CRDB YAHADHARISHA WATEJA KUWA MAKINI NA MITANDAO

Benki ya CRDB imewaonya wateja wake kuwa makini na baadhi ya mitandao inayoibuka na kulaghai kwa kuwataka wananchi, kutoa taarifa zao muhimu za kibenki, jambo ambalo linahatarisha usalama wa fedha zao zinazohifadhiwa na benki hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki CRDB, Dk Charles Kimei, alisema hayo Dar es salaam mwishoni  mwa wiki,  katika mkutano uliohusu  uboreshwaji wa huduma za benki kupitia simu za mikononi 'simbanking' na njia za wateja kujilinda na uhalifu kwa njia ya mtandao.
Kuhusu matapeli wa mitandao, alisema kumeibuka mchezo kwa baadhi ya mitandao ya kijamii, ikijaribu kuwalaghai wateja kwa kuwaomba taarifa za akaunti zao ili kufanya uhalifu.
"Huduma ya simbanking ni salama na imepitia viwango vyote vya kiusalama jambo muhimu ni kuwasisitiza wateja kutunza vizuri taarifa za akaunti zao ikiwemo kadi zao na namba za siri ili kujiepusha na matapeli hao," alisema Dk Kimei.
Alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini na kundi hilo, wasikubali kudanganyika kwa kutoa taarifa zinazohusiana na nyaraka za benki zao na kusisitiza kuwa ni marufuku kutoa taarifa hizo hata kwa wafanyakazi wa benki.
Dk Kimei alisema pamoja na kwamba benki hiyo inawapigia simu wateja wao wakiwataka kukamilisha usaili wao kuhusiana na kuingia katika  mfumo wa simbanking, watambue kuwa hawatoulizwa kutoa taarifa zozote za akaunti zao.
Kuhusu mbinu wanazotumia matapeli, Mkurugenzi wa Idara Hatarishi, James Mabula, alisema, huwapigia simu wakijifanya kuwa wakurugenzi ama wafanyakazi wa benki hiyo na kisha kuwaghilibu kwa kutaka kupatiwa namba za siri za akaunti husika.

Post a Comment

Previous Post Next Post