
Kauli
ya Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul (Chadema), aliyoitoa jana kwamba CCM
imechoka na haitoshi, ilisababisha kuibuka kwa malumbano kati ya makundi mawili
yaliyoundwa ndani ya Bunge Maalumu la Katiba la Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) na Tanzania Kwanza.
Gekul
ambaye ni mjumbe wa Ukawa, akichangia hotuba ya makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, alisema hayo akizungumzia matumizi mabaya ya fedha.
Alisema
kuwa Serikali ya CCM imechoka na haitoshi na wananchi wataishughulikia katika
sanduku la kura.
Akijibu
hoja hizo, Mbunge wa Sikonge, ambaye ni kiongozi wa kundi la Tanzania
Kwanza, Said Nkumba (CCM) alisema Chadema ndio imechoka kutokana na kila mwaka
kutafuta ushindi katika uchaguzi bila kuupata.
“Chama
kilichochoka ni kile kinachofanya juhudi kila mwaka kishinde lakini
kinashindwa…CCM ni njia kuu hatuwezi kuchepuka,” alisema Nkumba.
Nkumba
alishutumu hotuba iliyotolewa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe na kusema badala ya kujenga hoja za kisera,
alipeleka bungeni hoja ya Katiba ambayo ni hoja ya madaraka.
Akijibu
hoja ya Mbowe katika hotuba yake juu ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali,
Nkumba alihoji, “Mbowe ana usafi gani.”
Alikumbushia
tuhuma zilizowahi kuwasilishwa bungeni juu ya kiongozi huyo wa upinzani
kumwamuru mbunge mmoja wa kike atoke Marekani, alikokuwa katika safari
iliyogharimiwa na posho za Bunge, wakutane Dubai kwa ajili ya masuala
binafsi.
Vile
vile Nkumba alisema bungeni kwamba Mbowe alidanganya kwamba hatachukua gari la
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani na kusema alilikataa kwa sababu lilikuwa
kuu kuu na alipopewa gari jipya, alilichukua.
“Sasa
ile gari tena, katika hali ile ile ya matumizi mabaya kaenda nayo tena Mombasa
imekamatwa tena inashukiwa kwamba imebeba mabomu. Hayo hamyasemi hayo, mnazungumza
habari za Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake. Acheni michepuko, rudini kwenye
njia kuu,” alisema Nkumba.
Katika
hatua nyingine, kitendo cha baadhi ya wabunge kuendelea kukosa uvumilivu katika
mijadala inayoendelea bungeni na hivyo kuamua kuzomea, kimekemewa na Spika Anne
Makinda akihimiza kila mbunge au upande, kuheshimu mwingine hata kama ataumizwa
na hoja zinazotolewa.
Makinda
alikemea juzi baada ya kuwepo hali ya kuzomeana miongoni mwa wabunge
hususani upande wa upinzani dhidi ya CCM, pale
wabunge
wa chama hicho tawala walipokosoa na kujibu sehemu ya hotuba
iliyosomwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Akiahirisha
kikao cha juzi, Makinda alitaka wabunge kujenga utamaduni wa kuvumiliana hata
kama kutatolewa hoja ambazo wanapingana nazo, waache wahusika wazungumze.
Aidha
katika kuhakikisha kila mbunge anayechangia anakamilisha dakika zake saba bila
kuingiliwa, Spika amedhibiti utaratibu wa wabunge kukatisha wenzao kwa kile
ambacho kimezoeleka kuwa ni kutoa taarifa.
“Kuna
wengi walikuwa wakiomba kutoa taarifa wakati mzungumzaji mmoja mmoja
anazungumza. Sikuwapa nafasi mpaka saa ya kumaliza. Dakika saba ukimwingilia
mtu utavuruga na hautamsaidia. Na taarifa ni yako wewe. Dakika saba ni
chache ukimwingilia atapoteza hoja zake na hataeleweka,” alisema Spika juzi.
Miongoni
mwa maeneo ambayo Spika alilazimika kuingilia kati kwa kuwataka wabunge kujenga
tabia ya uvumilivu, ni pale Mbunge wa Magomeni, Muhammed Amour Chombo,
alipochangia akikosoa hotuba ya Mbowe ambayo pamoja na masuala mengine, ilisema
Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alitajwa kuwa siyo raia wa
Zanzibar.
Katika
hotuba hiyo ya Mbowe ambayo ilijikita kuzungumzia masuala ya Katiba mpya,
alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd katika mkutano wa
CCM, alisema Jussa siyo raia wa Zanzibar.
Alishutumu
kwamba kauli hiyo ni ya kibaguzi, kichochezi na yenye kupandikiza chuki dhidi
ya jamii ya watu wenye asili ya Kihindi.
