BABA WA MAREHEMU ASUSA KUMZIKA MWANAWE

Baada ya vuta nikuvute  iliyosababisha uhasama mkubwa  baina ya familia mbili mjini hapa  wakigombea  kuuzika mwili  wa mtoto  mwenye umri  wa mwaka mmoja na nusu,  hatimaye  familia ya  baba mzazi wa marehemu  imekubali 'yaishe' na kuruhusu  familia  ya mama  mzazi  kumzika mtoto huyo.
Shangazi ya marehemu, Evelyne Komba amebainisha kuwa  maamuzi  hayo yalifikiwa juzi baada ya  kuusindikiza  mwili wa marehumu  ili uhifadhiwe  katika  chumba  cha maiti  katika Hospitali ya  Wilaya  ya Mpanda,  chini ya ulinzi mkali  wa Jeshi  la Polisi  kupitia  Kikosi  cha Kutuliza  Ghasia (FFU).
Aliongeza kuwa vurugu zilizotokea  makaburini  kwa  ndugu  wa baba mzazi wa marehemu  kucharazwa  fimbo  na  kudungwa 'mangumi' baada ya familia ya mama wa marehemu  kufukia  kaburi lililochimbwa na  familia ya  baba mzazi wa  marehemu  ndio  kulikochochea  uhasama  mkubwa  baina yao.
Shangazi huyo wa marehemu alisema ndipo walipolazimika kuita Polisi ambao waliweka ulinzi mkali  nyumbani  kwa  bibi  ya marehemu  mtaa wa Kawajense   Madukani, ukifanyiwa tarartibu  za  maziko na kuamuru mwili huo kurejeshwa  katika  chumba cha maiti  hospitalini.
"Mwili huo hatimae   ulichukuliwa  na  'defender' (gari la polisi)  la Polisi  nyumbani kwetu  nasi  upande  wa  familia ya baba wa marehemu  tulipanda  gari hilo na kuusindikiza   mwili  huo  mpaka  uliohifadhiwa  mochwari. Ndipo hapo hapo  tulipokutana na kufikia maamuzi hayo,"  alisema Evelyne.
Hata hivyo alikiri kuwa  wao  familia  ya  baba  wa  marehemu wote  walizira kuhudhuria maziko  ya mtoto  huyo  wakihofia  usalama wa maisha yao.
"Hatukuweza kuhudhuria  maziko  ya mtoto Junior  kwa  sababu  bado kuna uhasama mkubwa baina ya familia  hizi  mbili  sasa kule  kuna  vifaa  vya kuchimbia  kaburi  vikiwemo  sepetu, majembe  vingeweza  kutumika  na wenzetu kutudhuru.Tuliona  tuepushe  dhahama hiyo  kwa kutokwenda kuhudhuria  maziko  ya  mtoto  huyo,"  alisema  kwa  hisia kali .
Akizungumza na mwandishi  wa  habari hizi,  baba  wa marehemu Joseph Bacho (26),  alikiri kuwa amejisikia huzuni kubwa kwa kukosa  kuhudhuria maziko ya mwanae Junior akidai anafikiria kuwachulia hatua zaidi  za kisheria hata hivyo hakuzifafanua.
"Najisikia huzuni kubwa  nilihofia usalama  wa maisha yangu, hivyo sikuweza kuhudhuria maziko  ya mwanangu  Junior. Ujue  uhasama  wa  wakwe zangu uliibuka  baada ya Junior kufariki  dunia,  wakidai eti  hawanitambui kama  baba  yake mzazi  marehemu  kwa  sababu zijatoa  posa. Sasa kwa nini wadai baada ya mtoto kufikwa na umauti badala ya kunidai  akiwa bado yu hai?" anahoji  Joseph .
Baadhi ya wanandugu  waliohojiwa na  mwandishi,  kwa masharti  ya
kutoandikiwa  wamekiri  kuwa   familia ya  mama mzazi  wa marehemu iliuchukua mwili  huo  saa  nane mchana,  katika  chumba cha kuhifadhia maiti  hospitalini hapo  na  kuustiri  saa  12 jioni jana.
Familia hizo mbili  zote  zikiishi  mtaa mmoja wa Kawajense Madukani, mjini hapa, zilijikuta zikiingia katika uhasama mkubwa hivi kiasi cha kupigana fimbo na ngumi makaburini katika ugomvi wa kugombea kuzika mwili wa mtoto Junior  Bacho.
Sababu kubwa ya mpasuko huo imeelezwa kuwa ni mahari, kwani wazazi upande wa mama wa mtoto huyo walikuja juu na kumzuia baba wa mtoto, Joseph Bacho asishiriki katika shughuli zozote za maziko ya mtoto wake wakidai hawamtambui kwa kuwa hajatoa mahari kwa binti yao.
Inaelezwa kuwa, Joseph na mzazi mwenzake, Anna Kizo (20) walimzaa mtoto Junior Bacho nje ya ndoa, ambapo hadi umauti unamfika mtoto huyo, baba yake mzazi alikuwa hajajitambulisha kwa upande wa mwanamke wala kutoa mahari.
