CHADEMA YATULIZA WANANCHI, YAAHIDI KATIBA MPYA ITAPATIKANA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Katiba mpya ya Tanzania itapatikana na kusisitiza kuwa suala la kundi la wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba linalounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurejea bungeni, linategemea utekelezaji wa masharti yao.
Bunge Maalumu la Katiba linatarajia kuendelea na vikao vyake Agosti 5 mwaka huu baada ya kuahirishwa Aprili 25 mwaka huu, kupisha shughuli za Bunge la Bajeti la Jamhuri ya Muungano na lile la Wawakilishi, Zanzibar.
Sambamba na hilo, Chadema baada ya kufuta na kuahirisha uchaguzi wake wa ndani kwa mara kadhaa, imetangaza kuendelea na hatua hiyo na kuweka wazi kuwa, haitasita kufuta uchaguzi pale itakapobaini kuna ukiukwaji wa Katiba yake katika mchakato huo.
Katika uchaguzi huo, mapema Septemba mwaka huu, nafasi za juu za uongozi ikiwemo ya mwenyekiti inayoshikiliwa hivi sasa na Freeman Mbowe tangu mwaka 2004 na ya katibu mkuu aliyoko Dk Slaa aliyeshika nyadhifa kadhaa za juu tangu mwaka 2000, itapata ama viongozi wapya au wenye nazo kuendelea.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliwaambia waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam kuwa Katiba mpya kwa Watanzania itapatikana lakini ikiwa mchakato mzima hautagubikwa na matakwa binafsi na ubabe.
"Huwezi kupata Katiba nzuri kwa mfumo unaoendelea sasa, kwa sababu ni ubabe
unaendelea. Na kuna waraka umeandaliwa kuhusu mwenendo wa katiba..." alisema Dk Slaa bila kufafanua kuhusu waraka huo.
Alisema suala la Ukawa kurejea bungeni linawezekana, lakini msimamo wao uko pale pale katika kutimiziwa masharti yao waliyotoa.
Miongoni mwa madai ya Ukawa kutoka nje ya Bunge ni kutoridhishwa na mwenendo mzima wa vikao vya Bunge hilo; kudai Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeteka mchakato wa Katiba; kutaka kujadiliwa kwa rasimu iliyoletwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kumekuwepo na jitihada za kuwasihi Ukawa warudi bungeni zikifanywa na uongozi wa Bunge hilo Maalumu akiwemo Spika wa Bunge hilo, Samuel Sitta, viongozi wa kidini na serikali akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na viongozi wengine.
Dk Slaa katika mkutano huo wa jana, alisema wanaowataka Ukawa warudi bungeni
ili wakajenge hoja waelewe kwamba hakuna hoja zinazojengwa.
"Chadema haitavumilia uongo…, tunaomba viongozi wa madhehebu ya dini watuelewe, sisi hatutavumilia uongo. Tunaamini Katiba ya Tanzania itapatikana hata kama si leo," alisema Dk Slaa.
Alisema anashangaa kuona viongozi wa Ukawa wakitakiwa kuhudhuria kikao cha kamati ya maridhiano wakati wapo nje na kwamba, kwanza wanatakiwa kufahamu kama watarudi bungeni.
"Watu wetu wa Ukawa hawatahudhuria kamati hiyo kwa sababu walitakiwa kufahamu kwamba je, watu hao watarudi bungeni au hawatarudi ndio waendelee, lakini msimamo wa watu wetu watarudi endapo masharti yatafikiwa, je yamefikiwa?" Alihoji Dk Slaa.
Kuhusu uchaguzi ndani ya chama hicho, alisema chama kinaendelea na uchaguzi katika ngazi za majimbo na wilaya hadi taifa.
Alisema tangu mwaka 2004 wamekuwa wakizunguka nchi nzima na wameweza kuunda kanda 10 zilizofanikisha kupatikana kwa mabalozi wa nyumba kumi nchi nzima na kwamba kwa sasa wana matawi 16,000 na wenyeviti wa vitongoji 196,000 nchini, kuacha  mikoa ya Mtwara na Lindi ambayo hawakuruhusiwa kufika.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, uchaguzi ngazi ya majimbo na wilaya unaendelea tangu Juni 26 hadi Julai 18 mwaka huu na kipindi cha rufaa ni hadi Agosti 2. Agosti 3 ni uchaguzi ngazi ya mkoa na Agosti 22 na 26 ni maandalizi ngazi ya Taifa.
Dk Slaa alisema Agosti 27 wataanza mchakato wa uchaguzi mkuu ngazi ya Taifa utakaofanyika kwa siku tano. Alisema siku hiyo pia utafanyika uchaguzi wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) na Wazee. Agosti 28 utafanyika uchaguzi wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha).
Aidha, Dk Slaa alisema Agosti 29 itakutana Kamati Kuu ya kwanza na Agosti 30 litakutana Baraza Kuu linalomaliza muda wake. "Agosti 31 utafanyika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi ambapo atachaguliwa Mwenyekiti Taifa na Makamu Mwenyekiti wawili wa upande wa Bara na wa Zanzibar".
Alisema Septemba mosi litakutana Baraza Kuu jipya litakalochagua Katibu Mkuu na
manaibu wake wawili pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu na Septemba 2 itakutana Kamati Kuu mpya.

Post a Comment

أحدث أقدم