
Dar es Salaam/Mwanza. Rais Jakaya Kikwete ameshauriwa kunusuru mchakato
wa kupata Katiba Mpya ili usisimame kwa kuvua koti la Uenyekiti wa CCM
na kubaki na Urais ili awaeleze wananchi nini cha kufanya kupata Katiba
Mpya.
Ushauri huo umetolewa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na
wasomi walioshiriki katika mdahalo wa Katiba uliofanyika jijini Dar es
Salaam na Mwanza jana. Walisema kuwa Rais ana wajibu kuunusuru mchakato
huo kwa kuwa yeye ndiye aliyeuvuruga kwa hotuba yake ya ufunguzi wa
Bunge Maalumu la Katiba iliyoonekana kuelemea upande wa chama chake CCM.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod
Slaa amesema Rais Jakaya Kikwete amekuwa kigeugeu juu ya Muundo wa
Serikali za Muungano kama zilizopendekezwa kwenye Rasimu ya Kwanza na ya
Pili ya Katiba.
Alisema kuwa Rais Kikwete alionyesha wazi kukubaliana na Muundo wa
Serikali tatu, kwani kabla Rasimu ya Pili ya Katiba haijapelekwa kwenye
Bunge Malaumu la Katiba ili kujadiliwa, alisaini kuonyesha kuwa
amekubaliana na yaliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Akihutubia kwenye Kongamano la Wazi na Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine
cha Mwanza (Saut) Dk Slaa alisema:
“Rais Jakaya Kikwete amekuwa kigeugeu, kwani yeye ndiye aliyesaini
Rasimu ya Pli ya Katiba ili ikajadiliwe kwenye Bunge Maalumu la Katiba.”
Aliongeza: “Kwa kuwa ndiye mtu wa mwisho kuruhusu rasimu hiyo ijadiliwe
kwenye Bunge Malaamu la Katiba ni wazi alikubaliana na
kilichopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyopendekeza Muundo
wa Serikali Tatu, hivyo inashangaza kuona leo anageuka na kutaka
Serikali mbili.”
Dk Slaa ambaye pia ni kiongozi katika Umoja wa Katiba ya Wananchi Nje ya
Bunge (Ukawa), alisema kuwa katika mikoa 17 waliyozunguka na kufanya
mikutano na wananchi, wamebaini kuwa Rasimu ya Katiba ya Pili wananchi
hawaifahamu na kwamba hiyo ni njia ya CCM kuchakachua maoni yao yaliyomo
kwenye rasimu hiyo, wakati wa kupiga kura za maoni.
Alisema wanatambua ujanja unaofanywa na CCM kutaka kupitisha mambo
wanayoyataka wao, lakini wao watendelea kuwaelimisha wananchi ili
watambue kwamba maoni yao ndiyo nguzo ya kuwapa Katiba bora na siyo
vinginevyo.
“Tumefanya mikutoano mikoa 17, lakini kote tulipopita wananchi
wametuambia hawaifahamu Rasimu ya Pili ya Katiba kutokana na janja ya
CCM kuficha rasimu ya hiyo ili wananchi wasiifahamu. Kutokana na hilo
ni wazi kwamba wanataka kuchakachua maoni ya wananchi kwenye kura za
maoni,”alisema Dk Slaa.
Akinukuu maneno kutoka katika hotuba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere aliyoitoa mwaka 1995 Dk Slaa alisema: “Watu wapumbavu ni wale
wanaoamini kwamba Katiba haibadiliki.”
Alisema lazima Katiba ibadilike na kwamba wananchi ndiyo wenye Katiba,
hivyo siyo busara kutaka kuchakachua maoni yao na kuweka maoni ya chama
au mtu binafsi.
“Watu wanamini kuwa Katiba haiwezi kubadilika, mimi naona ni upumbavu,
kwani hata Mwalimu Nyerera aliwahi kusema hivyo kwenye hotuba yake ya
mwaka 1995,” alisema Dk Slaa.
Tundu Lissu
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu alisema kuwa kuna
mambo mema ambayo Mwalimu Julius Nyerere alifanya na mengine ambayo siyo
mema, hivyo Watanzania na wasomi wanapaswa kuyachuja na kuyakataa
mabaya na kuchukua mema.
Alisema katika mambo mabaya ambayo Mwalimu Nyerere aliacha ni pamoja na
kuwarithisha Watanzania hofu, jambo alilosema hadi sasa limewatawala.
“Nyie kama wasomi wa Saut naomba niwaambie kwamba katika mambo mabaya
ambayo Mwalimu Nyerere aliwarithisha Watanzania ni hofu, jambo ambalo
hadi leo linaawatawala kwani Watanzania wengi wanaogopa kusema kwa
kuhofu kufukuzwa kazi au vyuo, “alisema Lissu na kuongeza:
“Mmoja ya mfumo mbaya ambao Mwalimu Nyerere aliuanzisha baada ya kupata
uhuru mwaka 1962 ni kuwaweka watu kizuizini. Hii ilikuwa inatokea kwamba
unakamatwa na watu usiowajua na unawekwa kizuizini, ”alisema.
Kutoka Dar es Salaam, Muungano wa Asasi za Kiraia (AZAKI), umemtaka Rais
Jakaya Kikwete kunusuru mchakato wa kupata Katiba Mpya usisimame
ukieleza kuwa yeye ndiye aliyeuvuruga.
Akizungumza katika mkutano wa AZAKI, jijini humo aliyekuwa Mjumbe wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, alisema kuwa
mchakato mzima ulikwenda vizuri, lakini baada ya Kikwete kulihutubia
Bunge Maalumu la Katiba, mwelekeo wa Bunge hilo ulibadilika.
Alisema kuwa Rais Kikwete alikwenda kulihutubia Bunge kama kiongozi wa
CCM, badala ya kiongozi wa nchi, ambapo aliweka msimamo wa chama chake
wa kutaka Muundo wa Serikali mbili.
“Rais apate ujasiri akiwa kama kiongozi wa nchi na siyo kama kiongozi wa
CCM, awahutubie wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kuwataka wajadili
Katiba ya wananchi na siyo ya chama wala yake binafsi,” alisema Baregu.
Aliongeza kuwa kama Rais hatalinusuru Bunge hilo na kila mtu akafanya
anavyotaka au kwa masilahi ya chama chake kama ambavyo ameonyesha mfano,
demokrasia nchini haitawezekana.
Baregu aliwataka wajumbe watumie miezi miwili iliyobaki kujipanga upya
iwapo wana nia ya dhati ya kuendelea na mchakato huo, ili ipatikane
Katiba bora ya wananchi akionya kwamba, tofauti na hapo Watanzania
hawatakubali.
Kauli ya Baregu pia iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Sheria
Zanzibar, Awadhi Ally Saidi ambaye ni pia ni miongoni mwa waliokuwa
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, aliyesema kuwa inafaa Rais
awahutubie wajumbe na kuwakumbusha kuwa jukumu lao ni kujadili Rasimu ya
Katiba ya kuipitisha na siyo kuondoa vipengele.
“Ndiyo maana walipewa siku 70 kujadili Rasimu ya Katiba, lakini
walitumia siku 21 kutunga kanuni ambazo zilitungwa na Baraza la
Wawakilishi likishirikiana na Bunge la Muungano,” alisema
Post a Comment