
WAAJIRIWA
wapya wa fani ya ualimu wa shule za msingi katika Wilaya ya Handeni,
Mkoa wa Tanga wameanza kazi kwa kuonja machungu ya madeni baada ya
kutopewa stahili zao zote kabla ya kuanza kazi na kusambazwa kwenye
vituo vyao vya kazi kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Wakizungumza
na Thehabari.com kwa masharti ya kutotaja majina yao kwa kuhofia
kunyanyaswa na uongozi wa juu wilayani hapo, walisema kuwa kwa mujibu wa
makubaliano na taratibu walitakiwa kulipwa shilingi 245,000 ikiwa ni
malipo ya fedha za kujikimu kwa siku saba yaani shilingi 35,000 kwa kila
siku jambo ambalo halikufanywa.
Mmoja
wa walimu hao walioanza kazi tangu Aprili Mosi, 2014 alisema walipoanza
kazi walilipwa shilingi 140,000 tu na kuahidiwa kiasi kingine kumaliziwa
ndani ya mwezi huo, ahadi ambayo haijatekelezwa ilhali wao wakiangaika
na maisha ya ugenini fedha hawana na wamepigwa marufuku kufuatilia fedha
halmashauri hadi hapo itakapotangazwa.
Alisema
walitegemea kwa kuwa malipo ya kujikimu hawakupewa yote wangelipewa
mshahara wa mwezi Aprili jambo ambalo nalo halikutekelezwa kwani
wamejibiwa kuwa, eti hakuna fedha kwa sasa hadi hapo watakapojulishwa
kwenye vituo vyao vya kazi.
"...Wakati
tunaanza kazi (Aprili Mosi) tulipewa shilingi 140,000 badala ya
Shilingi 245,000/- tuliahidiwa tungelipwa malipo yaliobaki ndani ya
mwezi wa nne lakini hadi leo hatujalipwa na tumezuiwa kwenda kufuatilia
wala kuulizia malipo, wametuma ujumbe toka halmashauri kwa walimu wakuu
kuwa tusiende kufuatilia mshahara wa mwezi wa nne hadi hapo
itakapotangazwa, jaribu kufikiria tunaishi vipi ugenini?," alisema mmoja
wa walimu hao.
Aidha
mmoja wa walimu hao alisema hali ya maisha walipopelekwa ni ngumu ilhali
wakitakiwa kununua vitu vya msingi vya kuanzia maisha kama vile godoro,
kitanda, vyombo vidogo vya ndani na vinginevyo jambo ambalo wengine
walifanya na kuishiwa kabisa na fedha kidunju waliopewa.
"Ndugu
mwandishi hebu wewe fikiria unawezaje kuishi ugenini kwa shilingi
140,000/- hujanunua godoro, kitanda na maji ndoo moja huku tunanunua
shilingi 500, vyombo vya ndani huna unaishi vipi katika hali kama hii?,"
alisema mmoja wa walimu hao huku akionesha kusikitika.
Akizungumzia
taarifa hiyo leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya Handeni, Dk. Khalfany
Haule alipopigiwa simu alioneshwa kushangazwa na taarifa hiyo na kudai
atawasiliana na mwandishi wa habari baadaye, lakini alipotafutwa baadaye
simu yake ilikuwa imezimwa.
إرسال تعليق