Ugonjwa wa
kuanguka na kupiga kelele unaowakumba baadhi ya 
wasichana katika shule mbalimbali nchini, umetajwa kusababishwa  na 
maambukizi ya hofu inayosababisha mwili kupata dalili za magonjwa
yasiyokuwepo. 
Mtaalamu wa
saikolojia na theolojia, Mchungaji  John
Rowse  kutoka taasisi ya The Uhakika
Christian Education Trust Fund kutoka Mbeya, alisema hayo hivi karibuni baada
ya kutembelea  shule zinazopata tatizo
hilo mara kwa mara na kuzungumza na wazazi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Alisema kuna mambo kadhaa yanayochangia kujenga hofu
hiyo ambayo mwili hujitayarisha kuambukizwa, ikiwemo vitisho vya maisha kwa
wanafunzi vinavyotokana na mambo mbalimbali kama vile ugomvi na mabadiliko
ambapo miili yao inahangaika kujihami. 
Kwa mujibu wa Mchungaji huyo, upo uwezekano kuwa
baadhi ya  wanaoanguka, ni wasichana
wanaonyanyaswa nyumbani, wengine wanafundishwa kujidharau na wengine
wanabaguliwa na kufanyiwa unyanyapaa shuleni.
Sababu nyingine ya kuanguka kwa wasichana shuleni
kwa mujibu wa Mchungaji  Rowse, ni hofu
wanayopewa wasichana hao na waganga wa kienyeji 
wanaotabiri au kupiga ramli, pamoja na wachungaji au wainjilisti wanaokemea
mapepo huku wakiwashika  kichwani, begani
au kwenye shingo na kuwatetemesha wasichana hao.
Mchungaji 
Rowse  alisisitiza kuwa  dawa pekee ya 
kutibu ugonjwa huo,  ni utulivu
kwani wanafunzi hao hususani 
wasichana  huambukizana kwa hofu
hivyo matibabu yake  ni kupunguza hofu na
mawazo.
“Hofu 
hiyo  kwa wasichana  hao  husababishwa  kwa imani potofu, waganga wa kienyeji  wanaotabiri au kupiga ramli ... waganga  hawa 
wanapenda kujenga hofu ya uchawi, ili baadaye wajidai kwamba ni wao
waliondoa laana na kuleta uponyaji.
“Dawa ya kusaidia kuzuia matukio hayo ni kuwa na
mipango ya kupunguza msongo wa mawazo shuleni, hasa miongoni  mwa 
wasichana,” alisema.
Mchungaji 
Rowse alipendekeza machifu na waganga 
wa jadi  wasikaribishwe shuleni
kuwaombea wasichana hao kwa kuwa watawaongezea hofu.
Pia alipendekeza wachungaji au wainjilisti
wanaopenda kushika mtu kichwani, begani au kwenye shingo na kumtetemesha,
wasikaribishwe shuleni kwa kuwa nao pia ni hatari.
“Hata wale wanaokemea mapepo kwa sauti kubwa na
wakati wakifanya hivyo hupenda kumwangalia msichana kwa ukali jicho kwa jicho.
”Katika mazingira hayo,  watoto 
watapata  tena  hofu na wakianguka  tena watasema ni pepo, lakini sivyo. Afadhali
mchungaji wa amani, amwombee kila mwanafunzi aliyekumbwa na ugonjwa huo kwa
sauti ndogo tu na kwa upole na upendo na kumfariji na utulivu. Asitamke wazi
neno lo lote juu ya mapepo,” alisisitiza.  
Alishauri kuwa kila shule iwe na mwalimu au mshauri
wa kike ambaye hatoi adhabu kwa wasichana, atakayepaswa kujenga urafiki nao na
kuwa karibu nao, ili wamwamini na kumwelezea mateso yao ya maisha, nyumbani na
shuleni. 
Alisisitiza kuwa 
wanafunzi  wa kike  wapewe nafasi za kukutana katika  vikundi, 
ili  wajadiliane pamoja kuhusu
mambo yoyote, pia  walimu  wajitahidi kumpa kila msichana nafasi ya kusikilizwa.
Alitoa mfano wa Shule ya Msingi Inyonga wilayani
Mlele katika Mkoa wa Katavi, ambayo aliitembelea na kuzungumza wazazi,
wanafunzi  na walimu wa shule hiyo. 
Alisema baada ya shule hiyo kuanza kutekeleza
ushauri huo,   Mwalimu Mkuu wa shule
hiyo, Casto Ismail, alimwambia kuwa kasi ya matukio imepungua. 
“Mwalimu Mkuu huyo alinieleza kuwa wamekuwa na
mitihani ya darasa ya saba, ambao kwa kawaida husababisha msongo wa  mawazo kwa wanafunzi, lakini hakuna
mwanafunzi wa darasa ya saba hata mmoja aliyeanguka wakati huo…katika madarasa
mengine ni wachache walioanguka.  
“Niliwaambia walimu wawe na uvumulivu. Mambo
yatatulia kweli baada ya mabadiliko ya imani ya wazazi na jamii… lakini
watalaamu bado wanashindwa kuelewa kwa nini hali hiyo inakutwa sana kwa
wasichana na wanawake,” alisema Mchungaji 
Rowse.   
Mwandishi alifika katika Shule ya Msingi Inyonga na
kuzungumza na Mwalimu Ismail, ambaye alieleza kuwa  ugonjwa 
huo  ulidumu kwa  zaidi ya miezi  sita tangu ulipowakumba wasichana wanaosoma
katika shule  hiyo Novemba mwaka jana. 
Alifafanua kwamba kasi ya kuanguka  kwa wasichana hao  shuleni 
hapo  imepungua baada ya kuanza
kufanyia kazi ushauri wa Mchungaji Rowse, aliyefika  shuleni hapo na kuzungumza na wanafunzi.  Pia alitoa 
semina  kwa wanafunzi, walimu  na wazazi.

Post a Comment