Uzinduzi wa
chapisho la Tatu la Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na
kiuchumi linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 (Basic
Demographic and Socio-Economic Profile) katika ngazi ya Taifa uliokuwa
umepangwa kufanyika siku ya Ijumapili tarehe 25 Mei, 2014 umeahirishwa.
Uzinduzi huo sasa utafanyika
rasmi tarehe 10 Juni, 2014 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa
Mwl. Julius Nyerere uliopo mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar es Salaam
kuanzia saa 3:00 asubuhi.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Aidha, uzinduzi huo unatarajiwa
kuhudhuriwa na watu wapatao mia tano (500) ambao ni pamoja na Viongozi
mbalimbali wa ngazi za juu Serikalini, Mabalozi, Wadau wa Maendeleo,
Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wawakilishi wa Mashirika
yasiyo ya Serikali na Wadau wa Takwimu nchini.
Kwa kifupi chapisho hili linatoa
viashiria mbalimbali ambavyo ni pamoja na Kiwango cha uzazi, umri wa
kuishi wa mtanzania, vifo vya watoto wachanga, kiwango cha vifo vya
wakina mama vitokanavyo na uzazi na taarifa nyingine kwa ajili ya
kupanga mipango ya maendeleo.
Chapisho hili ni mwendelezo wa
machapisho mbalimbali yanayotolewa na Ofisi zetu mbili yaani Ofisi ya
Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar kama
ilivyoainishwa kwenye kalenda ya machapisho ya Sensa ya Watu na Makazi
ya mwaka 2012.
Imetolewa na Hajjat Amina Mrisho Said
Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, 2012
23 Mei, 2014
Post a Comment