![]() |
Ingawa mapambano dhidi ya matukio mbalimbali ya manyanyaso ya
kijinsia kwa watoto (wakike na kiume) yamekuwa yakifanyika katika
jitihada za kupunguza ama kumaliza, lakini uchunguzi nilioufanya
umebaini kwamba bado kuna haja ya kuongeza kasi ya mapambano hayo!
Binafsi nimekuwa nikipokea taarifa za matukio mbalimbali toka kwa
wananchi na kuyarusha kupitia kipindi cha Hatua Tatu (katika kipengele
cha Habari Ndio Hii).
katika utafiti huo, nimebaini mambo mengi ambayo yanaweza
kuzorotesha ama kupunguza jitihada zinazofanywa na taasisi mbalimbali za
kiserikali na zisizo za kiserikali katika kupambana na matukio ya aina
hiyo.
Uchunguzi umebaini kwamba, baadhi ya matukio ya ubakaji, ulawiti na
ndoa za utotoni yanafanywa na watu wa karibu na watoto hao huku wakati
wengine baba, kaka ama wajomba wakihusika moja kwa moja!
“Kila mmoja wetu huko mitaani ambako watoto wanakuwa wanacheza
inabiti tuwajibike katika kuwa walinzi wazuri wa watoto wetu kwa sababu
tafiti zetu zinaonyesha matukio ya ulawiti na ubakaji kwa kiwango
kikubwa yanafanywa na watu wa karibu na watoto hawa wakiwemo akina baba,
wajomba na hata kaka.” Aliwahi kunukuliwa Mkurugenzi wa Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu, Hellen Kijo-Bisimba.
Kijo-Bisimba ambaye kitaaluma ni mwanasheria, akiongea na Times Fm,
alisema jamii inalazimika kutambua umuhimu wa watoto na kuwalea
kimaadili sambamba na kuwapa elimu bora kwa faida yao na taifa kwa
ujumla.
Aidha, taarifa ambazo Times Fm ilizipata mwaka jana kuhusiana na
ukubwa wa matukio ya ulawiti na ubakaji kwa mkoa wa Ilala, watoto zaidi
ya 176 walibakwa na kunajisiwa, mkoa wa Temeke walikuwa watoto zaidi
209 huku mkoa wa Kinondoni wakilawitiwa na kubakwa watoto zaidi ya 197!
Hata hivyo, takwimu hizo ni zile ambazo kesi zake zilifikishwa
Mahakamani achilia mbali zile ambazo ziliripotiwa katika vituo vya
polisi na kushughulikiwa kindugu!
Kwa mujibu wa Makamanda wa polisi wa mikoa husika, Temeke, Ilala na
Kinondoni, jitihada na elimu bado inaendelea kutolewa ndani ya jamii
katika kuelewa umuhimu wa mtoto lakini pia wazazi na walezi kuachana na
matukio hayo!
“Imani za kishirikina ni moja ya changamoto ambayo inachangia kwa
kiasi kikubwa sana matukio ya wazazi na walezi kufanya ngono na watoto
wao, awali imani hizi zilikuwa nyingi zaidi mikoani lakini sasa
changamoto hii imekuja hadi jijini Dar es Salaam hususani ndani ya mkoa
wangu wa Ilala lakini kama jeshi la polisi tutambana na imani hizi
katika kupunguza ama kumaliza tatizo hili.
“Kikubwa hapa tunachokiona baada ya uchunguzi wetu ni elimu tu ndani
ya jamii kujitambua, lakini pia kupitia upya uhalali wa ufanyajikazi kwa
hawa ndugu zetu wa tiba asilia (waganga wa kienyeji), baada ya kupitia
vibali vyao nadhani tutajua tatizo lipo wapi na vipi tunaweza kupunguza
ama kumaliza,” RPC wa Ilala, Marietha Minangi alinukuliwa alipokuwa
akizungumza na Times Fm.
Uchunguzi nilioufanya kwa hisani ya Times Fm na kuthibitishwa na
Kamanda Minangi, Mkoa wa Ilala ni miongoni mwa mikoa iliyoathirika zaidi
na matukio ya ubakaji sambamba na ndoa za utotoni.
“Pamoja na uwepo wa matukio hayo, jeshi langu kwa kushirikiana na
mmamlaka zinazohusika tumejitahidi kupambana nayo katika kuleta usawa
miiongoni mwa jamii na ustawi wao kwa ujumla,” Minangi alisema.
Sehemu ambazo zinaonekana kuathirika zaidi na ndoa za utotoni ndani
ya mkoa wa Ilala ni pamoja na Gongo la Mboto, Kivule, Chanika, Kinyerezi
na Kitunda.
Hakika, huu ni mwiba ndani ya jamii ya watanzania na unapaswa
kutolewa kwa juhudi zote bila kujali uhusiano wa watenda makosa ya aina
hii.
- TimesFm
إرسال تعليق