MADEREVA WA MABASI KANDA YA ZIWA WAGOMA

Abiria waliokuwa wanasafiri kwa mabasi kutoka Kanda ya Ziwa kuelekea mikoa ya Pwani na Kaskazini, juzi walijikuta wakilazimika kuchelewa kufika mjini Singida kwa zaidi ya saa tatu kutokana na mgomo wa madereva wao.
Madereva hao, walimlalamikia Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani Singida, Mohammed Likwata kwamba eneo lote la barabara kuu ya Singida limejaa alama zinazoonesha mwendo kasi wa kilomita 50 tu kwa saa na hakuna vibao vinavyofuta ukomo huo wa mwendo; hivyo kusababisha kukamatwa kwao kila wanapoendesha mwendo wa zaidi ya km 50.
Walimweleza Kamanda Likwata walipowasili mkoani Singida madai yao mengine kuwa ni pamoja kukithiri kwa rushwa na faini zisizofuata haki.
Walidai kuwa askari usalama barabarani mkoani Singida huwadai malipo ya Sh 200,000/- kwa kosa la mwendo kasi lakini risiti inayotolewa huwa ya Sh 30,000/- tu.
Lakini pia walalamikia tozo ya Sh 10,000 kila basi linapotoka getini katika vituo mbalimbali wanavyopitia katika safari zao na kusema kuwa hawajui fedha hizo ni kwa ajili ya shughuli gani kwa kuwa
hawapewi stakabadhi.
Abiria hao walendelea kumweleza wandishi wa habari hizi kwamba kutokana na uonevu wa askari wa usalama barabarani mkoani Singida wanaowakamata madereva kwa madai ya kwenda mwendo kasi, walipofika eneo la Malendi,  mpakani mwa Singida na Tabora, walipunguza sana mwendo wao.
Kutokana na madereva hao kuendesha  kwa mwendo wa taratibu kwa kile walichodai kuogopa kumulikwa na 'tochi' ya askari wa usalama barabarani, mabasi hayo zaidi ya 50 yaliingia mjini Singida saa tisa mchana badala ya muda wake wa kawaida wa saa sita mchana.
Katika kikao chao na Kamanda Likwata aliwasihi madereva hao kuendelea nasafari na kwamba malalamiko yao yatashughulikiwa wiki hii, pendekezo amblo lilikubaliwa na madereva na kisha kuendela na safari.

Post a Comment

Previous Post Next Post