Rais Jakaya Kikwete na Rais Goodluck Jonathan jijini Abuja, NIgeria leo.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo,
Alhamisi, Mei 8, 2014, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa
Nigeria, Mheshimiwa Goodluck Jonathan katika Hoteli ya Transcorp Hilton
katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Abuja.
Katika
mazungumzo hayo, Rais Kikwete kwa mara nyingine, amewasilisha rambirambi
rasmi za Tanzania, za Watanzania na za kwake mwenyewe kwa kiongozi huyo
wa Nigeria kufuatia vitendo vya kigaidi ambavyo vimeua maelfu ya watu
na wengine kutekwa nyara katika maeneo mbali ya nchi hiyo na hasa
kaskazini.
Rais
Kikwete pia ametoa pongezi nyingi kwa Rais Jonathan na wananchi wa
Nigeria kwa kuandaa Kongamano la Uchumi Duniani (WEF-Afrika) kwa Afrika
lenye mafanikio makubwa. Kongamano hilo lilianza jana na linamalizika
kesho mjini Abuja na Rais Kikwete amejiunga na viongozi kadhaa duniani
kuhudhuria Kongamano hilo.
“Mheshimiwa
Rais, nakushukuru sana kwa kupata muda wa kuja kujiunga nasi katika
mkutano wetu huu mkubwa. Kama ulivyosema wewe mwenyewe kuwepo kwako na
kwa viongozi wengine ni ishara muhimu kwa dunia kuwa nchi yetu, pamoja
na matatizo makubwa ambayo tunapitia, bado inaungwa mkono duniani na ina
usalama wa kutosha kuweza kuendesha mkutano kama huu,” Rais Jonathan amemwambia Rais Kikwete.
Naye Rais Kikwete amemwambia Rais Jonathan: “Tunakupogeza
sana Mheshimiwa Rais kwa kuandaa kongamano zuri hapa nchini kwako. Kama
unavyojua miaka yote makongamano hayo yalikuwa yanafanyika mjini Cape
Town, Afrika Kusini, mpaka sisi Tanzania tulipoandaa Kongamano la kwanza
nje ya Afrika Kusini. Siyo kazi rahisi, tunakupongeza sana.”
Rais Jakaya Kikwete katika mazungumzo na Rais Goodluck Jonathan jijini Abuja, NIgeria leo.
“Na
yale yanayoendelea katika nchi ni uendawazimu wa kiwango cha juu sana –
binadamu anao uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo ya ukatili wa hatari
kabisa. Hawa ni watu wasio na roho wala moyo. Ni ukatili wa kiwango cha
juu sana,” amesema Rais Kikwete.
Hata
hivyo, Rais Jonathan ameonyesha matumaini kuwa ugaidi huo unaweza kuwa
unaelekea mwisho hasa kufuatia uamuzi wa Marekani na Uingereza kuisaidia
Nigeria kukabiliana na hali hiyo. Ufaransa na China pia zimejitolea
kusaidiai.
Moja ya
mambo yanayoiwekea shinikizo Serikali ya Rais Jonathan kwa sasa ni
kutekwa nyara kwa watoto wa kike wa Sekondari zaidi ya 200 katika shule
moja kaskazini mwa nchi hiyo zaidi ya wiki tatu zilizopita. Mpaka sasa
hawajulikana walipo na kikundi cha Boko Haram ambacho kinapinga elimu ya
magharibi kimesema kinawashikilia watoto hao na kinataka kuwauza kwenye
utumwa.
Juzi,
Kikundi hicho ambacho kinafanya kila aina ya ugaidi kiliteka nyara watu
wengine wanane kutoka kijiji kimoja cha kaskazini mwa nchi hiyo na usiku
wa jana, kikundi hiki kilivamia vijiji kadhaa na kuua watu zaidi ya
300.
Post a Comment