IMEFAHAMIKA kuwa, Simba imepanga kuibomoa Mbeya City katika usajili wa msimu ujao kwa kuwasajili wachezaji watano kwenye kikosi cha timu hiyo kinachofundishwa na Juma Mwambusi.
Timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara hivi sasa zipo kwenye usajili kwa
ajili ya kuviimarisha vikosi vyao kuelekea msimu ujao uliopangwa kuanza
Agosti, mwaka huu.
Baadhi ya wachezaji wanaotajwa kuwaniwa na klabu hiyo ni mshambuliaji
Saad Kipanga na kiungo mkabaji Anthony Matogolo ‘Mmasai’ aliyewasumbua
viungo wa Simba, Yanga na Azam FC ndani ya msimu uliopita.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Simba,
wachezaji hao wanaotaka kuwasajili ni mapendekezo katika sehemu ya
ripoti ya Kocha Mkuu, Mcroatia, Zdravko Logarusic.
Chanzo hicho kilisema, wakati wakiwawania wachezaji hao, uongozi wa
Simba umekata tamaa ya kuwapata nyota hao kutokana na urefu wa mikataba
yao.
“Hivi sasa tumelisimamisha zoezi la usajili hadi pale tutakapowapata viongozi wapya katika uchaguzi wetu watakaoiongoza Simba.
“Wakati tukisubiria uchaguzi huo kupita, baadhi ya viongozi wa Kamati
ya Utendaji ya Simba wanaendelea kupitia mapendekezo ya ripoti ya kocha
ambayo inatupa ugumu katika usajili kwa kuwa inahitaji wachezaji watano
katika kikosi cha Mbeya City na wote wana mikataba mirefu,” kilisema
chanzo hicho.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Mbeya City, Mussa Mapunda, alisema: “Sasa
hao Simba wakiwachukua wachezaji hao watano si wataiua timu yenyewe
yote, lakini acha tuangalie, wao waje tufanye mazungumzo.”
إرسال تعليق