Na kwamba, tangu kuzaliwa kwa mtoto huyo, alikuwa akiishi na kulelewa na mama yake mzazi, Anna nyumbani kwa wazazi wake.
Kwa mujibu wa mashuhuda vurugu hizo ziliibuka baada ya upande wa ndugu wa baba wa mtoto kuweka msiba nyumbani kwao na kuandaa taratibu za kumzika mtoto huyo.
Hata hivyo, kitendo hicho kilipingwa na upande wa mama wa mtoto, ukisema ndio wenye haki ya kumzika mtoto huyo ambaye hawakuwahi kumtambua kisheria baba yake mzazi.
Ndugu wa upande wa baba ulifanikiwa kuchimba kaburi, kuutoa mwili mochari na kuufikisha nyumbani tayari kwa maziko, lakini vurugu za upande wa pili ikiwa pamoja na ndugu upande wa mama kufukia kaburi, zilisimamisha shughuli zote, huku malumbano yakishika hatamu hadi askari wa jeshi la polisi kupitia Kikosi chake cha Kuzuia Fujo (FFU) kilipolazimika kuingilia kati na kusimamia shughuli na kuurudisha mwili katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda.
Inaelezwa kitendo cha upande wa mama wa mtoto kufukia kaburi ndiko kulikochangia kuchochea vurugu hadi FFU walipoingia kati.
Ilivyoanza Mkasa mzima unadaiwa kutokea mtaani hapo Alhamisi wiki iliyopita, siku ambayo mtoto huyo alifariki dunia katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda alikokuwa akiuguzwa na shangazi yake, Evelyne Komba na bibi yake mzaa baba, Teddy Francis.
Inaelezwa kuwa, wakiamini wana haki zote za kumzika mtoto huyo, waliuchukua mwili na kuweka msibani nyumbani kwao, jambo lililopingwa na upande wa mama wa mtoto waliokuja juu na kusema hawamtambui baba wa mtoto kwa kuwa hakuwa ametoa mahari.
Inadaiwa Joseph aliamua kumchukua mwanae huyo Juni 18 , mwaka huu kwa nguvu kutoka kwa mama yake mzazi na kumpeleka hospitalini alikolazwa kwa matibabu baada ya kubainika kuwa anasumbuliwa na utapia mlo mkali .
Kwa mujibu wa mashuhuda ndipo upande wa ndugu wa mama mzazi wa marehemu walipozira ikidaiwa kuwa hawakuweza kufika hata siku moja kumjulia hali mtoto huyo aliyekuwa akiuguzwa hospitalini hapo na shangazi yake Evelyne na bibi yake Teddy hadi umauti ulipomfika .
Licha ya upande wa ndugu wa mama mzazi wa marehemu kushushiwa tuhuma na lawama hizo nzito waliendelea na msimamo wao kwamba walikuwa na haki ya kumzika marehemu hivyo nao wakaamua kuweka msiba nyumbani kwa mama wa marehemu katika.
Ndipo , Juni 27 wazee wa Mtaa wa Kawajense waamua kuingilia kati mgogoro huo kwa kuzikutanisha pande hizo mbili zilizokuwa zikivutana na kufikia uamuzi kuwa msiba uwe nyumbani kwa baba wa marehemu.
Kufutia uamuzi huo shangazi wa marehemu aliongoza ndugu zake akiwemo baba mzazi wa marehemu hadi chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda mjini hapa na kuuchukua mwili wa marehemu kisha kuupeleka nyumbani kwa bibi ya marehemu kwa ajili ya maandalizi ya maziko yake.
Maziko ya mtoto huyo yalipangwa kufanyika katika makaburi ya Kawajense ÐMsufini, ambako upande wa ndugu wa baba mzazi wa marehemu walichimba kaburi katika eneo hilo, lakini muda mfupi baada ya kukamilisha kuchimba kaburi hilo ndugu wanaodaiwa wa upande wa mama mzazi wa marehemu waliwawavamia wachimba kaburi na kuwalazimisha kulifukia .
Waombolezaji waliokuwa msibani nyumbani kwa bibi ya marehemu baada ya kutaarifiwa tukio hilo,lililotokea makaburini walitimua mbio na kuelekea makaburini na kukuta baadhi ya wanandugu upande wa mama wakimalizia kufukia kaburi hilo.
Walipoulizwa sababu za kufukia kaburi hilo, walianza kufoka ndipo inadaiwa kundi la ndugu wa mama wa marehemu waliibuka na kuanza kuwashambulia kwa kuwacharaza fimbo ndugu wa baba mzazi wa marehemu .

Post a Comment

Previous Post Next Post