KIUNGO na beki wa timu ya Taifa ya Tanzania,
Shomary Kapombe amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao
dhidi ya Msumbiji `Black Mambas` katika
mechi muhimu ya kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza
fainali za mataifa ya Afrika, AFCON, mwakani nchini Morocco.
Mchezaji huyo kiraka alisema wachezaji 11
wanaocheza uwanjani hawatoshi kupata ushindi, hivyo mashabiki kama wachezaji wa
12 wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuishangilia Taifa Stars.
“Napenda kuwaambia watanzania wote kuwa huu ni
mchezo muhimu, nawaomba watanzania waje kuisapoti timu”. Alisema Kapombe.
Aidha, Kapombe aliongeza kuwa kambi waliyoweka
Mjini Tukuyu mkoani Mbeya imekuwa ya mafanikio kwasababu wachezaji wote wapo
katika morali ya kufanya vizuri katika mchezo wa kesho.
Kapombe alisema kocha Mart Nooij amewabadili
katika baadhi ya mambo kiuchezaji na ufundi licha ya kukaa na timu kwa muda
mfupi.
Aliongeza kuwa kocha Nooij alikuwa anakazania
zaidi safu ya ulinzi kwasababu ndio inafanya kazi kubwa zaidi katika mchezo.
Taifa stars inahitaji kuifunga Msumbiji si chini
ya mabao 3-0 ili kujiweka vizuri kuelekea mchezo wa marudiano utakaopigwa mjini
Maputo nchini Msumbiji.
Mwaka 2007, Mambas waliifunga Stars bao 1-0 katika
mchezo wa kuwania kufuzu fainali za AFCON mwaka 2008 nchini Ghana na mechi hiyo
ilipigwa ndani ya dimba la Taifa.
Miaka miwili iliyopita, Stars ililazimishwa sare
ya bao 1-1 katika dimba la Taifa na kwenda kutoa sare nyingine Mjini Maputo,
lakini kikosi hicho kilichokuwa chini ya kocha Kim Poulsen kiliondolewa kwa
mikwaju ya penati.
Mechi hiyo ilikuwa ni kuwania tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2013 nchini Afrika kusini.
Post a Comment