Simba wala msijali, leteni milioni 320 - Mbeya City


TIMU ya Mbeya City imewaambia Simba kuwa watoe dola 200,000 (zaidi ya shilingi milioni 320) ili imuachie mshambuliaji wake tegemeo, Saad Kipanga, kwa ajili ya kukipiga Msimbazi.
Mshambuliaji huyo alijiunga na timu hiyo kwenye usajili wa msimu uliopita kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Rhino Rangers ya Tabora.
Kipanga hivi karibuni aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa, yupo tayari kutua kuichezea Simba kwa dau la shilingi milioni 30 na mshahara wa milioni moja kwa mwezi.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mwenyekiti wa Mbeya City, Mussa Mapunda, alisema kuwa hawatamzuia mshambuliaji huyo kwenda kuichezea Simba, kikubwa kanuni na sheria zifuatwe.
Mapunda alisema kuwa, dau hilo walilolitangaza limetokana na muda alioubakiza wa mwaka mmoja na nusu kati ya miwili aliyosaini katika mkataba wake.
Alisema kila mchezaji katika timu yao ana dau lake la usajili na uwezo wa mchezaji ndiyo wanaouangalia kama timu nyingine ikimhitaji kwenda kuichezea.
“Hatuwezi kumzuia mchezaji yeyote katika timu yetu kwenda kuichezea timu nyingine kutokana na kwamba soka ni ajira inayoendesha maisha yao.
“Na kama mchezaji yeyote akiondoka kwenye timu yetu kamwe hataacha pengo lolote kutokana na kuwepo wachezaji wengi wenye uwezo na vipaji vya kucheza soka,” alisema Mapunda.

Post a Comment

أحدث أقدم