KAPOMBE AWAANGUKIA WATANZANIA AKITAKA WAJITOKEZE KWA WINGI KUISHANGILIA TAIFA STARS IKIICHAKAZA MAMBAS


KIUNGO na beki wa timu ya Taifa ya Tanzania, Shomary Kapombe amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao dhidi ya Msumbiji `Black Mambas`  katika mechi muhimu ya kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika, AFCON, mwakani nchini Morocco.
Mchezaji huyo kiraka alisema wachezaji 11 wanaocheza uwanjani hawatoshi kupata ushindi, hivyo mashabiki kama wachezaji wa 12 wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuishangilia Taifa Stars.
“Napenda kuwaambia watanzania wote kuwa huu ni mchezo muhimu, nawaomba watanzania waje kuisapoti timu”. Alisema Kapombe.
Aidha, Kapombe aliongeza kuwa kambi waliyoweka Mjini Tukuyu mkoani Mbeya imekuwa ya mafanikio kwasababu wachezaji wote wapo katika morali ya kufanya vizuri katika mchezo wa kesho.
Kapombe alisema kocha Mart Nooij amewabadili katika baadhi ya mambo kiuchezaji na ufundi licha ya kukaa na timu kwa muda mfupi.
Aliongeza kuwa kocha Nooij alikuwa anakazania zaidi safu ya ulinzi kwasababu ndio inafanya kazi kubwa zaidi katika mchezo.
Taifa stars inahitaji kuifunga Msumbiji si chini ya mabao 3-0 ili kujiweka vizuri kuelekea mchezo wa marudiano utakaopigwa mjini Maputo nchini Msumbiji.
Mwaka 2007, Mambas waliifunga Stars bao 1-0 katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za AFCON mwaka 2008 nchini Ghana na mechi hiyo ilipigwa ndani ya dimba la Taifa.
Miaka miwili iliyopita, Stars ililazimishwa sare ya bao 1-1 katika dimba la Taifa na kwenda kutoa sare nyingine Mjini Maputo, lakini kikosi hicho kilichokuwa chini ya kocha Kim Poulsen kiliondolewa kwa mikwaju ya penati.

Mechi hiyo ilikuwa ni kuwania tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2013 nchini Afrika kusini.

Post a Comment

أحدث أقدم