Na Othman Ame OMPR
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika
kwa Wanafunzi Nchini kuendelea kujifunza Taaluma mbali mbali kupitia
mfumo wa kisasa wa Teknoloji ya Habari na mawasiliano { Teknohama } ili
kwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi Ulimwenguni.
Balozi
Seif alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi msaada wa Kompyuta 230
kwa ajili ya Skuli mbali mbali Unguja na Pemba iliyofanyika Makao Makuu
ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali Mazizini Nje kidogo ya Maji wa
Zanzibar.
Msaada
huo wa Kompyuta 230 zilizofikishwa hapa Zanzibar ni miongoni mwa
Kompyuta 2,500 zilizoahidiwa kutolewa msaada na Rotary Klabu ya
Kimataifa inayojishughulisha na Kituo cha uungaji na matengenezo ya
Kompyuta katika Mji wa Seattle Nchini Marekani.
Rotary
Klabu hiyo ilifikia uamuzi huo wa kutoa msaada kufuatia ziara yake
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyoifanya Seattle
Marekani mwishoni mwa mwaka 2013 kuhudhuria Mkutano wa 15 wa Chama cha
Wafanyabiashara wenye asili ya Bara la Afrika wa Kaskazini Mashariki ya
Pacific.
Balozi
Seif alisema suala la ajira hivi sasa limekuwa likizingatia zaidi
muajiriwa katika Taasisi yoyote ile mbali ya ujuzi wake wa kitaalamu
lakini pia unahusishwa na ufahamu wa suala la mtandao wa mawasiliano ya
kompyuta.
Alieleza
kwamba jamii inapozungumzia suala la sayansi na Teknolojia kwa sasa sio
Physics na Chemistry lakini hata fani ya mitandao wa mawasiliano na
Kompyuta imepewa nafasi kubwa zaidi ambayo pia inatoa fursa ya
kurahisisha masomo hayo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwataka walimu na wanafunzi
watakaobahatika kupatiwa Kompyuta na vifaa hivyo katika awamu ya kwanza
kuhakikisha kwamba wanavitunza katika mazingira yatakayoviwezesha
kudumu kwa muda mrefu zaidi.
Alisema
hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itaendelea kuwapa moyo watu, Mashirika na
hata Taasisi zinazoamuwa kujitolea kusaidia vifaa na miradi mbali mbali
katika sekta ya elimu.
Balozi
Seif aliushauri Uongozi wa skuli mbali mbali nchini kufikiria kujenga
vyumba maalum vitakavyokuwa na sifa ya kuwekwa kwa vifaa vya Kompyuta
pale wakati utakaporuhusu kufanywa hivyo.
Mapema
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Abdulla Mzee
Abdulla alisema awamu ya mwanzo ya msaada huo wa Kompyuta, Vifaa vyake
pamoja na baadhi ya vitabu itaelekezwa kwa skuli 15 za Msingi ,Sekondari
na baadhi ya vituo vya elimu Unguja na Pemba.
Nd.
Mzee alizitaja skuli na vituo hivyo kuwa ni pamoja na Mtende, Chuo cha
Sayansi ya Afya,Chuo cha Hoteli na Utalii, Kampuni ya Zitec
itakayojishughulisha na matengenezo ya vifaa hivyo pamoja na Skuli ya
Makunduchi.
Nyengine
ni Kituo cha PSI, Skuli ya Alraudha, Utaani, Vitongoji, Kengeja,
Vikokotoni, Kitope Lumumba, Mchanga Mdogo pamoja na skuli ya Sekondari
ya Tumekuja.
Naye
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna
ameishukuru Klabu ya Rotari ya Seattle Nchini Marekani pamoja na Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa juhudi wanazochukuwa katika
kuimarisha sekta ya elimu hapa Zanzibar.
Balozi
Seif katika ziara yake ya mwezi Novemba mwaka jana Mjini Seattle Nchini
Marekani alipata fursa ya kukitembelea kituo cha uungaji na matengenezo
ya Kompyuta { Inter Connection } cha Rotary Clabu katika mji huo .
Mkurugenzi
wa Kituo hicho Bwana Charles Brennik kupitia Klabu hiyo alitoa tamko na
ahadi ya kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kompyuta 2,500 kwa
ajili ya maskuli mbali mbali hapa Zanzibar.
Wakati
huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alitembelea Mradi wa Ujenzi wa Skuli ya msingi, Vyoo pamoja na Tangi la
Maji katika Kijiji cha Kiwengwa unaofadhiliwa na Mradi wa Kimataifa wa
Give kutoka Nchini Marekani.
Wanafunzi
46 wa vyuo na skuli mbali mbali za Sekondari kutoka Nchini Marekani
wamepiga kambi kwa zaidi ya wiki moja sasa katika Kijiji cha Kiwengwa
wakiendelea na kazi mbali mbali za kujitolea katika ujenzi wa Skuli
hiyo.
Kiongozi
wa Wanafunzi hao Bwana Criss Backam alimueleza Balozi Seif kwamba
wanafunzi hao ni mkupuo wa kwanza katika kuendeleza mradi huo katika
awamu ya kwanza ya ujenzi huo iliyoanza mwezi Mei, Juni na kumalizia
mwezi wa Septemba.
Bwana
Criss alisema awamu ya pili ya wanafunzi hao itaingia mwezi Disemba na
kuendelea na ujenzi huo hadi Mwezi Febuari mwakani ambapo alisema
taaluma ya matumizi ya chupa za maji iliyobuniwa Nchini Nicaragua
Amerika ya Kusini katika ujenzi huo inatumika ili kutunza mazingira ya
kijiji hicho.
Akitoa
shukrani zake Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la
Kitope aliwapongeza wanafunzi hao kutoka Marekani kwa uamuzi wao
waliochukuwa wa kusaidia maendeleo ya Elimu katika Visiwa vya Zanzibar.
Balozi
Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi hizo
zenye nia ya kuwakomboa wananchi hasa watoto wa vijijini ambao kwa muda
mrefu walikuwa wakikosa fursa muhimu za kielimu kutokana na mazingira
yao ya kimaisha.
Wanafunzi
hao wa Skuli mbali mbali za Sekondari Nchini Marekani wanatarajiwa
kuondoka Zanzibar kwa kupitia Dar es salaam na Arusha ili kuona sehemu
za kihistoria pamoja na mbuga za Taifa kabla ya kurejea nchini kwao
siku ya Ijumaa
Post a Comment