Kiongozi wa UKAWA Freeman Mbowe, akihutubia katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.
Mwenyekiti
wa NCCR Mageuzi James Mbatia, akihutubia katika mkutano wa hadhara
katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.
Mwenyekiti
wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba, akihutubia katika mkutano wa hadhara
katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.
Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia katika mkutano wa
hadhara katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.
Baadhi
ya viongozi wa UKAWA na wananchi wakisikiliza kwa makini hotuba Maalim
Seif, katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Gombani ya Kale,
Chake Chake Pemba.
Wafuasi
na wapenzi wa vyama vya upinzani wakifuatilia mkutano wa UKAWA
uliofanyika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba. (Picha na
Salmin Said, OMKR)
Na Hassan Hamad (OMKR)
Umoja
wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umesema utaendelea na kampeni yake ya
kutembea nchi nzima kuwafahamisha wananchi juu ya malengo ya umoja huo
pamoja na mustakbali wa katiba mpya ya Tanzania.
Akihutubia
mkutano wa hadhara ulioandaliwa kwa viongozi wa Ukawa katika viwanja
vya Gombani ya kale Chake Chake Pemba, kiongozi wa Umoja huo Freeman
Mbowe amesema umoja huo umekusudia kuwaungunisha watanzania, ili wapate
katiba mpya inayotokana na maoni na kuzingatia maslahi yao.
Amefahamisha
kuwa umoja huo una dhamira ya kwali, na kwamba kuanzia sasa hawatokuwa
tayari kugawanywa kwa misingi udini, ukabila au maeneo.
Mbowe
ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
amesema kwa kipindi kirefu vyama vya upinzani vimekuwa vikibaguliwa kwa
misingi hiyo, na kuahidi kuwa vitendo hivyo sasa vimefikia mwisho.
“Sisi
Chadema tumezushiwa propaganda kuwa ni chama cha Kikristo, na wenzetu wa
CUF wakaambiwa kuwa ni chama cha Kiislamu. Sasa tumegundua kuwa lengo
lao ni kutugawa na sasa hatugawiki tena”, alisisitiza Mbowe.
Kufuatia
kusonga mbele kwa UKAWA, Mbowe ambaye ni Kiongozi wa kambi rasmi ya
upinzani bungeni, amesema atavunja na kuunda upya baraza la mawaziri
kivuli bungeni ndani ya saa 24, ili kuwashirikisha viongozi wengine
wanaounda umoja huo.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba, amerejea kauli zake
kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma ndani ya serikali, na kwamba
ikiwa vitendo hivyo vitaachiwa kuendelea, nchi itashindwa kupiga hatua
za maendeleo kwa haraka.
Mwenyekiti
wa NCCR Mageuzi James Mbatia, amesema kitendo cha baadhi wa viongozi wa
serikali kwamba iwapo muundo wa serikali tatu utakubaliwa, Zanzibar
itakuwa dola ya kiislamu ni chokochoko ambazo hazina ukweli.
Amefahamisha
kuwa Waislamu na Wakristo wa Zanzibar wana uhusiano wa muda mrefu na wa
Kihistoria ambao hauwezi kutenganishwa, huku akielezea historia ya
kanisa la Minara Miwili la Zanzibar ambalo ni miongoni mwa makanisa
yenye historia ndefu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Nae
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amewashukuru viongozi wa
Ukawa kwa kuonesha umahiri ndani na nje ya bunge, na kuahidi
kushirikiana nao katika harakati za kupata katiba mpya inayotokana na
mawazo ya wananchi.
Viongozi
hao kwa pamoja wamewapongeza wananchi wa Pemba kwa kuonyesha mshikamano
katika kupigania haki na maendeleo ya kisiwa hicho, na kwamba ni mahali
pazuri pa kujifunza mshikamano.
إرسال تعليق