Zanzibar. Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameapa
kuendelea kudai mfumo wa Muungano wa serikali tatu nje ya Bunge la
Katiba kwa nguvu zote, ikiwamo kufanya maandamano ya amani nchi nzima.
Mbowe, Profesa Lipumba, Mchungaji Mtikila wahutubia.PICHA\MAKTABA
Msimamo huo ulielezwa na viongozi hao kwa nyakati tofauti katika mkutano
wa hadhara uliofurika mashabiki kwenye Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja
jana.
Mwenyekiti Ukawa, Freeman Mbowe alisema wameamua kuliacha Bunge la
Katiba kutokana na harufu za rushwa, vitisho na matusi huku baadhi ya
wabunge wakiahidiwa vyeo.
Mbowe ambaye hata hivyo hakufafanua zaidi, alisema Ukawa wameamua kwenda kwa wananchi kuwaeleza dhamira chafu walionayo wabunge wa CCM katika mpango wao wa kukataa Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba.
Mbowe ambaye hata hivyo hakufafanua zaidi, alisema Ukawa wameamua kwenda kwa wananchi kuwaeleza dhamira chafu walionayo wabunge wa CCM katika mpango wao wa kukataa Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba.
“Ni jambo la hatari katika mchakato wa Katiba wananchi kuwa waoga au
hofu... Lazima tuwe tayari kuwaonyesha watawala kuwa tuna umoja imara,
tunayapigania mataifa huru ya Tanganyika na Zanzibar, Rais Kikwete
(Jakaya) asiwatishe wananchi kwa kivuli cha jeshi kuchukua madaraka,”
alisema Mbowe.
Lipumba anena
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema wajumbe wa
Ukawa wameamua kujitoa bungeni kutokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete
ambayo alidai kuwa iliibeza na kuidhalilisha Tume ya Warioba.
Alisema hawatarudi bungeni na kwamba hawawezi kujadili Katiba ambayo siyo maoni ya wananchi.
Alidai kwamba kwa makusudi Rais Kikwete aliamua kutetea sera za chama
chake na kupingana na maoni yaliyotolewa na wananchi kupitia Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
“Rais Kikwete ameharibu nia ya kupatikana Katiba Mpya, amekuwa
akijulishwa kila hatua na jinsi maoni ya wananchi walivyokuwa
wakipendekeza serikali tatu katika Rasimu ya Kwanza na ya Pili naye
akawa anaafiki, inashangaza amegeuka na kukataa maoni ya wengi,” alisema
Profesa Lipumba.
Mtikila akumbushia jela
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alisema aliwahi kufungwa
jela mara tatu, kuwekwa mahabusu mara 43 kwa kudai lipatikane Taifa la
Tanganyika huku watawala wakikataa matakwa ya wengi kwa sababu na hoja
dhaifu.
Mchungaji Mtikila aliongeza kusema kwamba wanachokitaka CCM na Serikali
zake ni kuendelea kuwabana wananchi wa Tanganyika na Zanzibar wasiweze
kuwa huru na kujivunia mataifa yao.
Seif: Mimi Ukawa damu
Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad
alieleza msimamo wake kuwa anaunga mkono harakati hizo na yeye ni Ukawa
damudamu.
“Walikuwa hawajui msimamo wangu, waelewe kwamba mimi ni Ukawa damu,” alisema.
Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema
wanaotetea mfumo wa serikali mbili ni sawa na watu wanaopigania
kuendelea kuwapo kwa dhuluma Tanzania.
“Hatuwezi kuendelea na mfumo huu, tumekuwa tukipiga kelele kwamba
Muungano huu wa serikali mbili umeteka mamlaka yetu,” alisema Maalim
Seif. Alimtaka Rais Kikwete asiwatishe wananchi kwa sababu wamependekeza
mfumo mpya wa serikali... “Unaposema kwamba jeshi litapindua nchi kama
tukiwa na Muungano wa serikali tatu, unamaanisha nini kama Amiri Jeshi
Mkuu?” alihoji Maalim.
Katika mkutano huo, ulinzi uliimarishwa vya kutosha huku magari ya FFU
na vikosi vya SMZ yakiwa yameegeshwa pembeni na askari waliokuwa
wamebeba silaha na mabomu viunoni wakilinda.
Chanzo: mwananchi.co.tz
Post a Comment