![]() |
Azam raha; Shomary Kapombe kulia akiwa na mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco mazoezini hivi karibuni |
MWENYEKITI
wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amesema hawawezi kupokea chini ya
Euro 43,000 kutoka kwa Azam FC kutokana na uhamisho wa kiungo Shomary
Kapombe.
Akizungumza
na BIN ZUBEIRY leo, Rage amesema kwamba enzi za klabu hiyo kuuza
wachezaji kwa dola za Kimarekani 10,000 zimepitwa na wakati chini ya
viongozi ambao walikuwa si waelewa.
“Nasema,
chini ya uongozi wangu, mtu yeyote asitegemee biashara ya chee, Azam
wanamtaka Kapombe, walete Euro 43,000 vinginevyo hawatamtumia kwenye
mashindano yoyote, watafanya naye mazoezi tu,”amesema Rage.
Rage
amesema suala zima ka uhamisho wa Kapombe alilishughulikia Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe kwa ushirikiano
naye wa karibu.
Amesema
makubaliano yalikuwa kumpeleka Kapombe bure AS Cannes ya Ufaransa
akaendelezwe ili baadaye auzwe klabu za Ulaya kwa bei nzuri, Simba SC
inufaike.
“Na
tulikubali hivyo baada ya wao wenyewe kutuonyesha kwenye tovuti yao
namna wanavyouza wachezaji weusi kwa bei nzuri klabu za Ulaya. Hakuna
mchezaji ambaye waliwahi kumuuza chini ya Euro Milioni 1.8,”amesema
Rage.
Mbunge
huyo wa Tabora Mjini (CCM) amesema kwa kujua hilo hawakuona sababu ya
kuwa na tamaa ya kudai fedha mapema, wakaamua kuingia Mkataba na AS
Cannes.
“Tukakubaliana
wakifanikiwa kumuuza Kapombe popote, sisi watupe asilimia 40 ya bei
waliyomuuza na wao wachukue asilimia 40, wakati asilimia 20 ni ya wakala
wa Kapombe,”amesema Rage.
“Tulikuwa
na imani kama Kapombe angebaki Ulaya na kuendelezwa, tungenufaika kwa
sababu angeuzwa bei nzuri na Simba SC ingepata fedha nyingi,”.
Ilifikia
wakati Kapombe akagoma kurudi Ulaya akidai hajalipwa mshahara wa mwezi
mmoja, hadi ikabidi Hans Poppe ajitolee kumlipa huo mshahara huyu kijana
ili arudi Ulaya, lakini mwenyewe akagoma,”
“Kwa
kweli kitendo cha Kapombe kushindwa kurudi Ulaya kimetusikitisha sana,
siyo tu kimetuharibia sisi kama klabu, bali kimewaharibia wachezaji wa
Tanzania kwa ujumla,”.
“Wao
(wachezaji wa Tanzania) wasione Waafrika wenzao wengine wanacheza timu
kubwa Ulaya, kwa kweli wanaanzia mbali na wanakuwa wavumilivu na wenye
malengo, ndiyo maana wanafanikiwa,”
“Sasa kwa
Kapombe kugoma kurudi kule, maana yake kesho huwezi tena kumtafutia
nafasi mchezaji wa Tanzania akafanikiwa, wamekwishatudharau,” amesema
Rage.
Pamoja na
yote, Rage amesema baada ya Kapombe kuamua kurudi Tanzania na kujiunga
na Azam, Simba SC inataka taratibu zifuatwe ili wao wapate haki yao.
“Sisi
tunazo hadi barua za Azam wamepeleka ofa ya Euro 40,000 ikakataliwa na
Cannes. wakapeleka Euro 70,000 pia ikakataliwa. Sasa ambacho sisi
tunaona hapa, ni kwamba Azam wamemnunua huyu mchezaji kwa Euro
107,000,”.
“Cannes
wamepokea Euro 43, 000 ambayo ni asilimia 40 ya Euro 107,000. Maana yake
na sisi Azam wanatakiwa kutupa kiwango hicho hicho. Lakini Azam
wamemuandikia barua Katibu wangu wanasema wao wameambiwa na Cannes
watulipe asilimia 40 ya Euro 43,000 kitu ambacho si sahihi na
hatukubali,”amesema Rage.

Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage
Kapombe
alikwenda Ufaransa katikati ya mwaka jana kujiunga na klabu hiyo ya
Daraja la Nne, lakini Novemba mwaka huo aliporejea kuichezea Tanzania
katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Zimbabwe hakutaka tena
kurudi Ulaya.
Machi
mwaka huu, akaanza kufanya mazoezi na Azam FC kabla ya mwezi uliopita
kusaini Mkataba wa miaka mitatu na mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu
nchini.
Post a Comment