwa ni
‘ndoa’ anayoiombea kila la heri na hawezi kuibashiria mabaya, isipokuwa
anachoona ni kwamba kama wangekuwa na nia njema, ndoa hiyo ingeanza siku
nyingi tangu Chadema ilipounda baraza mwaka 2010.
“Ushirikiano huu ni jambo lao, wanafikiri litawasaidia. Lakini
kwani hatujui walivyokuwa (CUF na Chadema) wakitukanana? Siwezi
kuwabashiria mabaya. Wangelikuwa wema, hiyo ndoa ingeanza siku nyingi,” alisema
Mrema.
Alisema yeye ni mpinzani ambaye kamwe hawezi kushiriki katika
mambo ya kubomoa nchi.
“Kwanza mimi sijaomba huo uwaziri kivuli. Hawa watu ni wa ajabu
sana... Mbona Maalim Seif (Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu
wa CUF), yuko kwenye Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar. Mbona CUF
hawaambiwi ni CCM?
“Kwanza ukinilinganisha na wao, naona wananionea wivu. Nimeshika
madaraka ambayo hawajawahi kuyashika. Mbowe hana sifa za kuniteua. Ana sifa ipi
sasa?.”
Mrema alitamba kuhusu nafasi za uongozi serikalini alizowahi
kushika, ikiwemo ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Kazi na Maendeleo
ya Vijana na Naibu Waziri Mkuu.
Alisema licha ya kuwa miongoni mwa watumishi waliotukuka, katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 akiwa NCCR Mageuzi, alipata kura milioni 1.8
ambazo kwa mujibu wake, hakuna mpinzani anayeweza kuzipata. “Na nilikuwa
NCCR Mageuzi. Si watu wangenikataa kuwa mimi ni CCM…Nani amewahi kuvunja rekodi
hii ya kura?” Alihoji.
Akiendelea kutamba kwamba hatishiwi na cheo chochote,
alisema aliamua kuachana na kile alichoita ‘biashara ya jumla’
akimaanisha kugombea urais na badala yake, akaingia kwenye ‘biashara ya reja
reja’ kwa maana ya ubunge.
Alisisitiza, “mtu aliyewahi kugombea urais, leo hii unanipa
uwaziri kivuli, si badala yake watanipa uwaziri giza?.” Hata hivyo alisema
kuachwa katika baraza hilo kivuli, si suala la
kushangaa, kwani hata
walipoliunda mara ya kwanza na kuwabagua CUF, pia yeye hakuwemo.
Akielezea mgogoro kati yake na Upinzani, Mrema alisema umekuwa
mkubwa katika Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na kutokukubaliana nao katika
mtazamo juu ya muundo wa Muungano.
Alisema katika Bunge Maalumu, wabunge walikubali kutengeneza
utaratibu endapo itatokea kutoelewana. Alisema ipo Kamati ya Maridhiano ambayo
iliundwa kuwezesha wabunge kuzungumza na kupatana pale itakapotokea hali hiyo.
Licha ya Kamati ya Maridhiano, alisema upo uongozi wa Bunge la
Katiba na isitoshe, suala lolote linalohusu bunge hilo, linapaswa lizungumzwe
ndani ya bunge hilo limalizike.
“Sasa wenzangu wakaamua kutoka nje mimi sikutoka nje. Ndio
naonekana eti mimi ni CCM. Eti niende Kibanda Maiti (Zanzibar); hivi
niking’atwa na nyoka Kibanda Maiti, nitawaambiaje wananchi wangu? Nilikuwa wapi
na nilikwenda kufanya nini,” alihoji.
إرسال تعليق