Mbunge
Chombo katika kuchangia bajeti hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alikanusha kuwepo
ubaguzi dhidi ya Jussa. Alianza kuelezea namna anavyomfahamu Jussa na kueleza
Bunge kwamba alisaliti wazee wake.
Alisema
anamfahamu mwakilishi huyo vizuri kuliko Mbowe anavyomwelezea. Akaliambia Bunge
kuwa wakati mama yake anaolewa, mbunge huyo Chombo alimshuhudia.
Hata
hivyo wakati akiendelea kuchangia, akisema anamfahamu Jussa kuliko wanavyomjua,
zilianza kusikika sauti za kuzomea. Spika Makinda aliingilia kati na kuwaambia
kwamba kama upande mwingine usingekuwa na uvumilivu, kwa maana ya chama tawala,
hotuba ya Mbowe iliyosheheni shutuma kwa Serikali na chama tawala, isingesomwa
bungeni humo.
Mbunge
mwingine ambaye alizomewa na watu ambao hawakukubaliana na hoja
zake, ni wa Mbinga, John Komba ambaye alisema Chadema na CUF wamekwisha
ndiyo maana walisusa Bunge Maalumu la Katiba.
“Hii
hotuba ya Kambi ya Upinzani naichukua tu kama jamaa anapigana na mtu mwenye
nguvu kubwa. Amepigwa halafu anasema nishike nitamuua. Chadema na CUF
wamemalizwa. Rudini kule tukatwangane kule hapa si sehemu yake. Njooni mpate
makonde kule kwenye Bunge Maalumu,” alisema Komba.
Komba
aliendelea kuponda vyama hivyo vya upinzani vinavyounda Ukawa akisema, “Hawa
sasa hivi watashika mpira kwapani wataondoka...Vumilia yakuingie usishike
mpira,” alisema Komba.
Mbunge
wa Dole, Sylvester Mabumba (CCM) alitaka Mbowe aeleze Bunge mantiki ya kusema
Tanzania Bara ni mkoloni anayetawala Zanzibar kwa nguvu. “Lakini sifa ya
mkoloni huwa anateua gavana. Je gavana aliyeteuliwa Zanzibar ni nani?”
Alihoji.
Naye
Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi alisema ingawa anafahamu Bunge
la Bajeti na si la Katiba, yapo mambo ambayo
ameona
ni vyema kuyaeleza akisema Mbowe amepotosha Watanzania. “Nilitaka kusimama
wakati akitoa taarifa,” alisema Zambi.
Kwa
mujibu wa Zambi, katika hotuba ya Kiongozi huyo wa Upinzani, anatabiria mabaya
nchi kwa kusema ikifika uchaguzi bila Katiba, nchi haitaeleweka.
“Katiba
itakamilika saa ngapi wakati nyie mnakimbia mnaenda nje. Lazima mbaki ndani.
Sisi sio wa mwisho kuandika Katiba bali ni wananchi,” alisema.
Zambi
aliendelea kusema, “Tuache kuaminisha Watanzania kwamba tusipopata Katiba mpya
nchi itakwenda vibaya. Wakati mwingine
viongozi
wa Upinzani hawana nia njema na nchi hii. Nchi itakapoingia kwenye vurugu
viongozi hawa watakimbia nchi . Tuwe makini na kauli hizi za kupotosha.”
Kwa
upande wake, Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage alisema baada ya Chadema kufanya
vibaya katika uchaguzi mdogo wa ubunge Kalenga mkoani Iringa na Chalinze mkoani
Pwani, kimeamua kuunda Baraza la Mawaziri Kivuli kwa kushirikisha CUF jambo
linalodhihirisha wameshindwa kufanya kazi wenyewe.
Wakati
huo huo Chiligati aliasa Bunge la Bajeti lisigeuzwe kuwa Bunge Maalumu la
Katiba. Alisema hilo ni Bunge la wananchi ambalo wanataka kufahamu juu ya
utatuzi wa matatizo yao.
“Nimeshangaa
sana asubuhi hotuba ya kiongozi wa upinzani zaidi ya nusu ya muda amezungumza
mambo ambayo yalipaswa yazungumzwe kwenye Bunge la Katiba. Leo zaidi ya dakika
40 akazungumzia mambo ya Katiba badala ya matatizo ya wananchi,” alisema
Chiligati.
Akishutumu
kitendo cha Mbowe pamoja na wajumbe wengine wa Ukawa kutoka bungeni na badala
yake wakaja kutoa maoni kwenye Bunge la Bajeti, Chiligati alisema, “ Badala
yake, alichukua timu yake akaweka mpira kwapani akatoka nje…mwezi wa nane (Agosti)
timu yake airudishe ndani hayo yote yazungumzwe humu ndani.”
إرسال تعليق