Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametoa
salamu za rambirambi na pole nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Nigeria
Mheshimiwa Goodluck Jonathan na wananchi wa Nigeria kufuatia mfululizo
wa vitendo vya ugaidi ambavyo vimepoteza maisha ya maelefu ya wananchi
wa nchi hiyo na kutekwa nyara kwa mamia ya watu wakiwemo wanafunzi wa
kike wa sekondari.
Katika salamu zake za pole kwa Rais Jonathan, Rais Kikwete amesema: “Napenda
kutoa salamu za rambirambi na pole zetu nyingi kwako Mheshimiwa Rais na
wananchi wa Nigeria kufuatia mfululizo wa vitendo vya kigaidi ambavyo
vimepoteza maisha ya maelfu ya wananchi wa nchi hiyo na wengine kutekwa
nyara. Tumekuja kuonyesha mshikamano wetu na wananchi wa Nigeria.”
Rais
Kikwete ametoa pole hizo mwanzoni mwa hotuba yake kwenye mkutano wa
marais uliozungumzia umuhimu wa miundombinu ya kimkakati katika Afrika
ikiwa ni sehemu ya Kongamano la Uchumi Duniani (WEF) Afrika kwenye
Hoteli ya Transcorp Hilton mjini Abuja, Nigeria.
Akizungumza mbele ya Rais Jonathan na viongozi wengine wa Afrika, Rais Kikwete amemwambia kiongozi huyo wa Nigeria: “Tulishauriwa
sana tusije kuhudhuria kongamano hili kwa sababu ya hali ya usalama.
Lakini tusingefika tungewapa ushindi magaidi hawa ambao wanasumbua
sehemu kubwa ya Bara letu. Mheshimiwa Rais sala zetu ziko nawe na
wananchi wa Nigeria katika kipindi hiki kigumu.”
Serikali ya
Nigeria imekuwa inapambana na vikundi vya kigaidi na hasa kile cha Boko
Haram ambacho kimekuwa kinaendesha kila aina ya ugaidi hasa katika
maeneo ya kaskazini ya nchi hiyo.
Wiki tatu
zilizopita, kikundi hicho ambacho lengo lake kuu ni kupinga elimu ya
magharibi kiliteka watoto zaidi ya 200 wa kike kutoka mabweni ya shule
moja ya sekondari kaskazini mwa nchi hiyo.
Mpaka sasa
watoto hao hawajapatikana, jambo ambalo linaipa shinikizo kubwa Serikali
ya Nigeria. Boko Haram kimetishia kuwauza sokoni watoto hao wa kike.
Siku mbili
zilizopta, kikundi hicho kiliteka nyara watu wengine wanane na usiku wa
jana, kimeua watu wanaokadiriwa kufikia 300 katika vijiji mbali mbali
vya eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
8 Mei, 2014
إرسال تعليق