
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania DkT. Mohammed Gharib Bilal leo Jumatatu Juni 02,
2014 ameshiriki katika sherehe za kukabidhi madaraka kwa Rais mpya wa
Malawi Profesa Arthur Peter Mutharika katika sherehe zilizofanyika
kwenye uwanja wa Kamuzu Banda jijini Blantyre. Sherehe hizo pia
zilihudhuriwa na Rais wa Botswana sambamba na wawakilishi wa nchi za
Zimbabwe, Msumbiji, Afrika Kusini na nyinginezo.
Akihutubia baada ya kukabidhiwa
sime ambayo ni ishara ya kuwa kiongozi wa watu wa Malawi, Rais Mteule
Mutharika alisisitiza kuwa, katika kipindi cha utawala wake atahakikisha
kuwa anaifanyia makubwa Malawi sambamba na uhakikisha kuwa anaifanya
Malawi itimize majukumu yake ya kimataifa kufuatia kutambua kuwa
kujitenga kunaweza kuifanya Malawi kutonufaika na fursa zilizopo
duniani.
“Nchi hii ipo katika dunia na
siyo rahisi tena kuwa na fikra kwamba Malawi inaweza kubaki peke yake
kama kisiwa. Tunahitaji kuwa na wenzetu wa kusaidia maendeleo ya Malawi.
Tunawahitaji wahisani toka Kusini ama Mashariki, tunayahitaji mataifa
tajiri na mataifa yanayoendelea. Tutafanikiwa sana kama tutaendeleza
urafiki kwa wote. Tufanye hivi bila kujali kuwa sisi ni taifa kwani hali
ya sasa inahitaji kila mmoja wetu kushirikiana na mwenzake,” alisema.
Katika hotuba hiyo pia
amesisitiza kuwa kipindi chake cha utawala atajitahidi kukabiliana na
rushwa na kwamba hatakuwa na mchezo kwa wala rushwa katika kipindi akiwa
madarakani. Pia alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuiunganisha Malawi kwa
miundombinu bora ili kuboresha maisha ya wananchi sambamba na kusogeza
huduma za wananchi karibu.
Rais Mutharika aliapishwa juzi
baada ya kuwashinda washindani wake akiwemo Rais aliyemaliza kipindi
chake Joyce Banda ambaye hata hivyo hakuweza kutokea katika sherehe hizi
za kukabidhi madaraka. Akizungumzia suala la kutohudhuria kwa Rais
Banda, Rais Mteule Mutharika alisema alitegemea Rais Banda kuwepo lakini
hakufika nay eye anatambua kuwa wakati wa uchaguzi kulikuwa na tofauti
baina yao lakini kwa sasa uchaguzi umeisha na amesahau yaliyopita ili
kuanza ukurasa mpya wa kuijenga Malawi. Katika shughuli hiyo pia Rais wa
zamani wa Malawi Kamuzu Banda alihudhuria.
Makamu wa Rais Dkt. Bilal na
msafara wake walitarajiwa kurejea nyumbani leo hii Jumatatu mara tu
baada ya kukamilika kwa kazi hii ya makabidhiano.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Juni 02, 2014 Blantyre, Malawi
Post a Comment