
Dar es Salaam. Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
amewashauri wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na CCM kuacha
kuzunguka mikoani kufanya mikutano inayoeleza misimamo yao kuhusu
mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa haina tija kwa taifa.
Ameonya kuwa
mikutano hiyo inajenga mwelekeo mbaya kwa taifa na kuhatarisha mchakato
wa Katiba na kuzitaka pande hizo kumaliza tofauti zao.
Akizungumza katika
mahojiano maalumu yaliyofanyika Dar es Salaam jana, Warioba alisema:
“Kwa mustakabali mwema wa taifa, ni muhimu makundi haya ‘ya-resolve’
(yamalize), matatizo yaliyopo kabla ya Agosti, ili Bunge Maalumu la
Katiba likirejea, wote washiriki na kukamilisha mchakato wa kupata
Katiba Mpya. Hili ni kwa masilahi ya taifa.”
Kauli ya Waziri
Mkuu huyo mstaafu ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu, imekuja huku
makundi ya Ukawa linaloundwa na wabunge wengi wa upinzani na viongozi
wa CCM wakiendelea kung’ang’ania misimamo yao kuhusu Rasimu ya Katiba
Mpya iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Wakati CCM ikipinga mapendekezo ya kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu uliomo kwenye Rasimu, Ukawa unaunga mkono mapendekezo hayo.
Aprili 16,
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliiongoza Ukawa kutoka ndani
ya Bunge la Katiba baada ya kumaliza kuchangia mjadala huo, kwa madai
ya kutokutendewa haki na CCM katika mambo mbalimbali ikiwamo kupinga
mapendekezo ya upinzani hata yale ya msingi akisema hawawezi kuwa sehemu
ya watu wanaosambaza chuki na kuwa sehemu ya kuibomoa nchi.
Siku chache
baadaye, Ukawa ulianza mikutano nchi nzima kwa kile ulichodai kuwaeleza
wananchi namna CCM inavyotaka kuchakachua maoni yao yaliyokusanywa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa upande wake, CCM imekuwa ikifanya mikutano kueleza msimamo na sababu za kutaka kuendelea kwa muundo wa serikali mbili.
Jaji Warioba
alisema makundi hayo yana nafasi ya kumaliza tofauti zao kabla ya Bunge
Maalumu la Katiba kuanza tena vikao vyake, hivyo kuliwezesha taifa
kupata Katiba Mpya.
Alisema makundi hayo yasipopatana yanaweza kuhatarisha mustakabali wa taifa hata amani iliyopo.
Alionya kuwa amani iliyopo nchini ikivurugika kwa sababu yoyote ni vigumu kuirejesha na kwamba watakaotaabika ni wananchi.
Jaji Warioba ambaye
aliwahi kuongoza Tume ya Rushwa iliyoundwa na Rais wa Awamu ya Tatu,
Benjamin Mkapa, alisema amani ya Tanzania ikivurugika kutokana na
makundi kupingana katika mchakato wa Katiba wanasiasa ndio
watakaonyooshewa vidole.
Awali, Februari
mwaka huu baada ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba
katika Bunge Maalumu la Katiba wanaCCM wengi, kuanzia Mwenyekiti wake,
Rais Jakaya Kikwete waliichambua huku wakionyesha dhahiri
kutokuridhishwa na mapendekezo kadhaa kubwa ikiwa ni muundo wa Muungano.
Katika Bunge hilo,
wajumbe wengi wa CCM walimshambulia Warioba na tume yake wakidai kuwa
Rasimu ya Pili ya Katiba haikuzingatia maoni ya wananchi na Mabaraza ya
Katiba.
Baadaye katika
uzinduzi wa ripoti ya Twaweza kuhusu Mchakato wa Katiba, Jaji Warioba
alijibu shutuma hizo alipouliza maswali saba ya msingi ambayo aliwataka
wawajibu wananchi ili kutuliza kiu yao.
Maswali hayo yalikuwa:
1. Kwa nini mnapinga muundo wa Muungano wakati walioupendekeza ni wananchi?
2. Wapeni majibu wananchi kwa nini Tanganyika imevaa koti la Muungano?
3. Elezeni kwa nini Katiba imevunjwa, madaraka ya Rais kuchukuliwa na marais wawili katika nchi moja?
4. Tume ilitumwa na nani kukusanya maoni ya wananchi na kwa kutumia sheria ipi zaidi ya ile ya Mabadiliko ya Katiba?
5. Kwa nini
wanawatuhumu uongo yeye na Joseph Butiku kuwa walikuwa wajumbe wa Tume
za Kisanga na Nyalali zilizopendekeza serikali tatu?
6. Kwa nini hawataki kuzungumzia yaliyomo katika rasimu bali wanadai imeandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba?
7. Waeleze kwa nini wanadai Tume imeingiza maoni yake, wakati iliyakusanya kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba?
Bunge Maalumu la
Katiba litarejea Agosti mwaka huu baada ya kusitisha vikao vyake kupisha
Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.
إرسال تعليق