
BUNGE limeishauri
serikali kupitia upya mikataba ya gesi na kampuni za nje ili kubaini
kama kweli maslahi ya taifa yamezingatiwa.
Ushauri huo
ulitolewa jana bungeni na Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara
wakati Mwenyekiti wake, Luhaga Mpina, akisoma utekelezaji wa majukumu
ya Wizara ya Fedha na Uchumi pamoja na makadirio ya mapato na matumizi
kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Mpina alisema kuwa
kamati yake inatoa ushauri huo baada ya kubaini kuwapo kwa kasoro kwenye
mkataba kati ya serikali na Kampuni ya Statoil ya nchini Norway.
Alisema kuwa Aprili
18, serikali na Statoil ziliingia mkataba na kugawana uzalisaji (PAS)
kwa ajili ya kutafuta na kuendeleza mafuta katika kitalu namba mbili.
“Hapo baadaye
ilipoonekana kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa gesi asilia
katika kitalu hicho, serikali iliamua kuingia mkataba wa nyongeza ili
kujumuisha utafutaji na uendelezaji wa gesi asilia katika mkataba wa
kwanza.
“Kampuni ya
Exxonmobile Explomotion and Production Tanzania Ltd, nayo iliingia
katika mkataba wa nyongeza kama mbia wa asilimia 35 wa kampuni hiyo ya
Statoil,” alisema.
Mpina ambaye pia ni
mbunge wa Kisesa (CCM), alisema kamati yake ilibaini kuwa ushiriki wa
Watanzania katika uchumi wa gesi katika mikataba hiyo ya nyongeza,
haupo.
Alisema kuwa kwa
hali hiyo ina maana kuwa sera ya ushirikishwaji wa Watanzania haitakuwa
na nguvu yoyote kisheria kwa sababu tayari mkataba umeshaingiwa ambao
unasisitiza kuwa kampuni za nje zitakuwa na uamuzi wa mwisho.
“Swali ni kwamba,
je, sera yetu katika ushirikishwaji kwa wazawa ambayo ipo katika
mchakato wa kutayarishwa na Wizara ya Nishati na Madini itakuwa na nguvu
za kisheria juu ya vipengele vya mikataba ambayo imeshaingiwa huko
nyuma?” aliohoji.
Alisema katika
mkataba huo wa nyongeza, kampuni hizo za nje zimeruhusiwa kuchukua
asilimia 70 ya gesi ili kujilipa gharama zilizotumika kimkataba na
Watanzania kubaki na asilimia 30 hadi hapo watakapomaliza kujilipa
gharama walizotumia.
“Katika gesi yote
inayochimbwa, makampuni ya kigeni yanaanza kwa kuchukua asilimia 70 na
kubakisha asilimia 30. Katika hiyo iliyobaki, TPDC na makampuni ya
kigeni wanakaa na kugawana uwiano ambapo TPDC itaanza kwa kugawiwa
asilimia 30, makampuni ya kigeni asilimia 70,” alisema.
Kwa mujibu wa
Mpina, kihalisia TPDC itakuwa inapata mgawo wa asilimia 30 ambao ni sawa
na asilimia 10 ya gesi yote inayozalishwa wakati makampuni ya kigeni
yanapata asilimia 70, sawa na asilimia 90 ya gesi yote.
إرسال تعليق