Wanajeshi
nchini, wamemwahidi Rais Jakaya Kikwete kuendelea kusimama imara, kupokea na
kutii amri na maelekezo yake bila hila na kuhakikisha
hawayumbishwi
na kauli potovu za kisiasa.
Ahadi
hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein
Mwinyi kwa niaba ya wanajeshi wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya
Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Dk
Mwinyi ambaye wizara yake iliomba kuidhinishwiwa Sh trilioni 1.3, aliwasilisha
shukurani za wanajeshi kwa Rais Kikwete, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu kwa hiba
yake ya uongozi, ushupavu, uvumilivu na maridhiano vitakumbukwa na kuenziwa na
vizazi na vizazi hususani kwao.
“Ahadi yetu kwake ni kuwa tutaendelea kusimama
imara kupokea na kutii amri na maelekezo yake bila hila yoyote na kutoyumbishwa
na kauli potovu za kisiasa,” alisema Dk Mwinyi na kushangiliwa bungeni.
Aidha
katika hotuba hiyo ya Waziri, aliwasilisha salamu za pongezi za Rais Kikwete
kwa wanajeshi wote kwa kufanikisha maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa
Tanzania.
Katika
salamu hizo, Rais Kikwete alisema kazi iliyofanywa na wanajeshi ni kubwa na
waliifanikisha kwa weledi, utii, uhodari, ujasiri na kwa kishindo cha hali ya
juu.
“Ushiriki wao umedhihirisha umma wa Watanzania
na ulimwengu kwa ujumla kuwa jeshi letu ni imara, shupavu na lipo tayari
kulinda, kutetea na kudumisha Muungano wetu…nami nikiwa Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa natamka kuwa najivunia nao,” alisema Dk Mwinyi.
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, katika taarifa yake iliyosomwa na
Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa, pia imepongeza wizara na vyombo vyote vya
ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ya ulinzi na usalama wa nchi na hivyo
kudumisha amani, utulivu na umoja wa nchi.
Pia
ilipongeza majeshi yote kwa kufanikisha sherehe za Muungano ambazo kwa
mujibu wa kamati, zilifana na kuhakikishia Watanzania kuwa nchi iko
salama.
Awali,
akizungumzia bajeti ya wizara yake, Dk Mwinyi alitaja changamoto za utekelezaji
wa mpango na bajeti ya mwaka 2013/14, alisema kulikuwa na changamoto kubwa
katika utekelezaji wake kutokana na kuidhinishiwa kiwango kidogo cha Bajeti
ikilinganishwa na mahitaji halisi.
Alitoa
mfano katika mwaka huo wa fedha, wakati mahitaji halisi kwa kuzingatia
vipaumbele vya wizara yalikuwa ni Sh trilioni 1.74, bajeti iliyoidhinishwa
ilikuwa Sh trilioni 1.1 sawa na asilimia 63.3 ya mahitaji.
Kamati
ilizungumzia pia ufinyu wa bajeti na kushauri
Serikali
kutoa kwa wakati fedha zote zinazoidhinishwa na Bunge kila mwaka.
Wakichangia
kwa nyakati tofauti, wabunge wengi walitetea wanajeshi na kutaka Serikali
iendelee kuwajali wawapo kazini na wanapostaafu.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM) alisema ni lazima jeshi liwezeshwe
hususani vikosi vinavyotengeneza zana, Serikali ihakikishe inanunua vifaa hivyo
badala ya kununua nje ya nchi.
“Wakati wa amani ndiyo wakati wa kutoa jasho
jingi, ukitoa jasho wakati huu, ikija kutokezea damu itakuwa kidogo sana…Umoja
wa Mataifa unapenda majeshi yetu,” alisema.
Kwa
upande wake Mbunge wa Chambani, Yussuf Salim Hussein (CUF)m alitaka
stahiki za wanajeshi ziangaliwe upya na kusema haipendezi kukuta mwanajeshi
mstaafu akiwa katika hali mbaya.
Mbunge
wa Manyoni, John Chiligati (CCM) alisema amani na utulivu vinavyoonekana,
vinatokana na kuwepo Watanzania ambao usiku na mchana wanailinda nchi.
Alisema
kulinda amani ni aghali hivyo Serikali lazima iwekeze kwenye vyombo vya ulinzi
na usalama. Alitaka vyombo hivyo visichukuliwe kama vyombo vya kawaida.
Chiligati
ambaye ni mwanajeshi mstaafu, alisema wastaafu mambo yao hayajakaa vizuri.
Alisema kamati ilitembelea Bunge la India ambalo miongoni mwa mambo waliyotaka
kujifunza ilikuwa ni namna wanavyohuduma
wanajeshi
wastaafu. Chiligati alishauri askari hao waendelee kuundiwa mfumo wa
kijeshi wawapo uraiani baada ya kustaafu.
Mbunge
wa Wawi, Hamad Rashid (CUF) ameshauri viongozi kuwa makini katika
matamshi yao kuepuka kuchochea uvunjifu wa amani.
Alisema
jeshi linafanya kazi nzuri na kusisitiza kuwa watu wanaodhani vita ni
kitu cha kawaida, wafuatilie nchi zilizokumbwa na machafuko.
إرسال تعليق