Mwandishi alitembelea masoko kadhaa katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar na Shinyanga jana na kubaini kuwa bei za vyakula, zimepanda maradufu mara tu baada ya Mfungo kuanza juzi.
Masoko yaliyotembelewa jijini Dar es Salaam ni Buguruni, Tandale, Kariakoo, Urafiki na Makumbusho.
Viongozi mbalimbali akiwemo Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salam, Alhad Mussa Salum walikemea hatua hiyo ya kupandisha bei ya vyakula.
Ilibainika kuwa vyakula ambavyo bei yake imepanda ndani ya siku mbili zilizopita ni zile zinazotumiwa kwa futari, ikiwemo muhogo, viazi , ndizi, magimbi, mchele na vinginevyo ambapo tofauti na siku za nyuma kwa sasa uuzwaji wake umekuwa wa tofauti.
Ukichukulia mfano wa viazi vitamu na muhogo, fungu ambalo kabla ya kuanza kwa Mwezi Mtukufu, lilikuwa likiuzwa kwa Sh 1000, hivi sasa limepandishwa na bei hadi kufikia Sh 2000.
Pia, mkungu wa ndizi uliokuwa ukiuzwa kwa Sh 6,000 hadi 7,000 kwa sasa umepanda bei hadi kufikia Sh 10,000, jambo linaloashiria limechangiwa na mahitaji makubwa ya wanunuzi.
Wakizungumza na mwandishi kuhusu hali hiyo, baadhi ya wafanyabiashara katika soko maarufu la vyakula la Urafiki, walikiri kupanda kwa bidhaa hizo. Pia, walisema hatua hiyo imesababishwa na uhaba wa vyakula hivyo kwa sasa.
“Ukiangalia ndani ya wiki hii, hakuna bidhaa iliyoletwa hapa ikakaa zaidi ya siku mbili, siyo kwa vyakula hivyo tu, bali hata matunda, inaonekana watu walianza kufanya maandalizi ya mapema ya kujiandaa na Mfungo wa Ramadhani,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao, aliyejitambulisha kwa jina moja la Hussein.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa mchele katika Soko la Tandale, Pascal Swai alisema kwa kiasi fulani bei ya bidhaa katika soko hilo, imepanda. Lakini, alisema hali hiyo haijachangiwa na Mfungo wa Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumzia hali hiyo, Sheikh Salum aliwataka wafanyabiashara hao kuachana na tamaa ya kupandisha bei ya bidhaa hizo ili kujiepusha na dhambi zisizo za lazima.
Badala yake, aliwahimiza watende wema kwa kupunguza bei ili waweze kuchuma thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik alisema amesikitishwa na jambo hilo. Aliwataka wafanyabiashara hao, kumrejea Mungu kwa kushusha bei ya bidhaa hizo ili wananchi waweze kupata mahitaji yao katika hali ya kawaida.
Alisema inashangaza kuona bei za vyakula hivyo kupandishwa, licha ya mwaka huu kuwa wa neema ya vyakula vya kutosha, tofauti na mwaka jana, hivyo haoni sababu ya msingi kutokana na hali hiyo.
“Japokuwa kwa sasa nipo likizo huku Mwanza, lakini kutokana na umuhimu wa suala hilo, inanibidi nitoe wito kwa wafanyabiashara, ni vyema wakaepuka kujiingiza katika mtego wa kuchuma dhambi kwa kutaka faida ya haraka ambayo pengine wasingeipata kama watafuata taratibu,” aliongeza Sadik.
Huko Shinyanga, baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Shinyanga, wamewalalamikia wafanyabiashara wa viazi na muhogo katika Soko la Nguzo Nane kwa kupandisha bei za vyakula.
Wananchi hao walisema tamaa ya wafanyabiashara ya kutaka kupata faida mara mbili, inawaumiza wananchi kwa vile uwezo wa kununua bidhaa za vyakula kwa bei hizo ni mdogo, hali inayowafanya watu waliofunga wasifunge kwa amani.
Katika soko hilo, fungu la muhogo ambalo awali lilikuwa likiuzwa Sh 1,000, wafanyabiashara wamepunguza idadi yake, na kuuza kwa bei hiyo hiyo ya 1,000. Hali hiyo inawapa wakati mgumu wananchi, kutokana na gharama za maisha kupanda.
Ibrahimu Kondo na Hawa Makune, wote wakazi wa Kambarage, walisema hali hiyo imekuwa kero kubwa kwao, kwani imefanya watumie gharama kubwa, tofauti na awali.
Waliitaka Serikali kudhibiti wafanyabiashara wanaopandisha bei katika kipindi hiki. “Mwezi Mtukufu ulipoanza tu, kumekuwa na mabadiliko makubwa ya bei ya vyakula hasa mihogo,viazi na magimbi."
Kondo alisema wafanyabiashara wanawapunja muhogo, minne mpaka mitano kwa kuwauzia Sh 1,000. Alisema fungu hilo la muhogo, halitoshi kwa familia ya watu watatu kufuturu.
Baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo, Mwantumu Almas na Juliana Clement, walisema wanalazimika kupunguza ukubwa wa mafungu, kutokana na kuuziwa bei kubwa na wakulima.
Walisema awali walikuwa wakinunua mfuko kati ya Sh 8,000 hadi 9,000, lakini sasa imefikia mpaka Sh 16,000 huku magimbi gunia likiuzwa kwa Sh 70,000.
Kwa upande wake, Balozi wa Wafanyabiashara katika Soko la Nguzo Nane, Hassan Juma, alisema gunia la viazi awali liliuzwa kwa Sh 40,000, lakini hadi jana gunia hilo lilikuwa linauzwa kwa Sh 60,000.
