
Akizungumza
na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Jacqueline Maleko alisema
mpaka jana tayari kampuni 1,260 za kitanzania zilithibitisha kushiriki
na kuwataka washiriki wamalize ujenzi wa mabanda yao mpaka kufikia Juni
26.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa washiriki
kutoka mataifa ya Marekani na Jamhuri ya Czech kushiriki maonesho hayo,
hivyo kuwataka wajasiriamali wa kitanzania kutumia fursa hiyo kujifunza
na kupata uzoefu kutoka kwao kwani lengo la maonesho hayo ni kutengeneza
ajira na si kuuza bidhaa.
“Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni za
kimarekani na Jamhuri ya Watu wa Czech kuja kushiriki maonesho haya.
Hivyo tunataka maonesho yakiisha tuone fursa kwa wajasiriamali wetu
kujitengenezea ajira kutokana na ujuzi na uzoefu watakaoupata kutoka kwa
wenzao,” alisema.
Akizungumzia maonesho hayo, Mkurugenzi huyo
alisema maonesho ya mwaka huu yatakuwa na msisimko zaidi kutokana na
kuongezeka kwa idadi ya washiriki toka mataifa mbalimbali ya nje jambo
lililowalazimu kuongeza eneo katika viwanja hivyo.
Kwa upande wake
Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara za Nje wa Mamlaka hiyo, Anna
Mulondo alisema utaratibu wa uingiaji katika viwanja hivyo pamoja na
nauli haujabadilika na kubaki kama mwaka jana kwa lengo la kuongeza
hamasa kwa wananchi na watu kutoka nchi nyingine kwenda kwa wingi
kutazama maonesho hayo.
Alisema kwa upande wa nauli, mtu mzima
atalipa Sh 2,500 huku mtoto akilipa Sh 500 kwa siku zote za maonesho
isipokuwa siku ya kilele cha maadhimisho hayo ambayo ni Julai 7
kiingilio kwa mtu mzima kitakuwa ni Sh 3,000 wakati mtoto atalipia Sh
1,000.
“Utaratibu wetu ni ule ule wa mwaka jana haujabadilika. Magari
hayataruhusiwa kuingia ndani, kuna maeneo maalumu ya maegesho nje ya
viwanja na hivyo tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kutazama
maonesho hayo,” alisema.
Maonesho hayo ya Biashara ya Kimataifa ya 38
yanatarajiwa kuanza juni 28 na kumalizika Julai 8 mwaka huu katika
Viwanja vya Maonesho vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar
es Salaam.
Post a Comment