MTOTO AUWA WAZAZI WAKE WAWILI NA KUCHOMA MOTO NYUMBA MKOANI KILIMANJARO

WANANDOA wawili wameuawa kinyama baada ya mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Yusuf Njau (32),  anayeaminika kuwa ni mtoto wa wanandoa hao, kuwacharanga kwa shoka kisha kuchoma moto nyumba  yao na kutokomea kusiko julikana.
Tukio hilo la kusikitisha na la aina yake limetokea juzi majira ya saa 12:30 jioni katika kijiji cha Masama-Roo,  Kata ya Machame Mashariki, wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro baada ya kijana huyo kuchukua uamuzi huo ambao unadhaniwa ni sababu za ugomvi wa kifamilia. 

 
 
Waliouawa wametambulika kwa majina ya Shahidu Njau(60) ambaye  ni baba yake mzazi wa mtoto huyo na  Minae Swai (57) ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo ambao kwa pamoja waliuawa baada ya kupigwa na shoka katika maeneo mbalimbali ya mwili. 

Kwa mujibu wa Taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Halfani Swai alisema walipofika katika eneo la tukio baada ya kusikia ukunga, walikuta watu wakizima moto huku mwili wa Mama yake muuaji uliocharangwa na mapanga kila mahali ukiwa chini. 

Alisema kuwa wakati kijana huyo akiendelea kutenda unyama huo, alitokea baba yake mzazi, Mzee Shaidu  aliyekuja kuingilia kati ugomvi wa Mama na mwanae lakini naye alikatwa kichwani. 

Swali alisema Mwili wa Baba ulikutwa ukiwa pembeni wa mwili wa Mama ukiwa umekatwa kichwani na ubongo kufumuliwa lakini hata hivyo alikuwa bado hajafa. 

Alisema walimchukua kwa nia ya kuokoa uhai wake lakini muda mfupi baada ya kutoka kwenye eneo la tukio wakiwa katika kituo cha mafuta maeneo ya kwa Sadala Shaidu alipoteza maisha. 

"Tulikuta mwili wa Baba ukiwa pembeni nao ukiwa umejeruhiwa vibaya kichwani, ubongo ulikuwa pembeni, tulimchukua kumpeleka Hospitali lakini tulipofika kwa Sadala alipoteza maisha," alisema Swai.
 
Taarifa kutoka katika kijiji hicho zilisema muuaji, Yusuf Njau, ambaye amewahi kujifunza ngumi akiwa Dar es salaam amewahi kuwatishia Uhai baadhi ya ndugu zake zaidi ya mara mbili. 

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Halfani Swai alisema kuwa kijana huyo ambaye ni morofi sana aliwahi kutishia kuwaua Shangazi na Baba mdogo. "Muuaji aliwahi kuwatishia shangazi yake na Baba mdogo,amewahi kujifunza Ngumi na ni mkorofi sana kijijini kwake," alisema Swai.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema mtuhumiwa huyo katika tukio la kutishia kuuwa shangazi na Baba Mdogo alikatwa na kuachiwa. 

Alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Hai ambapo juhudi za kumsaka Muuaji anayedaiwa kuonekana akiranda kijijini hapo zinaendelea. 
Kwa upande mkuu wa wilaya ya Hai Novatus Makunga alisema tukio hilo ni kinyama na kuwataka wananchi kuwa na subira huku akitahadharisha raia kuchukua hatua mikononi. Makunga aliwataka Wananchi kuwaachia watu wa usalama kuchukua hatua huku akitahadharisha kuhusu jaribio la wananchi kuchukua hatua mikononi kuwa inaweza kuleta madhara zaidi. 

Wakati huo miili ya marehemu imezikwa jana mchana majira ya saa 7, kwenye makaburi ya Nyumbani, katika kijiji cha Masama Roo, Tarafa ya Masama, |Kata ya Machame Mashariki, wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
  Na Dixon Busagaga,Hai.

Post a Comment

أحدث أقدم