Alitoa mwito kwa wakulima, washushe gharama hizo ili na wao washushe bei ili wasiendelee kuwaumiza wananchi waliofunga.
Huko Zanzibar, bei ya vyakula vya futari ambavyo vinatumika katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, zimepanda juu, hivyo kuwapa wakati mgumu Waislamu, wanaotekeleza ibada hiyo.
Vyakula ambavyo vimepanda bei ni muhogo, ndizi na magimbi, ambavyo bei yake imeongezeka mara mbili.
Fungu moja la magimbi linauzwa kati ya Sh 5,000 wakati mkungu wa ndizi aina ya Sunuha, unauzwa Sh 15,000. Bei ya ndizi ya mkono mmoja, ambayo hupikwa zaidi ikiwa mbivu, bei yake imeongezeka maradufu na kufikia Sh 20,000 kwa mkungu mmoja, ambapo kwa dole moja huuzwa kati ya Sh 2,000.
Bei ya nazi ambazo hutumika kwa wingi katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, bei yake inaanzia Sh 1,000 kwa nazi moja.
Ofisa wa Soko Kuu la Mwanakwerekwe mjini hapa, ambalo linaongoza kwa kupokea bidhaa nyingi za vyakula, Said Juma, alisema bei ya vyakula inatarajiwa kupungua, kutokana na soko hilo kupokea aina mbalimbali ya vyakula kutoka Tanzania Bara.
Juma alisema vyakula vinavyotarajiwa kuingia katika soko hilo ni muhogo,viazi vikuu na maboga kutoka Mkoa wa Pwani.
Bidhaa nyingine zinatarajiwa kuingia Zanzibar kutoka Mkoa wa Tanga, kama vile muhogo, ambao umepata umaarufu mkubwa kwa ladha yake nzuri.
"Soko letu la Mwanakwerekwe linatazamia kupokea aina mbalimbali ya vyakula kutoka Tanzania Bara, ambavyo vitasaidia kushuka kwa bei ya vyakula vingine vinavyozalishwa nchini," alisema.
Aidha, alisema Soko Kuu la Mwanakwerekwe tayari limeanza kupokea kiwango kikubwa cha ndizi na muhogo kutoka Pemba.
Mfanyabiashara mmoja katika soko la Mwanakwerekwe aliyejitambulisha kwa jina la Iddi Haji, alisema baadhi ya bidhaa ikiwemo nazi, bei yake imekuwa ikipanda, kutokana na uhaba unaotokana na ukataji wa minazi kila siku kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kuishi.
Wakati huo huo, ikiwa ndio siku ya kuanza kutumika kwa ushuru mpya kwenye bidhaa, tayari wafanyabiashara wa jumla na rejareja wa bia wameshapandisha bei.
Utafiti uliofanywa na mwandishi mwishoni mwa wiki, ulibaini kuwa bei ya bia kwa reja reja, imepanda kati ya Sh 200 hadi 500 kwa bia za ndani na kwa zaidi ya Sh 1,000 kwa pombe kali na mvinyo.
Wauzaji wa jumla wameongeza bei kwa wastani wa Sh 5,000 hadi 10,000 kwa kreti.
Mmoja wa wamiliki wa maduka yanayouza bia katika eneo la Sinza, Godfrey Mushi alisema amelazimika kuongeza bei hata kabla ya muda wa utekelezaji wa marekebisho ya ushuru, kutokana na wauzaji wa jumla kupandisha bei.
“Nimezunguka maeneo mengi kwenye maduka ya jumla ili kupata bia za bei nafuu, lakini kote huko wamepandisha, hivyo nami nimelazimika kupandisha,” alisema.
Alipoulizwa kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Sheria wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Steven Kilindo alisema wateja wa bia zinazotengenezwa na kampuni yake, wana haki ya kukataa nyongeza ya bei, inayotolewa na wafanyabiashara.
Alisema mabadiliko ya bei, kwa kawaida yanatolewa kwa wafanyabiashara na umma, kwa kutoa bei elekezi.
“Mawakala wa mauzo wanaelimisha wafanyabiashara kufuata bei itakayotolewa. Ikiwa bei imepanda wakati hatujatangaza mabadiliko rasmi, basi wafanyabiashara wanakosea. Wateja wana haki ya kukataa kulipa bei yoyote ambayo sio rasmi,” alisema.
Aidha, Kilindo alisema kwa sasa TBL bado haijatangaza bei mpya ;na itafanya hivyo baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuangalia athari ya ongezeko la ushuru.
Meneja Mahusiano ya Ndani wa Kampuni ya Bia ya Serengeti, Imani Lwinga, alisema mpaka sasa bado hawajatangaza bei mpya za bidhaa zao mpaka hapo taratibu zitakapokamilika.
“Pamoja na kuwa ushuru umepanda, lakini mpaka sasa hatujatangaza kupanda kwa bei, kinachosubiriwa ni taratibu kufuata na ndipo tutakapoutangazia umma bei zetu mpya,” alisema.
Serikali ilipandisha ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa (unmalted), mfano kibuku, kutoka Sh 341 kwa lita hadi Sh 375 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 34 kwa lita ; na ushuru wa bia nyingine zote kutoka Sh 578 kwa lita hadi Sh 635 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 57 tu kwa lita.
Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu, inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 imepanda kutoka Sh 160 kwa lita hadi Sh 176 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 16 tu kwa lita.
Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu, inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka Sh 1,775 kwa lita hadi Sh 1,953 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 178 kwa lita. Ushuru wa vinywaji vikali kutoka Sh 2,631 kwa lita hadi Sh 2,894 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 263 kwa lita.
إرسال تعليق