MKATABA WA GESI TANZANIA 10% WAGENI 90% KAMATI YA BUNGE YATAKA UANGALIWE UPYA

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luhaga Mpina
BUNGE limeishauri serikali kupitia upya mikataba ya gesi na kampuni za nje ili kubaini kama kweli maslahi ya taifa yamezingatiwa.
Ushauri huo ulitolewa jana bungeni na Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara wakati Mwenyekiti wake, Luhaga Mpina, akisoma utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha na Uchumi pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Mpina alisema kuwa kamati yake inatoa ushauri huo baada ya kubaini kuwapo kwa kasoro kwenye mkataba kati ya serikali na Kampuni ya Statoil ya nchini Norway.


Alisema kuwa Aprili 18, serikali na Statoil ziliingia mkataba na kugawana uzalisaji (PAS) kwa ajili ya kutafuta na kuendeleza mafuta katika kitalu namba mbili.
“Hapo baadaye ilipoonekana kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa gesi asilia katika kitalu hicho, serikali iliamua kuingia mkataba wa nyongeza ili kujumuisha utafutaji na uendelezaji wa gesi asilia katika mkataba wa kwanza.
“Kampuni ya Exxonmobile Explomotion and Production Tanzania Ltd, nayo iliingia katika mkataba wa nyongeza kama mbia wa asilimia 35 wa kampuni hiyo ya Statoil,” alisema.
Mpina ambaye pia ni mbunge wa Kisesa (CCM), alisema kamati yake ilibaini kuwa ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa gesi katika mikataba hiyo ya nyongeza, haupo.
Alisema kuwa kwa hali hiyo ina maana kuwa sera ya ushirikishwaji wa Watanzania haitakuwa na nguvu yoyote kisheria kwa sababu tayari mkataba umeshaingiwa ambao unasisitiza kuwa kampuni za nje zitakuwa na uamuzi wa mwisho.
“Swali ni kwamba, je, sera yetu katika ushirikishwaji kwa wazawa ambayo ipo katika mchakato wa kutayarishwa na Wizara ya Nishati na Madini itakuwa na nguvu za kisheria juu ya vipengele vya mikataba ambayo imeshaingiwa huko nyuma?” aliohoji.
Alisema katika mkataba huo wa nyongeza, kampuni hizo za nje zimeruhusiwa kuchukua asilimia 70 ya gesi ili kujilipa gharama zilizotumika kimkataba na Watanzania kubaki na asilimia 30 hadi hapo watakapomaliza kujilipa gharama walizotumia.
“Katika gesi yote inayochimbwa, makampuni ya kigeni yanaanza kwa kuchukua asilimia 70 na kubakisha asilimia 30. Katika hiyo iliyobaki, TPDC na makampuni ya kigeni wanakaa na kugawana uwiano ambapo TPDC itaanza kwa kugawiwa asilimia 30, makampuni ya kigeni asilimia 70,” alisema.
Kwa mujibu wa Mpina, kihalisia TPDC itakuwa inapata mgawo wa asilimia 30 ambao ni sawa na asilimia 10 ya gesi yote inayozalishwa wakati makampuni ya kigeni yanapata asilimia 70, sawa na asilimia 90 ya gesi yote.

Post a Comment

Previous Post Next Post