BAADA
ya kuwepo malalamiko ya wasichana wadogo wa nchini kusafirishwa kwenda
China kutumikishwa katika biashara ya ngono pamoja na dawa za kulevya,
sasa serikali imenasa mtandao huo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alitoa taarifa hiyo
juzi bungeni wakati akihitimisha michango kuhusu bajeti yake kwa mwaka
wa fedha 2014/15 iliyopitishwa.
Chikawe ambaye hata hivyo hakufafanua kwa undani wa mtandao huo
ulivyokamatwa, alieleza Bunge namna watoto hao wanavyopatikana kabla ya
kufikishwa nchi hiyo ya nje.
Kwa mujibu wa Waziri, watu hao wamekuwa wakichukua watoto wadogo na
kuwaambia kwamba wanawapeleka China hususani mji wa Guanzhou kuwaajiri
kwenye saluni na maduka.
Alisema kinara wa usafirishaji amekuwa akitambuliwa kwa jina la ‘Mama’
ambaye baada ya kufika nchini humo, huwanyang’anya watoto hao hati zao
za kusafiria. Imebainika zipo hata wakala zinazojihusisha na biashara
hiyo haramu ya binadamu.
“Wakifika, Mama anawanyang’anya pasipoti zao. Anawaambia ili
kuwarudishia, lazima watimize masharti ya kumpa kati ya dola 8,000 na
10,000 baada ya kutumika katika vitendo vya ngono,” alisema Waziri Chikawe.
Aliendelea kueleza kuwa wanaposhindwa kutimiza masharti hayo, hukutana
na Wanigeria ambao huwapa hati bandia za kusafiria na kisha kuwaingiza
katika biashara ya kusafirisha dawa za kulevya kwenda nchi mbalimbali.
“Tumenasa mtandao huu…polisi imenasa mtandao,” alisema Waziri na kutoa
mfano kwamba hivi karibuni, alikamatwa mtu akiwa na hati ya kusafiria
akimpelekea binti mmoja. Alisema binti huyo alipoulizwa juu ya hati
hiyo, alikuwa hafahamu anakokwenda.
Awali, taarifa juu ya kuwepo usafirishaji wa wasichana wadogo kwenda
China kwa ajili ya kutumikishwa katika ngono, ilitolewa na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe baada ya kutoka
ziarani nchini humo.
Membe alisema serikali inashirikiana na ubalozi wa China katika kubaini
wahusika wa biashara hiyo sanjari na mkakati wa kuhakikisha wasichana
hao wanarudishwa nchini.
Akielezea mikakati ya serikali katika kukabili biashara haramu ya
usafirishaji wa binadamu, Waziri Chikawe alisema katika mwaka wa fedha
2013/2014 Sekretarieti ya kupambana na biashara hiyo imeratibu vikao
vinne vya Kamati ya kupambana nayo.
Aidha imeandaa kitabu cha anuani na majina ya watoa huduma kwa
waathirika wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu na vilevile
kutengeneza rasimu ya kanuni za sheria ya kupambana na biashara hiyo
nchini.
Katika mwaka wa fedha 2014/2015 sekretarieti itakamilisha kutengeneza
kanuni za Sheria ya kupambana na biashara hiyo ya mwaka 2008. Pia itatoa
elimu na kuimarisha mikakati ya kupambana na biashara hiyo ya
kusafirisha binadamu.
Watanzania zaidi ya 100 wakiwemo wasichana 20 wamedaiwa wapo gerezani nchini China wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Post a Comment