
HEKAHEKA za uchaguzi wa klabu ya Simba zinaendelea
kwa kasi na ifikapo juni 29 mwaka huu rais mpya, makamu wa rais na wajumbe wa
kamati ya utendaji watapatikana tayari kwa safari nyingine ya miaka minne.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, wakili Dkt.
Damas Daniel Ndumbaro jana aliweka hadharani majina 41 ya wagombea wa nafasi
mbalimbali baada ya zoezi la uhakiki wa fomu kukamilika mwishoni mwa wiki
iliyopita.
Hakuna jina lolote lililoenguliwa kwa sasa, lakini
Ndumbaro alisema hayo ni majina ya awali na walichokuwa wanaangalia ni kama
wagombea wamejaza fomu vizuri na kuweka
viambatanisho vyote.
Kwa wagombea wote walioomba kugombea nafasi zote
zilizotangazwa walijaza vizuri fomu zao kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya
uchaguzi.
Wakati Ndumbaro anataja majina hapo jana, nilishangaa
kusikia maelezo yake kuwa kuna wanachama wa Simba wanamtaka awaache wagombea
wote mpaka siku ya uchaguzi na wao ndio wataamua nani anafaa.
Yaani wanachama hao wachache wanataka sheria na
kanuni za uchaguzi zisitumike, wagombea wapite moja kwa moja mpaka juni 29 ili
wakachambue mbivu na mbichi.
Hii ni ajabu sana! Watu 41 wabebwe bila kuwekewa
pingamizi, bila usaili, bila rufaa na mengineyo, hakika itavunja rekodi.
| Ismail Aden Rage anaondoka zake Simba sc |
Ndumbaro alijibu hoja hii kwa umakini mkubwa na
kuweka bayana kuwa haiwezekani hata kidogo mambo yakaenda kienyeji namna hiyo.
Alisema kamati yake haimuengui mgombea, bali
kanuni za uchaguzi na katiba ya Simba ndio zinamuengua mgombea.
Ndumbaro alisisitiza kuwa kamati yake ina watu
makini na yeyote ambaye hatakidhi kanuni na katiba ya Simba hatapitishwa
kugombe nafasi. Alionya kuwa watu wasitegemee mtelemko hata kidogo.
Akaongeza kuwa kama wanachama wanataka watu
wapitishwe tu basi hakukuwa na haja ya kuunda kamati ya uchaguzi, watu wangechukua
fomu tu na kwenda ukumbini kufanya uchaguzi.
Ndumabro alimaanisha kuwa kila jambo lina miiko
yake, sheria na kanuni stahiki. Huwezi kuendesha mambo ya msingi bila kanuni,
hata katika maisha ya familia, kuna kanuni zinazoiongoza.
Uchaguzi wa Simba ni suala nyeti mno. Hii ni
taasisi kubwa yenye watu wengi kila kona ya nchi hii. Lazima kiongozi bora
apatikane kwa misingi ya kanuni na sheria.
Kwa muda mrefu wanasimba wamekuwa wakilia na mwenendo
mbovu wa klabu yao. Kila kukicha walikuwa wanaulaumu uongozi wa mwenyekiti
anayeng`atuka madarakani, Ismail Aden Rage.
Walifanya majaribio kadhaa ya kumpindua mpiganaji
huyo, lakini Rage alisimamia katiba ya Simba na kuendelea kudunda katika kiti
chake cha mwenyekiti mpaka wakati huu mchakato wa uchaguzi umeanza.
Sijawahi kusema Rage alikuwa mbaya wala mzuri.
Kuna mapungufu yake na mazuri yake. Si jambo jepesi kwa wanasimba wengi kuona
kama Rage anafaa kwasababu mabaya yake yameziba mazuri yake.
Lakini kwasasa hakuna haja ya kupiga kelele juu ya
Rage, muda muafaka wa kuchagua watu wengine umefika.
Wakati wa kuchagua viongozi watakaowapeleka mbele
umefika,lakini wanaibuka `wahuni` wachache eti! mwanasheria Ndumbaro awaache
wagombe wapite bila kuchujwa. Kuna hoja hapa kweli?
Mtu mwenye mapenzi ya dhati na Simba hawezi
kufurahia `Ujinga` huu. Mwacheni Ndumbaro afanye kazi yake kama alivyoteuliwa.
Namfahamu Ndumbaro kikazi na nje ya kazi. Ni mtu
anayesimamia haki wakati wote. Ni mtetezi wa haki siku zote. Si mtu mwepesi kupindisha
uongo ukawa ukweli. Uongo utabaki kuwa uongo na ukweli utabaki kuwa ukweli.
Kama kuna mtu anawaza kuwa maneno yake ni
masihara, basi subirini moune kama mtu asiyekidhi vigezo atapita.
Hata mimi namuunga mkono Ndumbaro kwa kuzingatia
kanuni. Wana Simba tulieni na muiache kamati ya uchaguzi iwafikishe juni 29 na
watu sahihi.
Ndumbaro na wenzake wanajua vizuri kanuni za
uchaguzi na kama wataliengua jina lolote watasema sababu.
Ndumbaro ni mwanasheria, hawezi kuja mbele ya
waandishi wa habari na kutangaza kuengua jina la mtu bila kubainisha sababu. Ikitokea mtu
kaenguliwa, sababu zitawekwa wazi ili kila mtu aelewe.
Hakuna haja ya kuanza kuingiza `uhuni` katika
mambo ya msingi. Kanuni zifuatwe na watu wenye vigezo wapite.
Dkt. Ndumbaro simamia haki. Endelea na msimamo
wako wa kufuata sheria na kanuni za uchaguzi. Achana na mawazo mepesi ya watu
wasiokuwa na mapenzi na Simba.
Kamwe usithubutu kuwaangusha Simba, naheshimu sana
uwezo wako wa kusimamia sheria na kauni, nikutakia kila la heri .
Simba kuweni watulivu na hakikisheni hamfanyi
makosa hata kidogo.
- (F.S)
Post a Comment