Waziri wa Fedha: Bajeti ya mwaka 2014/2015 ni Sh19.6 trilioni

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiteta jambo na  Waziri wa Fedha, Saada Mkuya kwenye mkutano wa wabunge ambapo waziri wa fedha aliwasilisha mapendekezo na mwelekeo wa bajeti ya serikali  kwa mwaka fedha 2014/15, Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao Dar es Salaam. 

Serikali imetoa mwelekeo wa Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/15 kuwa ni Sh19.6 trilioni, ikilinganishwa na Sh18.2 za Bajeti iliyopita.
Vipaumbele vya Bajeti hiyo ni kuendeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioanza mwaka 2011 na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao unajumuisha maeneo sita ya kitaifa ya kilimo, elimu, maji, utafutaji wa rasilimali fedha, nishati, uchukuzi na uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara.
Katika kuhakikisha inakusanya fedha za kutosha, Serikali imeahidi kuunda kikosi kazi cha kufuatilia mapato yote yanayotoka halmashauri zote nchini ili kuondoa visingizio vilivyojitokeza wakati wa ufuatiliaji wa mapato.
Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya wakati akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti hiyo kwa kamati zote za Bunge, Dar es Salaam.
Alisema matumizi ya kawaida kwa mwaka ujao wa fedha yanalenga kufanikisha mambo 20 muhimu, yakiwamo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014, Uchaguzi Mkuu 2015, kukamilisha mchakato wa Katiba na nyongeza ya mishahara na kulipa kwa wakati.
Mkuya alisema makadirio ya matumizi ya maendeleo ni Sh7.7 trilioni sawa na asilimia 39 ya matumizi yote ya Serikali.
Kati ya fedha hizo, miradi ya maendeleo imetengewa Sh5.4 trilioni sawa na asilimia 27 na matumizi mengine ya maendeleo ni Sh2.2 trilioni.
Utegemezi
Mkuya alisema katika mwaka unaomalizika, Serikali ilipanga kukopa Dola 700 milioni za Marekani sawa na Sh1.1 trilioni na kati ya kiwango hicho, iliambulia mkopo wa Dola 259 milioni hivyo kuweka nakisi ya Dola441.
Alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali imekusudia kukopa Sh4.2 trilioni kutoka vyanzo vya mapato vya ndani na nje ili kuziba pengo la mapato.
Misaada na pato la taifa
Katika mwaka wa 2013/2014, Serikali ilipokea misaada ya Sh1.1 trilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo ikiwa ni asilimia 50 ya ahadi ya Sh2.3 trilioni, hivyo kuweka nakisi ya Bajeti ya Sh1.2 trilioni.

Post a Comment

أحدث أقدم